Tanzania ilivyotoka relini michezo mingi

Muktasari:
- Hiyo ni tofauti na ilivyokua miaka ya 1970 hadi mwanzoni mwa 2000 ambapo michezo mbalimbali iliandikwa, kujadiliwa na kutangazwa na vyombo vya habari nchini.
SIKU hizi habari za michezo katika magazeti, redio, runinga na mitandao ya kijamii zinatawaliwa na kandanda ukiwa ndio mchezo unaojulikana na kupendwa zaidi na Watanzania.
Hiyo ni tofauti na ilivyokua miaka ya 1970 hadi mwanzoni mwa 2000 ambapo michezo mbalimbali iliandikwa, kujadiliwa na kutangazwa na vyombo vya habari nchini.
Miaka michache kabla ya Uhuru wa Tanganyika 1961 baadhi ya michezo ilionekana kama ya makabila na watu wa tabaka fulani tofauti na ilivyokuwa Zanzibar. Miongoni mwa michezo ilionekana ni ya watu wengi waliokuwa Wazungu na wenye asili ya India hasa Goa na Singasinga.
Mpira wa magongo ulichukua sura mpya Tanzania Bara mwanzoni mwa miaka 1970 vijana wa Visiwani waliohamia Dar es Salaam walipounda timu ya Bantu iliyokuja kuwa bingwa na kutawala mchezo huo Bara kwa muda mrefu.
Kabla ya hapo timu maarufu zilikuwa Sikh Union, Goan Institute (baadaye Dar Institute) na Gymkhana.
Baadaye Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), liliunda timu iliyofanya vizuri na kuwa tishio katika mchezo huo Afrika Mashariki. Pia ziliundwa timu za Arusha Twiga na Tanga Institute.
Aliyekuwa Mwenyekiti wa Chama cha Mpira wa Magongo Tanzania (THA), ambaye alikuwa meneja wa tawi moja la Dar es Salaam la Benki ya Taifa ya Biashara (NBC), Tarlochan Singh Sandhu aliupeleka mchezo katika shule za Dar es Salaam, lakini mafanikio hayakuwa mazuri.
Hivi sasa mchezo huo umefifia jeshini na kwa klabu za Dar es Salaam na mikoani umekufa na unachechemea. Baada ya wachezaji wa Bantu kupumzika kutokana na umri mkubwa na kwa kuwa hapakuwepo vijana waliojiunga nao timu ilitoweka na kuwa sehemu ya historia.
Hivi sasa hakuna timu za mtaani - mchezo unasuasua na ushindani umetoweka. Vyombo vya habari vinaonekana kama havina habari za mpira wa magongo.
Kriketi ilichezwa sana na Wahindi wa makabila yote, Wazungu na Waafrika waliokuwa wachache hadi mwishoni mwa miaka ya 1970.
Katika miaka ya nyuma uongozi wa kriketi ulialika timu za Afrika Mashari, India na Uingereza. Wachezaji wengi walijitokeza kuwa na ustadi na miongoni mwao ni Visant Tapu na Pranlal Divecha wa Dar es Salaam.
Divecha aliyeanza kupata umaarufu 1967 anakumbukwa kwa jinsi alivyong’ara mwaka huo alipodaka wiketi tatu za timu mashuhuri ya India iliyoongozwa na nahodha Nawab Pataudi.
Vilevile alikuwa mchezaji bora Tanzania ilipocheza na Zambia katika mashindano ya Afrika Mashariki yaliyopigwa Nairobi 1968 na alikuwemo katika kikosi cha Arika Mashariki kilichopambana na MCC ya England 1974.
Divecha na Tapu walikwenda Uingereza na huko walichezea klabu kubwa kwa miaka mingi.
Divecha alikuja nchini miaka mitatu iliyopita katika tamasha lililowakutanisha wachezaji wa zamani wa mchezo huo nchini na kucheza michezo ya maonyesho 2022.
Kundi hilo lilikuwa la wachezaji karibu 40 waliokuja kutoka Uingereza, Canada, nchi za Ghuba na India, lakini habari zao hazikupewa uzito uliostahiki.
Miongoni mwa walioutumikia sana mchezo huo nchini ni daktari maarufu wa meno, Kulbir Gupta aliyefanya kazi Hospitali ya Aga Khan kwa zaidi ya miaka 20 na kuandika habari za kriketi katika magazeti ya Daily na Sunday News.
Timu ya taifa ya kriketi ilichukua ubingwa wa Afrika Mashariki na Kati mara nyingi na ilikuwa tishio Kusini mwa Jangwa la Sahara.
Michezo ya mpira wa wavu na wa mikono ilipendwa kuanzia mwanzoni mwa miaka ya 1970, lakini si sana kama kandanda.
