Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Ugumu, Nafuu kwa Mbeya kwanza kutimkia Songea

Ugumu, Nafuu kwa Mbeya kwanza kutimkia Songea

Muktasari:

  • Mbeya Kwanza imecheza mechi nane uwanja wa Sokoine bila kushinda ikiambulia sare 4.

MBEYA. BAADA ya mambo kutoiaendea vizuri, Mbeya Kwanza imeukimbia Uwanja wa Sokoine na kusaka sehemu nyingine nafuu kwao ili kuweza kukwepa rungu la kushuka - itimkia mkoani Ruvuma.

Pamoja na uamuzi huo ambao kimsingi ni sahihi, lakini huenda ikakutana na changamoto nyingine ndani na nje ya uwanja.

Hoja ya kukimbia Sokoine ni kutokana na ishu ya matokeo kutokuwa mazuri kwani tangu waanze kuutumia uwanja huo uliopo jijini Mbeya hawajapata ushindi na kuzua maswali yenye kufikirisha.

Mwanaspoti linakuletea tamu na chungu katika kufikiwa kwa malengo ya timu hiyo msimu huu.


Historia ikoje

Pamoja na Mbeya Kwanza kutumia Uwanja wa Sokoine, lakini historia inaonyesha kuwa hawakuwa na matokeo mazuri tangu wakiwa Daraja la Kwanza (Championship).

Mbeya Kwanza kabla ya kupanda Ligi Kuu msimu huu, ilikaa misimu minne mfululizo ikisota bila mafanikio ikitumia Sokoine kabla ya kukimbilia mkoani Pwani hadi kumaliza shughuli.

Japokuwa katika msimu wa 2019/20 Sokoine ulipofungwa kwa matengenezo, timu hiyo ilitumia viwanja vya Vwawa - Mbozi mkoani Songwe na Highland Estate wilayani Mbarali mkoani hapa.

Msimu uliopita ilikimbia na kutumia Uwanja wa Mabatini mkoani Pwani ambapo ilifanya vizuri na kupanda Ligi Kuu Bara ikiwa na mechi tatu mkononi.

Baada ya kupanda ilirejea Uwanja wa Sokoine, lakini mambo hayakuwa mazuri ikicheza mechi nane bila kushinda ikiambulia sare nne na vipigo michezo minne ikikalia nafasi ya 15 na pointi 14.


Rekodi ugenini

Katika mechi 16 ilizocheza hadi sasa, timu hiyo imeshinda mechi mbili tu na zote ilipata alama sita ugenini ikiwachapa Mtibwa Sugar bao 1-0 katika mchezo wa ufunguzi wa ligi uliopigwa kwenye Uwanja wa Mabatini na pia ikainyuka Kagera Sugar bao 1-0 katika mchezo uliofanyika Uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba.

Ku-tokana na matokeo kutokuwa mazuri, mabosi walifikia uamuzi mgumu wa kusitisha kibarua cha kocha mkuu Harerimana Haruna na msaidizi wake, Michael Mnyali ‘Chuji’.

Kwa sasa timu hiyo ngeni kwenye ligi msimu huu iko chini ya kaimu kocha mkuu, Maka Mwalwisi akisaidiana na Nizar Khalfan ambao wanapambana kuinusuru na janga la kutoshuka daraja.


Ugumu uko hapa

Pamoja na kufikia uamuzi wa kuhamia Uwanja wa Majimaji uliopo Songea timu hiyo inaweza kukutana na kisiki na kujikuta ikishindwa kufikia malengo kutokana na sapoti ya mashabiki mjini huo.

Ikumbukwe Mkoa wa Ruvuma hauna timu ya Ligi Kuu baada ya Majimaji kushuka daraja misimu miwili nyuma, huku ikielezwa mwamko wa wadau kusapoti mambo ya mpira kuwa chini.

Mbeya Kwanza itakuwa na kazi ngumu kuwashawishi haraka wadau na mashabiki kuweza kuipa nguvu itakapokuwa kwenye uwanja huo ili kuweza kulinda heshima yake kutoshuka daraja.

Pia, kama ilivyokuwa Sokoine kuwa na timu mbili Ligi Kuu ikiwa ni Mbeya City na Tanzania Prisons na zile za chini, Ken Gold na Boma zinazotumia uwanja wa huo, huko Songea itakutana na Tunduru Korosho na Majimaji FC.


Nafuu ilipo

Matarajio ya Mbeya Kwanza ni kuwa kutimkia Songea ni kukwepa vita dhidi ya wapinzani wao wakubwa - Mbeya City na Tanzania Prisons ambao ndio wakongwe wa Uwanja wa Sokoine, lakini wenye wafuasi wengi kuliko wao.

