Ubora! Gomes, Milton na mageuzi ya kimkakati Simba

Sunday February 28 2021
New Content Item (2)
By Imani Makongoro

MASHABIKI wa Simba wanacheeka. Kila mmoja ana raha juu ya mwenendo wa timu yao kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika.

Timu hiyo imevuna pointi sita katika mechi mbili za kundi A ilizocheza dhidi ya AS Vita ya DR Congo na Al Ahly ya Misri, matokeo yanayoifanya Simba kutanguliza mguu mmoja kwenye robo fainali ya Ligi ya Mabingwa.

Ujio wa kocha mkuu Didier Gomes na kocha wa makipa, Milton George unatajwa kuwa miongoni mwa siri za mafanikio ya kikosi hicho cha mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Bara.

Kwa makipa wa Simba, Aishi Manula na Beno Kakolanya, ukiachana na ubora wa viwango vyao kuimarika, lakini kocha Milton ameonekana kuimarisha zaidi maelewano ya makipa hao.

“Makipa wa Simba wamebadilika sana, hasa Aishi amekuwa na mabadiliko, kuna vitu ambavyo bila shaka kocha anayewafundisha sasa amevibadilisha,” anasema kipa nyota wa zamani wa timu hiyo, Mohammed Mwameja.

Anasema siyo kwa Manula pekee, bali hata Kakolanya na kwenye kikosi cha Simba sasa presha ya makipa haipo.

Advertisement

Mbali na viwango kuimarika, ujio wa Milton tangu Januari, mwaka huu, umebadili hata ile tafsiri ya nje ya mashabiki ambao waliamini Kakolanya na Manula hawapiki chungu kimoja. Wakiwa mazoezini, makipa hao wanaelekezana na kusaidiana tena kwa kusikilizana na kwenye mechi wanapishana kucheza.

“Kuna kitu ambacho kocha wa makipa hivi sasa anakipatia, nimejaribu kuwafuatilia makipa wetu wamebadilika sana, Aishi alikuwa na changamoto kwenye mipira ya krosi, lakini sasa tatizo limekwisha na kwenye mechi na Al Ahly alicheza kwa kiwango na anaonekana amebadilika sana,” anasema Mwameja.

Mbali na kocha wa makipa, kocha mkuu Mfaransa, Gomes ametajwa kuja na mapinduzi ya kimkakati kwenye kikosi cha Simba.

Kocha huyo aliajiriwa hivi karibuni kuchukua mikoba ya Mbelgiji Sven Vandenbroeck.

“Tangu ameanza kuinoa Simba kuna vitu vingi ambavyo vimebadilika kwenge kikosi hicho,” anasema mchambuzi wa soka, Alex Kashasha ‘Mwalimu Kashasha’.

Anasema tofauti na Simba ya Sven, hii ya Gomes ina mbinu nyingi zaidi za kutafuta mabao.

Chini ya Sven mara nyingi Simba ilicheza ikitumia mfumo wa 4-2-3-1, ikiwatumia mabeki wanne, viungo wakabaji wawili, viungo washambuliaji watatu na mshambuliaji mmoja.

Mfumo ambao nyota wa zamani wa timu hiyo, Mtemi Ramadhan alishauri ubadilike kwenye mechi za Ligi ya Mabingwa hasa kwenye mechi na Al Ahly.

“Kocha awatumie washambuliaji wawili au watatu ili kuongeza kasi ya mashambulizi hasa kwenye mashindano ya kimataifa,” anasema Ramadhan.

Hata hivyo, Gomes ni kama amebadili mfumo mara nyingi wanacheza 4-3-3, wanatengeneza timu imekuwa na mbinu nyingi za kutafuta matokeo.

Siri nyingine ya Gomes ni aina ya kocha ambaye muda mwingi anawasoma wapinzani ili kujua ubora na udhaifu wao.

“Kwenye ubora uwa anatafuta mbinu ya kuwadhibiti na kwenye udhaifu anautumia kuwamaliza,” anasema Mwalimu Kashasha.

Mchambuzi huyo maarufu wa soka nchini anasema hata haina ya uchezaji wa Simba tangu ametua Gomes umebadilika kikosini.

“Simba ya Sven ilikuwa inacheza pasi hadi golini, lakini kwa Gomes timu inajaribu kufunga hata nje ya boksi,” anasema Mwalimu Kashasha.

Kingine ambacho Gomes amebadili Simba ni kuwapa nafasi wachezaji ambao mtangulizi wake hakupenda kuwatumia akiwamo Meddie Kagere, Kennedy Juma na Thadeo Lwanga.

Advertisement