Linalosikitisha ni kwamba huoni juhudi za kuwashawishi watu wengi washiriki na kilichokuwepo ni vyombo vya habari kuzungumzia michezo hii yanapofanyika mashindano.
Vilevile vyombo vya habari vinatoa maelezo machache ya mafunzo juu ya michezo hiyo inavyochezwa, sheia na kanuni. Mbio za magari zilivutia Watanzania na kila zilipofanyika ulikuwepo mvuto wa aina yake hasa mashindano ya East African Safari na Tanganyika 1000.
Miongoni mwa wawakilishi wa Tanzania walioiletea sifa nchi ni Waingereza waliofanya kazi na kampuni ya magari ya Tanganyika Motors, Bert Shankland na Chris Bates.
Majina yao yalikuwa maarufu katika masikio ya Watanzania miaka ya 1960 hadi 1970 kutokana na kuwashinda madereva maarufu kama Joginder Singh wa Kenya na waliotoka Finland, Ujerumani na Uingereza.
Mwaka 1968 wakati wa Pasaka nikiwa naandikia Daily News nilikwenda Milima ya Usambara na mpiga picha Ardash Nayar kusubiri magari kufika eneo hilo, hasa Mlalo ili kutuma habari na kuandika makala ya mashindano ya East African Safari.
Mwaka huo mashindano yaliyozipeleka gari Kenya na Uganda yalianzia Hoteli ya Kilimajaro na kumalizikia hapo baada ya siku nne. Tulifika milimani Jumaatatu alfajiri baada ya kulala Tanga na magari yalifika eneo hilo liliojaa matope na maji ya kina cha karibu mita moja na njia nyembamba.
Dereva wa kwanza kuchomoza majira ya saa 6 mchana alikuwa Bert Shankland na baada ya kuvuka eneo la tope tairi moja ya gari lake aina ya Peugeot 404 lilipasuka.
Sitasahau kasi iliyotumika kufungua taili lililopasika na kuweka lingine. Haikuchukua zaidi ya dakika tatu na wakati wakimalizia kufunga zilichomoza gari nne huku ile ya mbele ikiwa ya Joginder Singh wa Kenya.
Shankland aliondoka akiwa wa tano na kuelekea Mombo na baadaye Korogwe kwa hatua ya mwisho ya kwenda Dar es Salaam. Baada ya hizo gari kupita tuliingia katika Land Rover kwenda Korogwe na tulipofika tuliambiwa Shankland alishafika akiwa wa pili dakika kama mbili baada ya Joginder Singh. Safari yao ilieleka Ubena Zamozi na Morogoro na baadaye kwenda Dar es Salaam.
Taarifa tuliyoipata usiku wa manane ilieleza Shankland alikuwa wa kwanza kufika Morogoro na kumuacha Singh kama mita 100 nyuma. Siku ya pili asubuhi Shankland na Bates waliugusa utepe wa mwanzo wa Hoteli ya Kilimanjaro na Singh alikuwa wa pili dakika nne baadaye.
Siku hizi mbio za magari hufanyika mara chache na msisimko haupo licha ya Waafrika wengi kushiriki mbio hizo. Mbio za baiskeli zilipendwa na watu wengi walioshiriki, lakini ushindani ulionekana zaidi Dar es Salaam.
Katika miaka ya nyuma Tanzania ilipeleka waendesha baiskeli katika mashindano ya kimataifa, lakini washiriki walikuwa washindikizaji kutokana na baiskeli zao kuwa za kizamani na hawakuwa na uzoefu wa mashindano.
Siku hizi ni mara chache washiriki wa mbio za baiskeli wa Tanzania wanakwenda nje ya nchi kushiriki mashindano.
Tanzania ina eneo kubwa karibu na Bahari ya Hindi na ipo mito na maziwa, lakini bado ipo nyuma katika mchezo huo. Watu wengi huzungumzia kufanyia mazoezi na burudani, na hawana mawazo ya mashindano.
Michezo ya jadi hutajika katika mikutano wanayoalikwa viongozi au ikifanyika sherehe na kuelezwa kwamba Tanzania ina hazina kubwa ya michezo ya jadi na ni urithi ulioachwa na wazee wetu.
Mbali ya karata na bao, ipo michezo mingi kama kupiganisha majogoo, kurusha mikuki, vishada, gololi, mbio za waendesha punda au kucheza soka ukiwa juu ya punda, kufukuza kuku na miengineyo, lakini ushiriki wetu ni wa kiwango cha chini.
Mji wa Kabul, Afghanistan ndio makao makuu ya Shirikisho la Kimataifa la Vyama vya Kurusha Vishada na maelfu ya watu huhudhuria fainali za mchezo huo.
Ni vyema tukatafakari na kujivunia michezo ya asili ambayo gharama ya kuicheza sio kubwa kwani inaliwaza na kuwapa burudani watu.