Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mwamnyeto, tunachukia kumpenda na tunapenda kumchukia


KAPTENI Nondo ni rafiki yangu. Hana baya. Bakari Mwamnyeto. Beki mzuri mwenye makosa machache lakini watu wanasubiri akosee zaidi kuliko kupatia. Akipatia wanakaa kimya. Juzi kafunga bao zuri dhidi ya Mashujaa pale Kigoma watu wamekaa kimya.


Mara ya pili hii anafunga. Beki wa kati aliyefunga mabao mawili katika lango la timu pinzani. Mabao ambayo siyo ya faulo. Mara nyingi walinzi wa kati huwa wanafunga katika kona au mipira ya faulo. Mwamnyeto amefunga katika katika mchezo wa wazi (open play). Zaidi ya hayo ni beki mzuri kwa jumla yake. Mrefu, anakaba vema na ana makosa machache kuliko inavyosemwa.

Alikuwa mchezaji wetu bora katika michuano ya kombe la mataifa ya Afrika pale Morocco mapema mwaka jana. Watu walimshangaa kwa uwezo wake mkubwa alionyesha katika mechi zake. Sasa hivi amerudi klabuni kwake lakini mashabiki zake hawamuamini sana. Alijifunga katika pambano la hivi karibuni dhidi ya Dodoma Jiji na ikawa nongwa kwa mashabiki wa timu yake.

Kapteni Nondo analazimika kuishi na mashabiki wa timu yake kama hivi. Wanapenda kumchukia na wanachukia kumpenda. Wanasubiri akosee. Huwa kuna wachezaji wa namna hii katika klabu kubwa. Ni wachezaji wazuri lakini mashabiki wanawatazama kwa jicho la chuki bila ya sababu za msingi. Ajabu ni Nondo ana muda mrefu anacheza Yanga. Inaweza kuwa misimu mitano sasa.

Anapoongeza mkataba hauoni mashabiki wakichukia kwa sababu wanajua ni mchezaji mzuri. Kwa nini hawamlaumu Injinia Hersi Said wakati Yanga wanapotangaza wameongeza mkataba wa Mwamnyeto? Ukweli ni wanajua ni mchezaji mzuri. Tatizo kubwa la mashabiki wetu ni kuchagua kutomsapoti mchezaji fulani. Majuzi aliomba hadi apumzishwe baada ya kujifunga dhidi ya Dodoma Jiji.

Mara ngapi amekuwa akihusishwa kujiunga na timu mbalimbali kubwa za ndani hasa Simba? Mara kibao. Mkataba wake unapokaribia kumalizika utasikia anahusishwa na Simba. Ni kwa sababu kwa ujumla wake ni beki mzuri. Makosa ya hapa na pale yapo lakini kwa jumla ni beki mzuri na ndiyo maana Hersi na wenzake huwa wanamwongezea mkataba kila kukicha.

Jambo jingine ambalo mashabiki wanalisahau ni ukweli kando ya watu anaocheza nao Dickson Job na Ibrahim Bacca yeye ni miongoni mwa mabeki bora wa kati. Nenda katika timu nyinginezo kama utakutana na beki kama Mwamnyeto. Huwa tunaangalia makosa yake machache kuliko kujiambia ukweli wachezajj wetu wengi wa ndani ni wa kawaida tu.

Ziangalie timu nyingi kubwa hapa nchini. Zinategemea mabeki wa kati wageni kasoro Yanga. Wakati Simba iliokoa pesa kwa muda mrefu kwa walinzi wa pembeni Mohamed Hussein Tshabalala na Shomari Kapombe pamoja na langoni kuwa na Aishi Manula Yanga waliokoa pesa za kigeni kwa kuwa na mabeki wa kati wazawa wenye uwezo. Bakari Nondo Mwamunyeto na Dickson Job kabla ya kuibuka kwa Bacca.

