UBISHI WA MZEE WA KALIUA: Umemuona Dk Khalid Aucho?

VUTA picha mbili kichwani mwako. Ya kwanza, fikiria upo mwenyewe unakatiza katika uchochoro wa kutisha usiku wa manane, lazima utakuwa unatetemeka, pengine na jasho litakuwa linakutoka kwa hofu ukiwaza unaweza kudhurika kwa hatari yoyote itakayojitokeza mbele yako.

Pili vuta picha, unakatiza katika uchochoro huohuo usiku wa manane, kando yako wapo wanajeshi waliobeba silaha nzito wakikusindikiza. Utakuwa na hali gani?

Lazima utakuwa unatembea kwa madaha na maringo ukifahamu upo katika mikono salama na hatari yoyote itakayojitokeza itashughulikiwa vilivyo. Kitu kinachoitwa hofu, ‘kitakuwa kilometa 1000 mbali na wewe’.

Hii picha ya pili kwa sasa inaonekana katika timu yenye maskani yake pale makutano ya mitaa ya Twiga na Jangwani, Yanga Afrika.

Kuna kitu kimoja kikubwa kimeongezeka kwa wachezaji wa Yanga. Kitu gani hicho? Kujiamni. Uwatazamapo wachezaji waliokuwepo Yanga misimu iliyopita wakicheza leo, unapata hisia uwezo wao umeongezeka mara dufu, unasikia sauti fulani ikikunong’oneza ndani yako, ‘Hawa ndiyo wachezaji wanaostahili kucheza Yanga’.

Unajikuta ukisahau wachezaji hawa walikuwa sehemu ya kikosi cha Yanga kilichokosa taji lolote kubwa msimu uliopita, unasoma magazeti unashangaa ghafla Fei Toto ameibuka kuwa staa mkubwa nchini.

Unamtazama Farid Musa uwanjani unahisi kama amerejea katika ubora wake, hisia kama hizo unazipata kwa wachezaji wengine wachache waliofanikiwa kuingia kikosi cha kwanza cha kocha Nabi.

Dickson Job na Kibwana Shomari wanaweza kusema wana uhakika wa nafasi kikosi cha kwanza cha Yanga, mwisho unajiuliza swali, kipi kipya kimeongezeka Yanga? Jibu ni hakuna! Zaidi ya wachezaji bora waliongezwa kikosini, hakuna kipya kingine kilichofanyika Yanga kikainua uwezo wa wachezaji wengi waliokuwepo miaka iliyopita.

Kwa sasa hivi, ni rahisi kwa Fei Toto kutulia na mpira na kuamua wapi apige pasi sahihi zaidi kwasababu anajua hata kama atapoteza, nyuma yake wapo kina Khalid Aucho na Yanick Bangala wataukaba na kumrudishia tena, ni tofauti kidogo nyuma yake akiwa na Zawadi Mauya.

Kwa sasa hivi Farid ana ujasiri wa kuchukua mpira na kuukokota katikati ya kiwanja pasipo uwoga kama alivofanya siku ile dhidi ya Simba kwasababu anajua hata kama atapoteza bado timu haitakuwa katika hatari. Kwa sasa Farid anacheza kichwani mwake akijua pasi yake ya mwisho ina mtu wa kuigeuza kuwa bao, mfano mzuri ni bao gumu alilofunga Fiston Mayele siku ile ya ngao jamii.

Miezi mitatu iliyopita Michael Saprong asingeweza kufanya chochote pale zaidi ya kupiga nje au kuupoteza kwenye miguu ya mabeki, kwa sasa Farid ana ujasiri kuwa ana mtu wa kushirikiana nae vema, hali kama hiyo ipo kwa Kibwana aliyesogezwa upande wa kushoto ili kumpisha mtaalam kutoka Congo Djuma Shaban upande wa kulia.

Ni hivyo hivyo kwa Dickson ambaye ana mtu wa kumuongoza na kufukia mashimo yake, Yanick Bangala.

Licha ya kwamba ni mapema sana, kwa msimu huu unaweza kusema Yanga wamepatia usajili walioufanya. ‘Hakuna mchezaji waliyepigwa’. Kwa sasa lango lao lipo katika mikono salama ya Djigui Diarra.

Si kama ilivokuwa kwa Klaus Kindoki na Farouk Shikalo, Aucho ni kiungo waliyemkosa tangu azeeke na kuondoka nchini fundi kutoka Zimbabwe, Thaban Scara Kamusoko, fundi aliyekuja kutimiza mpango wa Yanga kucheza soka safi la ardhini, soka ambalo Yanga walilipachika jina la ‘kampa, kampa tena’.

Bangala ni beki kiongozi ambaye uzoefu wake umeshaanza kuwafaidisha Yanga, bado tunasubiri mabao ya Mayele na Heritier Makambo ambaye ni chaguo la pili nyuma ya Mayele. Ni suala la muda.

Mwisho kabisa nafikiri msimu huu Yanga watampa Simba upinzani wa kweli, si kama ule waliokuwa wakijidanganya mdomoni misimu kadhaa iliyopita lakini akilini wakijua haiwezekani.

Nafikiri kama wataepushwa na majeraha, na wachezaji wakawa katika ubora muda mwingi wa msimu, watampa Simba upinzani wa kweli. Ndiyo! Simba.

Sidhani kama Azam FC wapo katika mbio za ubingwa.