AFCON 2025: Wilfred Ndidi akabidhiwa kitambaa Super Eagles
Muktasari:
- Ndidi amepewa jukumu la kuwa nahodha wa Super Eagles, kufuatia kustaafu kwa William Troost-Ekong, aliyekiongoza kikosi cha taifa hilo tangu mwaka 2019, akicheza mechi zaidi ya 70.
Kiungo wa Leicester City, Wilfred Ndidi amekabidhiwa jukumu la kukiongoza kikosi cha Nigeria maarufu Super Eagles katika fainali za Mataifa ya Afrika (AFCON 2025) zinazotarajiwa kuanza Desemba 21, 2025 nchini Morocco.
Ndidi amepewa jukumu la kuwa nahodha wa Super Eagles, kufuatia kustaafu kwa William Troost-Ekong, aliyekiongoza kikosi cha taifa hilo tangu mwaka 2019, akicheza mechi zaidi ya 70.
Troost-Ekong alitangaza kustaafu kuichezea timu ya taifa ya Nigeria jana Alhamisi, Desemba, 04, 2025. Ndidi, ambaye aliiongoza Super Eagles katika mechi za kufuzu Kombe la Dunia 2026, sasa anachukua rasmi jukumu la unahodha.
Kiungo huyo atasaidiwa na winga Moses Simon, ambao kwa sasa ni miongoni mwa wachezaji wenye uzoefu zaidi katika kikosi cha Super Eagles.
Kwa mara ya kwanza Ndidi aliitwa kwenye kikosi cha Super Eagles Agosti 2015 na hadi sasa ameshacheza mechi 71. Kwa bahati mbaya, majeraha yalimsababishia kukosa nafasi ya kushiriki AFCON 2023 nchini Ivory Coast.
Katika AFCON 2025), Nigeria imepangwa Kundi C, ambapo itakutana na Tunisia, Uganda, na Tanzania. Kundi hili linatarajiwa kutoa ushindani mkali, huku kila timu ikiwa na lengo la kusonga hatua ya 16 bora.
Katika mechi ya ufunguzi Kundi C, Nigeria itaanza kampeni yake dhidi ya Tanzania Desemba 23, 2025 katika uwanja wa Complexe Sportif de Fès, mjini Fès. Hii itakuwa fursa muhimu kwa Nigeria kuweka msingi mzuri katika mashindano na kuonyesha uwezo wa kikosi chake chini ya uongozi wa Wilfred Ndidi kama nahodha mpya wa timu.
Mashindano ya AFCON 2025 yanatarajiwa kuangazia wachezaji wenye uzoefu pamoja na vipaji vipya, na Nigeria itakuwa na changamoto ya kuendeleza historia yake ya ushindi na kusonga mbele katika mashindano haya ya bara la Afrika.