Prime
Ujumbe wa Moses Phiri Simba akiitaja dabi

Muktasari:
- Nyota huyo anasema hajaona tofauti ya wazawa na wageni kwani licha ya wageni kutajwa sana lakini hata wazawa wana ubora uwanjani na wanazibeba timu zao.
MOSES Phiri ni miongoni mwa majina yaliyoangaziwa sana katika usajili wa wachezaji miaka ya karibuni kabla ya kutua nchini, yakihusishwa na Simba pamoja na Yanga.
Hata hivyo, Simba ndiyo iliyoshinda vita ya kumsajili mshambuliaji huyo kutoka Zanaco ya Zambia msimu wa 2022/23.
Bahati mbaya maisha yake Msimbazi hayakwenda kama ilivyotarajiwa na wengi na alijikuta akiishia kuandamwa na majeraha na mara kadhaa alizocheza hakuwakosha kiviiile mashabiki wa timu hiyo kiasi cha kuishia kuondoka Bara na kurejea nchini kwao alikojiunga na Power Dynamos, kisha akatimkia zake Nkana Red Devils aliko hadi sasa.
Hata hivyo, straika huyo amezungumza na Mwanaspoti na kueleza kwa usajili wa sasa Simba imelamba dume kutokana na kujaza vijana kikosini, huku akiutaka uongozi na benchi la ufundi kuwalinda wachezaji hao.
Katika mahojiano hayo anasema Tanzania anaichukulia kuwa ni nyumbani kutokana na kufanya kazi kwa sapoti kubwa.
USAJILI SIMBA
Phiri amegusia usajili na mastaa wapya Simba na anaamini uwepo wa vijana wengi na wakikaa kwenye mfumo wa Kocha Fadlu Davis kwa muda mrefu watafanya mambo makubwa.
"Unaposajili vijana wengi klabu inakuwa inatengeneza timu itakayokaa muda mrefu, kwani kadri muda uvyokwenda ndivyo wanavyozoeana," anasema.
"Kabla ya sisi kujiunga na Simba ambayo ilikuwa inachukua mataji mfululizo, ilikuwa na wachezaji wanaoelewana kiuchezaji. Ndiyo maana ilikuwa rahisi kwao kufanya vizuri, hivyo waliopo sasa ni wao kujua majukumu yao na malengo ya klabu wakiamua kupambana wataandika rekodi zao."

WAZAWA, WAGENI
Nyota huyo anasema hajaona tofauti ya wazawa na wageni kwani licha ya wageni kutajwa sana lakini hata wazawa wana ubora uwanjani na wanazibeba timu zao.
Anasema ni mtazamo tu wa watu wageni wana ubora ingawa yeye anaona wote ni sawa akitolea mfano baadhi ya nyota wazawa wanaofanya vyema.
"Kuna wazawa ambao wanafanya vizuri kama Shomari Kapombe, Mohamed Hussein 'Tshabalala', John Bocco, Beno Kakolanya, Aishi Manula, Feisal Salum 'Fei Toto' na wengine wengi. Wana nidhamu na kazi zao. Binafsi sijaona tofauti zaidi ya mitazamo ila viwango ni vile vile," anasema.
"Unapocheza ugenini huwezi kujiendekeza kwa sababu tunakuwa tumeziacha familia nyumbani zinazotutegemea. Hivyo, ni lazima nitapambana na akili inatanuka, nitaongeza juhudi ya mazoezi ili kupata nafasi ya kucheza."
DABI HAIZOELEKI
Anasema mechi zote walizocheza dhidi ya Yanga zilikuwa bora kutokana na ushindani ulivyokuwa pamoja na mapokeo ya mashabiki yaliyomfanya awe na moyo wa kuipambania timu ili kuhakikisha anawapa furaha.
"Dabi ya Simba na Yanga hazizoeleki mashabiki wanakuwa na matokeo yao yakija vinginevyo unakuwa ni wakati mgumu kwa wachezaji, viongozi na makocha, siyo jambo la mchezo unasikia watu wamezimia ama wanalia, inagusa moyo," anasema.

