UBISHI WA MZEE WA KALIUA: Nini kimekuvutia zaidi Qatar?

KWA sasa macho na masikio ya wengi yapo Qatar ambako Kombe la Dunia linaendelea katika viwanja mbalimbali na lile la awamu hii ni la 22 kufanyika tangu lilipofanyika mara ya kwanza 1930 nchini Uruguay.

Mwaka huu wa michuano hiyo mikubwa kwa ngazi ya timu za taifa umeghubikwa na mambo mbalimbali ikiwemo marufuku ya unywaji pombe viwanjani na nje ya hapo wenyeji wamepiga marufuku kampeni zinazohamasisha mapenzi ya jinsia moja.

Hilo limemkuta nyota wa England, Harry Kane na Manuel Neuer wa Ujerumani ambao kwa nyakati tofauti walisema watavaa vitambaa vya unahodha vyenye ujumbe wa neno ONE LOVE wakihamasisha usawa kwenye mambo mbalimbali ikiwemo mapenzi ya jinsia moja kabla ya Shirikisho la Soka Duniani (Fifa) kupiga marufuku na mara moja nyota hao walibadilisha mpango huo.

Nje ya tukio hilo, haya hapa matukio na rekodi zinatokea au zilizotokea Qatar ambapo michuano hiyo inachukua nafasi.


WENYEJI KUPOTEZA UFUNGUZI

Imeshuhudiwa wenyeji wa mashindano wakiingia katika rekodi ya miaka 92 tangu kuanza kwa michuano hiyo baada ya kuwa mwenyeji wa kwanza kupoteza mchezo wa ufunguzi baada ya kufungwa mabao 2-0 na Ecuador. Kwenye miaka ya hivi karibuni ilishuhudiwa 2018 mwenyeji - Russia akianza kwa kuifunga Saudi Arabia mabao 5-0. Nje ya kombe hilo nyuma kabla ya Russia yaani 2014 nchini Brazil wenyeji walianza kwa ushindi wa kishindo kwa kuichapa Croatia kipigo cha mabao 3-1. Pia 2010 ambapo kwa mara ya kwanza Kombe la Dunia lilipofanyika barani Afrika wenyeji Afrika Kusini walipata sare ya bao 1-1 dhidi ya Mexico kwenye mchezo wa ufunguzi. Hivyo kitendo cha Qatar kupoteza mchezo wa ufunguzi wameingia katika vitabu vya kumbukumbu ya michuano hiyo.


BAO LA KWANZA

Mwaka huu straika wa Ecuador, Enner Valencia mwenye umri wa miaka 33 amekuwa mchezaji wa kwanza kufunga bao la kwanza kwenye michuano hiyo baada ya kufunga katika dakika 16 dhidi ya wenyeji Qatar. Pia straika huyo wa zamani wa West Ham United ambaye kwa sasa yupo Fernabahce ya Uturuki alifunga bao la pili dakika ya 31.


KUFANYIKA NOVEMBA

Katika hali ya kawaida tangu kuanza kwa michuano hiyo 1930 hufanyika Juni na kumalizika Julai na mara zote huwa kwenye utaratibu huo, lakini hii imeingia kwenye vitabu vya rekodi kwa kufanyika Novemba hadi Desemba na sababu kubwa inatokana na Juni na Julai kuwapo kwa hali mbaya ya hewa nchini humo hasa joto, hivyo ingekuwa shida na tabu kwa timu hususan za Ulaya, hivyo mwezi huu hali ya hewa huwa tulivu kwa kiasi flani.


WAZAWA AFRIKA

Kwa mara ya kwanza kwenye historia ya timu za Afrika mataifa yote matano yataongozwa na makocha wazawa wa mataifa hayo. Senegal wataongozwa na nahodha wa zamani, Alliou Cisse huku Cameroon wakiongozwa na mchezaji mkongwe wa zamani, Rigobert Song, ilhali Ghana itaongozwa na Otto Addo, huku Morrocco iko chini ya Walid Regragui na Tunisia ni Jalel Kadri.


MSHINDI BALLON D’OR

Baada ya Karim Benzema, mshindi wa tuzo ya Ballon d’or kuumia katika mazoezi ya timu ya taifa ya Ufaransa, rasmi ataikosa michuano hiyo na straika huyo ameingia kwenye rekodi ya kuwa mshindi wa ballon d’or na kushindwa kucheza mashindano hayo. Benzema anakuwa mchezaji wa tatu kukosa mashindano baada ya kubeba tuzo hiyo akifuata nyayo za kina Allan Simonsen wa Denmark aliyekosa 1978 baada ya kushinda tuzo ya ballon d’or pamoja na gwiji wa Real Madrid, Alfred de Stefano aliyekosa fainali za 1958. Mbali na rekodi hiyo pia kwa mara ya kwanza mwaka huu mshindi wa pili wa tuzo hiyo ambaye ni Sadio Mane naye amekosekana uwanjani Qatar baada ya kupata majeraha na kushindwa kucheza mashindano hayo.


MABAO YA KWANZA

Kwa mara ya kwanza England imetoa wachezaji wengi kwenye mchezo mmoja ambao wamefunga mabao yao ya kwanza. Wachezaji hao ni pamoja na Bukayo Saka, Raheem Sterling, Jude Bellingham na Marcus Rashford. Pia kwenye mchezo wa England waliowafunga Iran kwa kipigo cha mabao 6-2 waliweka rekodi ya upigaji pasi 35 kabla ya Jack Grealish kufunga bao la sita. Hizo ni pasi nyingi kwenye utengenezaji wa bao katika michuano hiyo.


PENALTI UFUNGUZI

Bao alilolifunga Enner Valencia ambalo ndilo la kwanza kwenye mashindano hayo pia limeingia katika rekodi baada ya kuwa la kwanza kufungwa katika mchezo wa ufunguzi kwa mkwaju wa penalti dhidi ya wenyeji, Qatar. Kwa ujumla huenda mashindano ya mwaka huu yakaweka rekodi nyingi kutokana na mwanzo wa rekodi za mapema zilizowekwa kwenye michezo ya awali.