Hapo katikati alipita Gift Fred lakini aliishia kuwa chaguo la nne kikosini. Wangeanza Bacca na Job kisha angeingia Kapteni Nondo. Baadae Gift ambaye haikueleweka amefikaje Yanga aliachwa na akarudi zake kwake Uganda kufurahia chakula cha matoke.

Kwa sasa Yanga wana beki wa kati wa kigeni anaitwa Frank Assinki. Katika muda huu ambao Job ameumia chaguo la kwanza la walinzi wa kati limebakia kwa Mwamnyeto na Bacca. Kwa nini sio Assinki? Makocha sio wajinga. Wanajua kapteni Nondo ni bora kuliko Assinki. Tuna wachezaji wetu wengi wazuri lakini tuna shida ya kuwaamini tu. Basi. Hakuna shida nyingine.

Wakati huu tukiwa na upungufu wa wachezaji wengi wazuri wazawa katika timu zetu kubwa nadhani Yanga wajifunze kumuamini na kumpenda kapteni Nondo. Kwanza kabisa Yanga wana bahati ya ajabu. Wana bahati ya kuwa na manahodha wanaokaa benchi na hawalalamiki wala kuigawanya timu.

Yanga waliwahi kuwa na Fred Mbuna. Alikuwa nahodha na kuna wakati alikuwa anakaa benchi. Hata hivyo, alikuwa na uvumilivu na aliweza kutimiza majukumu yake vema alipoitwa uwanjani. Na sasa wana Kapteni Nondo ambaye amekuwa hivyo hivyo. Vizazi vinabadilika, nilidhani hiki kizazi cha sasa kingejifunza.

Nadhani baadhi ya watu wabadili mtazamo wao kwa kapteni Nondo. Wasimzamishe katika bonde. Tuzingatie pia wamewekeza sana kwake. Sio rahisi kumpata mchezaji mzawa aliyecheza mechi nyingi za kimataifa kama yeye. Hii kwa lugha nyingine tunaita uwekezaji. Amecheza mechi nyingi za tinu ya taifa na zile za michuano ya CAF. Ni uzoefu ambao tunawekeza mara chache.

Mfano mzuri nilifurahi ujio wa Wilson Nangu alipotoka JKT kwenda Simba na akawa anacheza. Ni mara chache inatokea kama vile katika miaka ya karibuni. Bahati mbaya alipatwa na majeraha ambayo yanemfanya ashindwe kucheza kwa muda mrefu sasa. Tayari tulishapata ongezeko la mchezaji mwingine mzawa ambaye aliingia katika kikosi cha kwanza cha timu kubwa.

Baadhi ya watu wa Yanga waanze tu kujaribu kumpenda Kapteni Nondo. Kuna sababu nyingi za kufanya hivyo. Sababu nyingine ni ukweli yeye ni miongoni mwa wachezaji walioanza kuijenga Yanga mpya baada ya utawala wa muda mrefu wa Simba. Wakati GSM alipoanza kutia pesa za uhakika Yanga alianza kwa watu kama kina Kapteni Nondo. Wao ndio msingi wa Yanga imara ya leo.

Kabla ya hapo walikuwepo kina Vincent Bossou. Walikuwa walinzi wazuri lakini akina kapteni Nondo waliipeleka timu hadi katika fainali za michuano ya Shirikisho. Tujifunze kuwaheshimu wachezaji kama hawa. Kuna wakati vifua vyetu vinapaswa kuhimili na kustahimili maumivu machache yanayoletwa na mchezaji kukosea  uwanjani.

Lakini kama kuna Watanzania huwa wanamtukana Mbwana Samatta mchezaji ambaye ametuheshimisha kwa wazungu, sishangai sana kebehi anazopewa kapteni Nondo. Ndivyo waswahili tulivyo. Hatuna heshima dhidi ya watu waliowahi kutuheshimisha katika nyakati muhimu. Ndivyo tulivyo. Hata kwa kapteni Nondo tupo hivyo hivyo. Tunapenda kumchukia na tunachukia kumpenda.