Prime
Kila ongezeko la shindano linarefusha msimu
PAMOJA na kuongeza hamasa kwa mashabiki, uamuzi wa Shirikisho la Kimataifa la Soka (Fifa), kuongeza idadi ya timu katika mashindano yake mawili yaani fainali za Kombe la Dunia na Klabu Bingwa ya Dunia kuna lawama nyingi dhidi ya uamuzi huo na shauri hilo liko mahakamani.
Klabu na Umoja wa Wanasoka Dunia kwa pamoja zinadai uamuzi huo umeongeza idadi ya mechi na hivyo kuathiri mashindano mengine ya nchi na afya za wachezaji.
Leo hii wanasoka walioteuliwa kwenye timu za taifa zinazoshiriki fainali za Kombe la Dunia 2026 watakuwa na muda mfupi wa mapumziko kabla ya msimu mpya wa ligi duniani kuanza.
Hata uamuzi wa kuwapa muda zaidi wa kupumzika tofauti na wachezaji wengine, bado klabu zitaathirika kwa kukosa huduma za wachezaji zilizowanunua kwa bei mbaya.
Ligi za nchi zitaathirika kwanza kwa kukosa nyota hao mwanzoni mwa msimu au kuwapata wakati bado wana uchovu na pili kusababisha zibane mashindano yake ili kuendena na yale ya Fifa.
Si hivyo tu, kwenye ligi kubwa kama zile tano za Ulaya, vita inakuwa hadi kwa wadhamini kwa kuwa kampuni kubwa zinaweza kuwekeza zaidi katika mashindano ya dunia kuliko ya nchi.
Katikati ya hoja zote ni afya za wachezaji na ndiyo maana chama chao kilifungua kesi kupinga fainali za Klabu Bingwa ya Dunia, kikisema pamoja na uamuzi huo kuathiri afya za wachezaji, Fifa haikukishirikisha katika mchakato wa kufikia uamuzi huo.
Sisi kwetu hatuna hoja nyingi dhidi ya uamuzi huo kwa sababu si nyota wetu tu, hata wale tunaowanunua kutoka nje bado hawamo kwenye vikosi vya nchi zao vinavyoshiriki Kombe la Dunia licha ya Afrika kupeleka timu 10 mwaka huu, jambo ambalo ni rekodi.
Lakini kuna mambo tunayoyafanya yanayolingana na kiburi hicho cha Fifa.
Miaka michache iliyopita tuliongeza idadi ya timu katika mechi za Ngao ya Jamii kutoka mbili hadi nne. Hili ni onghezeko kubwa kwa timu zinazoshiriki na pili uamuzi huo unaongeza idadi ya mechi katika msimu na kuufanya kuwa mrefu tofauti na awali.
Kama vile haitoshi, tukaongeza mashindano ya Ligi ya Muungano ambayo ni kama mechi za kirafiki kwa kuwa hazilengi kupata mwakilishi kwenye mashindano yoyote yale ya Afrika, tofauti na ilivyokuwa awali wakati bingwa alikuwa akishiriki Ligi ya Mabingwa Afrika
Hili pia limeongeza idadi ya mechi na kuurefusha msimu na hivyo kuongeza uchovu kwa wachezaji.
Zaidi ya hayo, tuna mashindano ya Kombe la Mapinduzi ambayo ni kama lazima kushiriki na kutumia vikosi vya kwanza kwa ajili ya kujijengea heshima. Awali, klabu zilikuwa zinatumia wachezaji ambao hawapati nafasi kwenye vikosi vya kwanza lakini ushabiki umewafanya viongozi kutuma vikosi kamili.
Bado tuna Ligi Kuu, Championship na nyingine, huku tukiwa na Kombe la TFF, maarufu kama Kombe la Shirikisho (FA).
Hapa katikati timu ya taifa itaitwa kwa mechi za kirafiki zilizo ndani ya siku za Fifa na zile mashindano na hivyo kusababisha ligi za ndani kusimama hadi Taifa Stars imalize majukumu yake kimataifa.
Licha ya yote hayo, bado kuna mashindano ya kimataifa ya klabu; Ligi ya Mabingwa na Kombe la Shirikisho. Tukiwa na timu zinazojikakamua hadi hatua ya makundi, maana yake tutakuwa na maombi ya kila mara ya kuahirisha mechi ili kuzipa muda wa kujiandaa na kusafiri. Na timu zikiwa nne, ndio kabisa ratiba inavurugika, hasa kutokana na unyonge wa wasimamizi kukubali maombi ya kuahirisha mechi ovyo na kutojipanga vizuri kuhakikisha ratiba inazingatia zile za mashindano ya Afrika.
Kwa hiyo, si ajabu sana kuona dunia inaelekea kuangalia fainali za Kombe la Dunia wakati nchi yetu ikihaha kumalizia msimu unaotakiwa uwe umemalizika mwezi Mei kama ilivyo sehemu nyingine duniani.
Muda ambao wachezaji wetu walitakiwa wawe mapumzikoni wakiungana na ndugu zao kwa masuala mengi ya kijamii, ikiwa ni pamoja na kushuhudia fainali za Kombe la Dunia, wao watakuwa viwanjani wakipambana kutafuta ushindi.
Muda ambao mashabiki watapenda kuelekeza fikra na macho yao kwenye Ligi Kuu na nyingine, akili zao zitalazimishwa kugeukia Marekani, Canada na Mexico ambako wenzao wote duniani watakuwa wakifuatilia na hivyo kufisha mijadala kuhusu timu zetu.
Ni kama vile wapangaji ratiba hawakujua mwezi Juni na Julai 2026 kutakuwa na fainali za Kombe la Dunia ambazo zingewafanya wahakikishe wanafanya kila jambo msimu kuisha mapema ili nchi ijielekeze kwenye mashindano hayo makubwa kuliko yote katika soka duniani.
Ni muhimu mamlaka zinazosimamia soka zianze kujifunza kutokea fainali za mwaka huu kila ongezeko la shindano linaongeza idadi ya mechi na kurefusha msimu. Kunahitajika umakini mkubwa katika kupanga na kusimamia mashindano na ni muhimu kujiwekea malengo kuwa msimu ni lazima uishe mfano mapema Juni mwakani na iwe ni sheria kama ilivyo bajeti ya nchi.