Ufahamu mchezo wa mieleka ya kidole?
Muktasari:
- Mchezo huo ulianza kama burudani baina ya familia, lakini kwa sasa umejizolea umaarufu mkubwa kiasi cha kuwa na shirikisho maalum linalousimamia. Leo tunakusogezea hapa uufahamu mchezo huo kuanzia historia na kila kitu kinachouhusu.
LONDON, ENGLAND: Thumb Wrestling ni mchezo wa ushindani wa vidole gumba vya mikono unaochezwa kwa kushindana, ambao kwa sasa unachezwa zaidi nchini Marekani na England.
Mchezo huo ulianza kama burudani baina ya familia, lakini kwa sasa umejizolea umaarufu mkubwa kiasi cha kuwa na shirikisho maalum linalousimamia. Leo tunakusogezea hapa uufahamu mchezo huo kuanzia historia na kila kitu kinachouhusu.
HISTORIA
Mchezo ulianza kuchezwa na watoto na watu wazima mwanzoni mwa karne ya 20. Baadhi ya ripoti zinadai kwamba ulianzishwa rasmi na Bernard Davidson miaka ya 1940, huku watu wengine wakidai ulianzishwa na baadhi ya vijana miaka ya 1930.
Kwa miaka mingi, mchezo huu ulienea ulimwenguni kote, ukitumika kama sehemu ya burudani. Pia ulitumika katika ubishani, ambapo watu walipokuwa wanajiuliza nani awe wa kwanza kufanya kitu fulani, walikuwa wakiucheza, na atakayeshinda ndiye alianza.
Hata hivyo, kidogo kidogo mchezo huu ulianza kupata umaarufu mkubwa kiasi cha baadhi ya watu kuamua kuunda mashindano na shirikisho rasmi la kuusimamia.
SHERIA NA KANUNI
Ingawa 'thumb wrestling' mara nyingi huchezwa bila mwamuzi rasmi, kanuni za kawaida za mchezo ni kama ifuatavyo:
Washindani wawili hukaa uso kwa uso na kugusanisha vidole vyao, na lengo huwa ni kuhakikisha unakandamiza kidole cha mpinzani wako kwenda chini kwa muda wa sekunde tatu hadi nne. Ukifanikiwa kufanya hivyo, unatangazwa kuwa mshindi rasmi.
Mechi mara nyingi huanza kwa kuhesabiwa, yaani “1, 2, 3”, au wakati mwingine mwamuzi husema, “I declare a thumb war!”, na mara baada ya hapo washindani hutakiwa kuanza kushindana.
Katika mashindano rasmi, mara nyingi mechi huchezwa katika mzunguko wa raundi tatu hadi mshindi atakapopatikana.
Ikiwa hakuna mshindi baada ya muda uliowekwa, ambao mara nyingi huwa ni dakika moja kwa kila mzunguko, muda wa ziada huongezwa na mechi husogea kwenda raundi ya nne.
Ni marufuku kutumia sehemu nyingine za mwili kwa ajili ya kushinda. Pia hairuhusiwi kutumia mikono miwili au vidole vya ziada; kidole pekee kinachotakiwa kushinda huwa ni gumba.
Wachezaji hawaruhusiwi kuinua mikono yao juu ya kiwango kilichowekwa.
SHIRIKISHO NA USIMAMIZI
Mchezo huo kwa sasa unasimamiwa na World Thumb Wrestling Championships lenye makao yake makuu nchini England, ambalo mwaka 2011 lilianzisha rasmi mashindano ya World Thumb Wrestling Championships. Mashindano hayo yamekuwa yakifanyika kila mwaka, yakivutia washiriki kutoka mataifa mbalimbali.
Mashindano haya yaliyoboreshwa hufanyika ukumbini, na washiriki hutakiwa kuvaa viplastiki katika vidole vyao kwa ajili ya usalama. Pia vidole wanavyotumia kushindania huingizwa katika viulingo maalum.
Taarifa zinadai pia kuna shirikisho lingine liitwalo British Thumb Wrestling Championships, ambalo nalo limeanzisha mashindano yake yanayofanyika Lowestoft, Suffolk, Uingereza.
WACHEZAJI MAARUFU
Ingawa mchezo huu si kama soka au tenisi yenye nyota wengi, baadhi ya wachezaji wamejipatia umaarufu mkubwa katika mashindano haya.
Paul “Under the Thumb” Browse ni mchezaji wa kwanza maarufu wa mchezo huu, na pia ndiye mshindi mara nyingi wa michuano ya World Thumb Wrestling Championships, akiwa bingwa kuanzia mwaka 2016 hadi 2019.
Mbali na Paul, pia kuna Janet “Nanny-Thumb” Coleman, ambaye ni bingwa wa muda wote wa mchezo huu kwa upande wa wanawake kwenye mashindano rasmi.
Kamran Farid naye ni miongoni mwa wachezaji mashuhuri, anayejulikana kwa mbinu yake ya Torque Lock.
NCHI ZINAZOCHEZA ZAIDI
Thumb wrestling ni mchezo unaochezwa ulimwenguni kote. Hata hivyo, baadhi ya maeneo yenye shughuli kubwa za mashindano haya ni Uingereza, ambako ndiko kunakofanyika zaidi mashindano ya dunia. Vilevile, nchini Marekani mchezo huu umeshika kasi, na kuna ligi maalumu ya mashindano yake.
ZAWADI ZA UBINGWA
Katika mashindano ya 'thumb wrestling' kuna zawadi tofauti kulingana na aina ya michuano husika. Katika mashindano ya dunia mara nyingi washindi hukabidhiwa mikanda na zawadi ya fedha inayofikia Dola 50,000.
Kwa mashindano madogo zawadi huwa ni vyeti na medali za ubingwa pamoja na kiasi cha fedha kisichozidi Dola 10,000. Baadhi ya wachezaji maarufu pia wamekuwa wakipata mikataba ya udhamini kutoka kampuni mbalimbali.