Ufalme Simba, Yanga unapanda na kushuka

UTAWAAMBIA nini watani wa jadi kwa mastaa wao hawa ambao kila wakikaa vijiweni wanatambiana kwamba usajili wao ni bora na kutaja baadhi ya nyota ambao walikuwa wanaona wanaweza kuzibeba timu zao mwanzoni mwa msimu, Simba kukiwa na Luis Miquissone Yanga yupo Carlos Carlinhos.

Majina ya mastaa hao yalikuwa yanatamba na kuonekana wafalme mbele ya mashabiki wao, lakini ghafra yameporomoka, hakuna aliye juu ya mwingine zaidi ya ujio wa Mzee Mpili kuchukua nafasi ya kutawala kwa muda kwenye mitandao ya kijamii.

Kabla ya ligi hiyo kufikia hatua iliyopo sasa, wachezaji hao walikuwa hawakauki midomoni mwa mashabiki kutokana na kufurahishwa na majukumu yao viwanjani, sio kwamba wameacha kufanya kazi, la, isipokuwa ni upepo ulivyowaendea.

Mwanaspoti linakuletea orodha ya mastaa hao na endapo kama hawatafanya kitu cha kushtua kufunga nacho msimu huu watamaliza majina yao yakiwa yamepoa tofauti na walivyoanza Ligi Kuu.


Carlos Carlinhos - Yanga

Usajili wake ulifunika msimu huu. Ukiachana na mapokezi ya kufuru aliyoyapata, lakini alikuwa ni mchezaji mwenye nyota ya kupendwa akiingia uwanjani tu. Pamoja na hilo halikumzuia kuvunja mkataba kisha kurejea kwao Angola na jina lake likiwa linaelekea kufifia.

Wakati anasajiliwa Yanga alitokea timu ya Interclube ya Angola. Hata hivyo, hajaondoka bure ndani ya klabu hiyo kwani aliacha alama ya kuifungia mabao matatu.


Said Ntibazonkiza ‘Saido’ - Yanga

Japokuwa usajili wake haukuwa wa kutisha kivile, Yanga ilipomuona akiwa na timu yake ya taifa ya Burundi, Saido ambaye alitokea klabu ya Vital’O nyota yake ilikuwa kali baada ya kujiunga na Wanajangwani.

Wakati jina lake linawaka mbele ya mashabiki wa Yanga ni muda ambao alikuwa anafunga kwani hadi sasa anamiliki mabao manne na mechi ya majuzi alitarajiwa angefanya kitu katika dabi, lakini haikuwa hivyo badala yake bahati hiyo Mungu alimpangia Zawadi Mauya.


Bakari Mwamnyeto - Yanga

Mwamnyeto amecheza dakika 2,426 hadi sasa akiwa Yanga na amefanikiwa kuifungia timu hiyo mabao matatu. Umuhimu wake kikosini hadi hapo umeshaonekana nyota huyo alijiunga na Yanga akitokea Coastal Union msimu wa mwaka 2020/2.

Ubora wake uliwastua viongozi wa Yanga na kuamua kuachana na mkongwe Kelvin Yondani na kumpa nafasi Mwamnyeto ambaye amefanya vizuri na kuwafanya mashabiki wasahau kabisa umuhimu wa Yondani kikosini kwao, lakini ghafla baada ya kufanya makosa madogomadogo kabla ya dabi kuuwasha kwenye baadhi ya mechi jina lake lilianza kuchafuka kwa kuona hana maana tena kikosini.


Luis Miquissone - Simba

Ni kama morali ya winga wa Simba, Luis Miquissone imepungua. Wakati jina lake la moto kwa wanasoka ndani na nje ya nchi na kwenye vyombo vya habari alikuwa msumbufu kwa timu pinzani, ila sasa jina lake linaonekana kufifia. Haimanishi ni mchezaji ambaye ameishiwa, la.

Luis ana mchango mkubwa ndani ya kikosi hicho akiwa na mabao tisa na asisti 10. Mapema jina lake lilikuwa juu kwani alikuwa akikukosa kufunga atamtengenezea mwingine asisti.


Clatous Chama - Simba

Japokuwa bado ni mchezaji muhimu ndani ya kikosi cha Simba kutokana na kipaji alichojaliwa na Mungu, Chama nyota yake ni kama imefifia. Hii ni pengine ni kutokana na matatizo ya kuondokewa na mkewe, hivyo hajawaweza kurejea katika morali ya kazi kwa asilimia 100.

Hata hivyo, Chama ndiye anaongoza kwa asisti Ligi Kuu Bara, huku akifunga mabao nane na kama angefanya maajabu mechi ya watani ufalme wake ungerejea mbele ya mashabiki na endapo kama atafanikiwa kufanya kitu kabla ya msimu huu kumalizika huenda akarejesha juu jina lake.


Rally Bwalya - Simba

Bwalya wakati anasajiliwa Simba hakuwa na kishindo kivile, ingawa ujio wake ulijulikana kwamba kuna kifaa kimetua Msimbazi kutokana na alichokifanya katika timu yake ya Power Dynamos inayoshiriki Ligi Luu ya nchini Zambia.

Baada ya muda, Bwalya alianza kuwa tishio katika Ligi Kuu Bara ambapo alifanikiwa kufunga mabao mawili na asisti tano.


John Bocco - Simba

Jina la nahodha wa Simba, Bocco kuna wakati linawaka na anatajwa kila mahali. Pia kuna nyakati linapoa. Juzi limeibuka upya baada ya kufikisha bao la 15 alipofunga mojawapo dhidi ya Coastal Union.

Kama Bocco atafanikiwa kufunga katika fainali ya Kombe la Shirikisho atafunga msimu kwa kishindo kwani ni mechi inayowakutanisha watani wa jadi na inazungumziwa zaidi.