Baada ya kutua Songea inaweza kupata wadau wapya ambao wanatamani kuziona Simba na Yanga, hivyo kutengeneza mazingira na ushawishi kwa timu hiyo kuweza kupata ushindi.

Misimu miwili iliyoisha bila mji huo kuwa na timu ya Ligi Kuu Bara inawaumiza wengi, hivyo hatua ya Mbeya Kwanza kuhamia mjini humo inaweza kupata nafuu na kuweza kufikia malengo.

Pia, rekodi yao ya kuwa na matokeo ugenini inaweza kuwapa faida zaidi kwani hata walipopanda Ligi Kuu walipandia kwenye uwanja wa ugenini, jambo ambalo linawapa matumaini makubwa.

Vilevile kuwapo kwenye Uwanja wa Majimaji kutaifanya kuutawala kwa muda wote tofauti na ilipokuwa Sokoine ambapo ilikuwa ikipishana muda wote na ndugu zao - Mbeya City na Tanzania Prisons na kukosa uhuru wa maandalizi.


Ya Prisons kuwakuta?

Msimu uliopita Tanzania Prisons ilihamia Uwanja wa Nelson Mandela mkoani Rukwa na japo walikuwa na mwanzo mzuri, lakini baadaye hali ilikuwa mbaya na kujikuta wakirejea mbio jijini Mbeya.

Japokuwa sababu ya timu hiyo kutimkia Rukwa ni tofauti na Mbeya Kwanza, lakini yote yanatafsiriwa kwa pamoja kwani maafande walidai kuwa ni maboresho ya miundombinu.

Msimu huu Tanzania Prisons ilikuwa na matokeo yasiyoridhisha, jambo ambalo liliwafanya mabosi kubadili mwelekeo na kurejea nyumbani, ambapo sasa Mbeya Kwanza nao hali imekuwa tete na kuamua kutimkia Songea.


Benchi la ufundi

Kaimu kocha mkuu wa timu hiyo, Maka Mwalwisi anasema kazi ya benchi la ufundi ni kufundisha bila kujali uwanja waliopo akieleza kuwa wao wako tayari kupambana.

Hata hivyo, anasema kuwa inahitajika nguvu zaidi ndani na nje ya uwanja kuhakikisha wanajinasua kutoka katika nafasi za mkiani na kupanda juu.

Anasema matarajio yao ni kufanya vizuri akisisitiza kuwa wanapambana kurekebisha upungufu ulioonekana kwenye mechi zilizopita.

“Matokeo siyo mazuri kweli, lakini hatujakata tamaa. Tunaendelea kujiandaa na mechi zinazofuata. Sisi benchi la ufundi hatuwezi kuchagua uwanja, kimsingi ni kufanya kazi yetu kuipa timu matokeo mazuri,” anasema Mwalwisi.

Kwa upande wake, meneja wa timu hiyo, David Naftar anasema wameamua kutimkia Songea kutokana na kanuni kuwaruhusu, lakini ishu pia ya matokeo na sapoti ndogo ya mashabiki ni miongoni mwa yaliyowakimbiza.

Anasema matarajio yao ni kupata ushindi katika Uwanja wa Majimaji akieleza kuwa malengo ni kumalizia michezo yao ya nyumbani mkoani Ruvuma kutegemeana na matokeo.

Naftar anasema hawajakata tamaa kwani muda upo wa kujisahihisha hasa wanapoanza raundi ya pili ya lala salama ili kuhakikisha wanapata ushindi na kubaki kwenye ligi.

“Tumeangalia mwenendo wetu pale Sokoine tukaona ipo haja ya kutafuta sehemu nyingine, lakini hata sapoti ya mashabiki ukilinganisha na timu za Mbeya City na Prisons ilikuwa ngumu kwetu,” anasema Naftar.


Wadau hawa hapa

Mdau wa soka mjini hapa, Osward Faustine anasema: “Sokoine haikuwa rafiki kwao tangu Daraja la Kwanza hawakuwa na matokeo mazuri hadi walipoenda Mabatini - Pwani wakapanda Ligi Kuu, wamerejea (Sokoine) umeona yaliyowatokea, binafsi nakubaliana nao.”

Naye Christian Mwasongwe anaeleza kuwa bado ni mapema kuwatabiria mazuri akifafanua kuwa michezo minne ya nyumbani ndio itaonyesha mwelekeo wa kubaki kwenye ligi.

“Tusubiri michezo minne tuone wanafanyaje.”