UBISHI WA MZEE WA KALIUA: Kwanini huyu Kipanya Malapa hayupo studio?

ILE picha ya Kipanya Malapa akiwa katika kijiwe chake cha kuuza mishikaki imekuwa gumzo mitandaoni wengi wakiitumia kama dhihaka. Wapo walioielewa na kuona anachokifanya ni kitu kizuri kwa ajili ya kuendesha maisha yake.
Kipanga ni nyota wa zamani wa Yanga na Singida United - timu alizozichezea kwa mafanikio makubwa miaka michache iliyopita.
Kipanya, mchezaji aliyeivaa jezi ya klabu kubwa na kongwe nchini ya Yanga ameishia vipi katika kuuza kachori na mishikaki?
Pengine baada ya kulitumikia soka, hivi sasa mkongwe huyo alipaswa kuwa ametulia ndani ya makazi yake bora kabisa akifuatilia mwenendo wa biashara zake.
Kama sio hivyo, basi angekuwa pembeni ya uwanja akiwa amevaa suti akitoa maelekezo akisimama kama kocha - kama ilivyo kwa wachezaji wengi wa zamani walioamua kuishia katika kufundisha mchezo wenyewe.
Kama sio kufundisha soka, basi Kipanya alipaswa kuwa mbele ya kamera au katika kipaza sauti cha kituo kimoja cha habari nchini akichambua soka kama wanavyofanya kina Garry Neville, Jamie Caragher na wengineo waliowahi kukiwasha miaka ya nyuma na sasa ni wachambuzi.
Kama sio hivyo basi angekuwa na kazi moja katika kazi nyingi ambazo ni za watu wa familia ya mpira. Hizo ndizo kazi kama ukurugenzi wa ufundi, lakini hayo yote yapo kushoto kwa Kipanya na sasa yupo kijiweni kwake akiuza mishikaki.
Kwanza napenda ieleweke kwamba naheshimu alichochagua kufanya Kipanya na sina tatizo lolote na kazi aliyoichagua kumpa mkate wake wa kila siku.
Mungu humpa kila mtu kadiri ya uwezo wake. Licha ya hilo bado haiondoi ukweli kwamba kuna sehemu kubwa ambayo wanasoka na wachezaji wetu wa zamani wamekwama.
Mara ngapi umesikia mchezaji wa zamani wa Simba au Yanga amelala ndani anaumwa hoi na hana pesa ya matibabu?
Majuzi tu nilisikia mjadala mahali kwamba wachezaji wa zamani watafutiwe utaratibu wa kuingia uwanjani kutazama mechi bure kwa sababu hawana uwezo wa kujilipia tiketi za mechi.
Hii inaonyesha ni kwa kiasi wachezaji wetu wa zamani wanaishi chini ya kipato cha Mtanzania wa kawaida.
Ni ukweli kwamba soka la zamani lilikuwa halilipi na wahusika walicheza kwa mapenzi zaidi kuliko kufikiria kipato. Zamani mchezaji angefurahia tu kuvaa jezi ya Simba kwa sababu ni shabiki wa Simba. Kipato kisingekuwa kipaumbele sana. Huwezi kuwalaumu sana kwa sababu hawakupata bahati ya kuishi katika dunia ya mwanga kama ilivyo sasa. Kitu pekee ambacho bado najiuliza mpaka sasa ilikuwa vipi hawa wazee wakashindwa kuingia katika kazi ya familia za mpira baada ya kustaafu?
Ni wachezaji wangapi wa zamani wamefanikiwa kuwa makocha? Tuna wachambuzi wangapi waliocheza mpira? Wapo wapi wakurugenzi wa ufundi waliovaa jezi za klabu na timu ya taifa ya Tanzania?
Ukweli ni kwamba tunawakilishwa na wachezaji wachache wa zamani katika familia ya mpira. Hawa ndio kina Charles Mkwasa, Juma Mgunda, Fred Felix Minziro, Jamhuri Kiwelu, Ally Mayay na wengine kadhaa. Wamepotelea wapi wengine? Kuna hoja huwa zinaibuliwa kwamba wachezaji wengi hawakwenda shule, hivyo ni vigumu kwao kupata nafasi.
Siikubali mara nyingi sana hii hoja. Huwa nawatazama kina Garry Neville wakichambua Ligi Kuu ya England pale Sky Sports na wanachambua kwa umaridadi mkubwa.
Garry Neville alikwenda shule lini kama aliingia Manchester United ya wakubwa akiwa kijana na umri wa miaka 16?
Leo hii Thiery Henry ameshakuwa kocha wa Monaco na sasa ni mchambuzi wa chaneli moja inayoonyesha Ligi ya Mabingwa Ulaya nchini Marekani. Bila shaka anaingiza pesa ya kutosha ya kuendesha maisha yake.
Thiery alisoma lini kama aliingia timu ya wakubwa Monaco akiwa mdogo wa miaka 16? Kuna ukweli inabidi tukubali kwamba wachezaji wetu wamegoma kubadilika kuendana na mabadiliko ya dunia. Mabadiliko yanayohitaji ujiandae na kazi nyingine ya mpira baada ya kustaafu.
Unapotazama mahojiano ya wachezaji baada ya mechi za Ligi Kuu Bara kutamatika pale Azam TV, unakosa hamu ya kusikiliza kwa sababu unaweza kabisa kutabiri kitakachozungumzwa. Hupati maelezo ya kiufundi yanayoweza kukuelewesha nini kilitokea uwanjani. Ni lini mchezaji kama huyo atakuwa mchambuzi wa mpira. Matokeo yake tuna kundi kubwa la vijana kutoka mtaani ambao hawajacheza lakini wanakalia viti vya studio kuchambua mpira na wanachambua vizuri. Ni kwasababu wachezaji wamegoma kubadilika na kujiandaa na maisha baada ya soka. Ukweli mchungu.