MAISHA YAKE SIMBA
Phiri anasema alikuwa na wakati mzuri Simba hasa msimu wake wa kwanza wa 2022/23 aliomaliza akiwa na mabao 10 na alionyesha kiwango cha juu katika mashindano mbalimbali klabuni hapo.
"Isingekuwa kuumia ningemaliza na zaidi ya mabao 10, huenda ningeingia kuwania kiatu cha ufungaji na Fiston Mayele na Saido Ntibazonkiza ambao walimaliza na mabao 17. Niliufurahia ushindani ulivyokuwa mkubwa," anasema Phiri.
Anasema hakukaa muda mrefu Msimbazi kutokana na sababu za majeraha, akidai: "Ilifika wakati wa kuondoka na lilikuwa jambo zuri kwa kazi yangu, kwani mzunguko wa pili ambao sikuumalizia nilifunga mabao matatu, nilipitia majeraha ya hapa na pale na ni changamoto za kawaida katika kazi yetu."
Phiri anasema anakumbuka Simba ilimpa nafasi ya kuonyesha kipaji na kumkutanisha na watu wapya kama wachezaji, mashabiki, viongozi na makocha.
"Simba ni miongoni mwa klabu kubwa Afrika, mchezaji anapopata nafasi ya kuichezea anakuwa anaongeza thamani katika kazi yake. Ndivyo ilivyo pia na kwangu," anasema na kuongeza:
"Kupitia klabu hiyo wachezaji wazawa na wageni wameonekana na timu nyingine za nje ya Tanzania kutokana na ushiriki wake katika michuano ya CAF, hivyo anayefanya vizuri ni rahisi kupata dili."

WACHEZAJI WENZAKE
Mchezaji huyo anasema kila mchezaji aliyecheza naye Simba amebaki katika kumbukumbu ya maisha yake, kwani waliishi kwa upendo na kushirikiana katika majukumu.
"Wengi ni marafiki zangu kama Kakolanya, Bocco ambao wameondoka tayari; Kapombe, Tshabalala yaani ni wengi nawakumbuka na wengine nawasiliana nao. Maisha ya soka hayana uadui tunaweza kukutana sehemu nyingine," anasema.

MASHABIKI SIMBA, YANGA WANA MZUKA
Anasema Ligi Kuu Bara ina mvuto na ushindani, ingawa Simba na Yanga ndizo anazoziona zina wafuasi wengi ambao wananogesha soka kwa jinsi ambavyo wanazisapoti timu zao.
"Simba na Yanga zina mashabiki ambao wanapenda sana timu zao, wanawapa thamani wachezaji wao ambao inakuwa rahisi kupata umaarufu kama wakiwa wanafanya vizuri," anasema.
"Sitawasahau mashabiki wa Simba katika maisha yangu. Walinisapoti katika nyakati ngumu na zenye furaha, walitamani kila wakati wanione nacheza, ilinipa nguvu kujituma kwa ajili yao. Bado nawapenda na kuwaona wanakuwa na furaha Simba inapofanya vizuri."

AIPELEKA SIMBA FAINALI
Phiri anasema anapopata muda anapenda kuiangalia Simba ikicheza, hivyo anaiona itafika mbali katika Kombe la Shirikisho Afrika (CAF), huku akiwataka wachezaji kujituma na kuwa na moyo wa kujitolea itakuwa silaha yao ya kutinga fainali.
"Simba ina uzoefu wa kufanya vizuri katika michuano ya CAF nina uzoefu na hilo. Nimecheza kwa mafanikio nikiwa nayo, kikubwa wachezaji wajenge moyo wa kujitolea kwa ajili ya timu yao hakuna ambalo litashindikana," anasema Phiri.
Simba itakabiliana na Al Masry ya Misri katika mchezo wa robo fainali kuwania kutinga nusu fainali ya kombe hilo.

MAISHA YA TANZANIA
Mchezaji huyo anasema Tanzania ni nchi ya amani na watu wake ni wakarimu na upendo, ingawa haitofautiani sana na Zambia.
"(Tanzania) unatembea kwa uhuru, watu wake wana upendo, mchezaji ukifanya vizuri unapewa zawadi, unapata huduma kirahisi. Kiukweli kuna namna ambavyo thamani inakuwa kubwa kwetu kama wachezaji," anasema Phiri.
Msimu uliopita akitokea Simba alifunga mabao mawili katika mechi mbili za Power Dynamos na sasa yupo Nkana Red Devils.