UBISHI WA MZEE WA KALIUA: Hichi ndicho kilichoiua Yanga

IMEWALAZIMU Simba kusubiri miaka minne kupata ushindi mbele ya Yanga katika mchezo wa Ligi Kuu Bara. Katika hiyo miaka minne walipata ushindi katika Kombe la Shirikisho la Azam, lakini katika Ligi Kuu waliangukia pua mara zote.
Kama mchezo haukumalizika kwa sare basi Yanga waliondoka na matokeo ya ushindi. Unaweza kujiuliza ni kwa jinsi gani Simba walishindwa kufurukuta mbele ya Yanga kwa miaka minne? Je Yanga walikuwa bora sana? Je Simba walikuwa hovyo sana? Sidhani kama majibu ya maswali yote ni sahihi.
Katika kipindi cha miaka minne maisha yamekwenda kushoto na kulia kwa kila mmoja wao. Simba walikuwa juu sana, halafu ghafla Simba wakashuka na Yanga wakapanda walipokuwepo Simba.
Ajabu ni kwamba katika kipindi chote cha 'baridi na joto' ni Yanga waliowasumbua zaidi Simba katika mechi za mtani. Kuna kitu kimoja kiliwasaidia Yanga katika mechi zao dhidi ya Simba. Mara zote waliingia kwa hofu na tahadhari kubwa bila kujali ubora wao wala ubora wa Simba. Hii heshima iliwasaidia kuondoka na tabasamu mbele ya Simba mara kadhaa.
Simba mara nyingi waliingiza uwanjani ubora wao tu wakati Yanga waliingiza heshima na jitihada. Matokeo yake uwanjani Yanga wakajikuta wakikimbia mara mbili zaidi ya Simba. Ghafla wakajikuta wakiondoka na matokeo mazuri hata kipindi ambacho hawakuwa imara kama Simba.
Katika mchezo wa mwishoni mwa wiki ni Simba walioingia uwanjani wakiwa timu ya pili huku Yanga wakiingia kama wababe. Yanga walisahau kinachowapa matokeo siku zote.
Yanga waliingia wakijitazama kama wababe, vichwani mwao wakiwa na kumbukumbu za mechi kadhaa nyuma. Ilianza nje kwa mashabiki wao. Safari hii hawakuwa na ule msemo wa "Hii ni derby, haitabiriki". Walimaliza wiki wakiimba ubora wao na wakiamini lazima wamfunge Simba. Hili lilichagizwa zaidi na wasemaji wao vijana waliotamba katika mitandao ya kijamii.
Simba wao walitamba kwamba watashinda lakini walichukua tahadhari wakikumbuka jinsi Yanga walivyowasumbua miaka ya karibuni. Hawakujiamini sana. Hii iliingia hadi kambini kwao. Wachezaji wa Simba wakajikuta wakiuheshimu mchezo zaidi kuliko Yanga. Simba wakajikuta katika mazingira mazuri zaidi ya mechi.
Ushahidi wa hilo ni bao la mapema walilofunga Simba. Ilikuwa kona ya mapema ambayo Saido Ntibazonkiza aliianza kwa Shomary Kapombe. Walikuwa wapi Yanga wakati Kapombe anaanzishiwa mpira karibu kabisa na eneo la hatari?
Ni kwa sababu hawakujiandaa kukabiliana na mchezo kwa heshima. Kapombe aliuweka vyema mpira katika kisanduku na Henock Inonga alimalizia vyema kwa kichwa. Nina uhakika Inonga hakuamini amepewa uhuru mkubwa vile katika sanduku la mpinzani. Walikuwa wapi walinzi wa Yanga wakati Inonga anaushambulia mpira wa juu? Ni ukosefu wa heshima tu.
Hawakuishia hapo. Simba walikuwa na nafasi kadhaa ambazo zingeweza kugeuka mabao kama wangezidisha umakini. Katikati mwa kipindi cha kwanza, Yanga walikamatwa katika shambulizi la kushtukiza na Kibu Denis alijikuta akitazamana na kipa wa Yanga, Djigui Diarra na alifanya kitu sahihi alichopaswa kufanya. Hata hivyo angekosa tusingeshangaa. Mara nyingi hupaisha katika mazingira kama yale.
Hadi kufikia hapo msumari wa mwisho ukawa umepigwa katika jeneza la Yanga. Simba wangeweza kuondoka kipindi cha kwanza wakiwa na mabao manne mbele kama Jean Baleke angekuwa katika ubora wake. Kipindi cha pili Yanga walifanya mabadiliko yaliyowasaidia kutawala mchezo, lakini hawakupata mabao.
Baada ya mechi nilimsikia kocha wa Yanga, Nasreddine Nabi akilalamika kwamba bao la kwanza la Simba halikupaswa kuwepo.
Pengine ni kweli Lomalisa hakuutoa mpira nje na haikupaswa kuwa kona, lakini Yanga walipata muda wa kujipanga na wangeweza kuzuia vyema. Nafikiri awalaumu zaidi walinzi wake kuliko mwamuzi.
Kwa sasa kikubwa zaidi ni kupambana kumaliza ligi wakiwa mabingwa. Wapo alama tano mbele na wamebakiza mechi nne pekee. Wahakikishe wanatetea ubingwa wao na kupambania Kombe la Shirikisho la Azam.
Kwa upande mwingine nafikiri Simba wamepata cha kujitetea iwapo Yanga watakuwa mabingwa. Kwamba mmekuwa mabingwa, lakini tumewafunga. Hali ingekuwa ngumu zaidi kama Yanga angekuwa mabingwa kisha washinde na mechi ya mtani.