UBISHI WA MZEE WA KALIUA: Kuna Dullah Mbabe na Abdalla Pazi

ILIKUWA wiki nyingine ngumu kwa bondia Abdallah Iddi Pazi, yeye mwenyewe anajiita ‘Rais wa Wazaramo’ sisi tunamfahamu zaidi kama Dullah Mbabe.

Mabondia wote korofi duniani wanamiliki majina maarufu (a.k.a) ya kikatili. Hili linatokana na mchezo wenyewe. Boxing ni mchezo unaochezwa na watu katili na korofi waliojaa tambo, mbwembwe na dharau kwa wapinzani wao.

Ndiyo maana haishangazi kusikia Hassan Mwakinyo ‘akimcharara’ Twaha Kiduku kwamba siyo bondia wa hadhi yake. Ndivyo ilivyo asili ya boxing duniani kote. Hata kina Mayweather hawana uungwana wanapowazungumzia wapinzani wao.

Dullah Mbabe na yeye anatumbukia katika kundi hili la mabondia korofi wanaomiliki majina ya kikatili. MBABE. Jina la kikatili linaloendana na boxing.

Zamani Mike Tyson alikuwa anajiita ‘The baddest man on planet’ yaani mtu mbaya zaidi duniani. Ni kweli alikuwa mtu mbaya zaidi duniani? Ni ukatili tu. Muhammad Ali alikuwa anajiita ‘The greatest’ yaani bora zaidi ya wote.

Mayweather ameamua kujichagulia majina mawili. La kwanza ni ‘Money’. Ndiyo! Money kwa sababu anaamini sura yake inafanana na pesa. La pili ni ‘The best ever (TBE) akimaanisha yeye ni bora zaidi kuwahi kutokea. Msururu ni mrefu tukisema tukumbuke a.k.a za majabali wote waliowahi kucheza ngumi hatutamaliza leo.

Tofauti ya Dullah Mbabe na mabondia wote waliozungumzwa hapo juu ni kwamba, hao hapo juu walikuwa mabondia kweli! Hawakuwahi kuibua mijadala juu ya uwezo wao.

Kama majina yao yalivuokuwa katili nao pia walikuwa katili ulingoni. Hawakuwahi kuyumbishwa

katika ubora wao. Waliwahi kupoteza mapambano, lakini uwezo wao haukuibua mijadala. Walikuwa bora na walionyesha ubora wao.

Jumapili ya majuzi, Dullah Mbabe alileta tena mjadala mezani juu ya uwezo wake baada ya kupokea kipigo kutoka kwa Mkongo Tshimanga Katompa.

Lilikuwa pambano la pili mfululizo anapoteza baada ya kupoteza lile la Twaha Kiduku. Jumapili hakuwa Dullah Mbabe tunayemfahamu, japo alimaliza pambano lakini alipigwa.

Alikuwa hovyo sana. Nafikiri, lile ni kati ya mapambano mabovu aliyowahi kucheza Dullah Mbabe. Juzi baada ya pambano nikasikia watu wananong’ona kwamba zama zake zimefika mwisho.

Niliguna kidogo. Zama zinafikaje mwisho kwa bondia mwenye miaka 28? Mabondia wanaanza kuchoka wanapofikisha miaka 35, nyuma ya hapo ni umri wa kuwa katika ubora wa kiwango juu. Dullah Mbabe yupo katika umri huu wa kuwa bora.

Sio kweli kwamba zama zake zimefika mwisho. Nafikiri swali zuri la kujiuliza lilipaswa kuwa nini kinamkumba Dullah Mbabe? Mbona anaporomoka katika umri ambao alipaswa kupanda?

Nafikiri kitu kikubwa kinachomtesa Dullah Mbabe zaidi kwa sasa ni presha ya kutaka kupanda haraka na kuwafikia mabondia wawili waliopo juu zaidi nchini kwa sasa, Hassan Mwakinyo na Twaha Kiduku.

Presha inayoshambulia ubongo na kuathiri saikolojia yake. Saikolojia ya Dullah Mbabe haipo sawa kwa sasa. Ushahidi ni pambano la juzi.

Inashauriwa bondia ‘professional’ apambane mapambano mawili hadi matatu kwa mwaka - tena yatofautiane kwa muda wa miezi minne hadi sita. Juzi, Dullah Mbabe alipambana ulingoni zikiwa zimepita wiki tano tu toka apambane mara ya mwisho.

Bado alikuwa na uchovu wa pambano lililopita - uchovu uliomsababisha kupoteza pambano.

Ilikuwaje akakubali kucheza akiwa amechoka? Jibu ni rahisi, presha ya kutaka kwenda juu haraka.

Katika pambano la Jumapili, Mbabe alipoteza sifa mbili kubwa kati ya tatu za bondia.

Kwanza ulinzi wake ulikuwa mdogo, lakini pili ushambuliaji wake ulikuwa hafifu. Sifa pekee aliyokuwa nayo ni uvumilivu. Hauwezi kushinda ngumi kwa uvumilivu pekee unapaswa kujilinda na kushambulia huku ukivumilia. Nimalizie kwa kumshauri Dullah Mbabe. Nafikiri zama zake hazijafika mwisho kama wanavyodhani baadhi ya watu, bado yupo katika umri sahihi wa kung’ara.

Anachohitaji sasa hivi ni kutuliza akili yake. Aache kuangalia waliopo juu yake kisha apate mapumziko ya muda mrefu ili kutibu mwili wake uliochoka. Baada ya hapo arejee ulingoni.

Ikiwezekana apotee kabisa Dar es Salaam. Amuombe rafiki yake Nikki wa Pili ambaye ni mkuu wa Wilaya ya Kisarawe ampatie hifadhi kwa mwaka mmoja. Akusanye nguvu za kutosha kisha arejee tena. Zama zake hazijafika mwisho, bado Dullah yupo katika zama zake.