UBISHI WA MZEE WA KALIUA: Bwana Pablo Franco ataweza wachezaji wakubwa?

Thursday November 25 2021
Pablo PIC
By Oscar Oscar

AMEKUWA na timu kwa siku 10 tu kabla ya mchezo wake wa kwanza lakini kuna kitu kinaonekana. Kocha wa Buyern Munich wa sasa Julian Nagelsmann aliwahi kusema “Kocha bora ni yule anayeweza kujenga mahusiano mazuri na wachezaji wake kwa asilimia 70 na asilimia 30, akawekeza kwenye mbinu.” Ndicho nilichokiona kwenye mechi ya kwanza ya Pablo.

Hakukuwa na mambo mengi lakini vijana walikuwa wanafurahia kila kitu uwanjani, hakukuwa na jina geni kwenye kikosi chake cha kwanza, hakukuwa na mbinu ngeni kwenye mfumo wake wa kwanza, hivi ndiyo makocha bora huanza kujenga timu zao.

Alianza na wachezaji wengi waliokaa na timu kwa muda mrefu, alianza na mchezaji mgeni mmoja tu Kibu Dennis, ambaye naye hakumwangusha.

Ni mwanzo mzuri sana kwake kwa kutazama umri, uzoefu na maisha ya baadaye, Pablo Franco ni mtu sahihi sana pale Simba. Ni kweli Clatous Chota Chama hayupo tena lakini Simba bado ipo sana.

Ni kweli Luis Miquessone hayupo tena Simba lakini bado ipo pale pale, wachezaji huja na kuondoka lakini, klabu siku zote huendelea kuishi.

Kikosi cha Simba dhidi ya Ruvu Shooting pale Mwanza, kilikuwa kinatukumbusha kuwa hata kama Simba wasingeongeza mchezaji hata mmoja dirisha hili la usajili, bado wanatimu ya kushindana msimu wa 2021/22.

Advertisement

Hata kama Chama na Luis wangekuwepo, huenda Simba wangeanza kwa kusuasua huku huku tulikokuona, sio jambo la ajabu. Msimu uliopita Chama na Luis wakiwepo, Simba ilianza ligi kwa kupokea vichapo kutoka Tanzania Prisons, mechi ilipigwa kule Sumbawanga, mechi iliyofuata, Simba alifungwa kwa Mkapa na Ruvu Shooting.

Pablo ameanza vizuri kwa sababu kubwa moja tu, ameamua kuanza na wachezaji waliotengeneza muunganiko kwa miaka mingi bila kuwa na haraka ya kueleta mawazo yake mapya. Hapa ndipo akili kubwa ya Kihispaniola ilipotumika.

Ukifika kwenye timu mpya, usibadilishe kila kitu, watu wengi wanadhani Simba imeanza Ligi kwa tempo ya chini kwa sababu ya kumkosa Luis na Chama, sio kweli ndugu zangu. Ni kweli hao wachezaji walikuwa tegemeo lakini, wachezaji nao ni binadamu.

Ukuta wa Simba wa sasa, ndiyo umekuwa ukuta wa Taifa Stars kwa miaka yote hii ya mafanikio, hawa wachezaji wametumika sana katika miaka minne ya hivi karibuni wamecheza Afcon, wamecheza Chan, ingefika wakati wangechoka tu.

Msimu uliopita Liverpool walikuwa wanapumulia mashine, Sadio Mane alikuwepo, Moh Salah alikuwepo, Virgil Van Djik naye alikuwepo. Hawa ni wachezaji ambao miaka minne ya hivi karibuni wametumia nguvu kubwa sana.

Wamecheza fainali ya Klabu Bingwa Ulaya mara mbili, wametwaa Ubingwa mara moja , wameshinda EPL, ilifika wakati walichoka tu, wachezaji nao ni binadamu. Pale Simba kuna wachezaji wametumika sana kwenye timu ya Taifa na Klabu, kama binadamu, kuna kuchoka.

Unahitaji kumpata kocha mzuri ambaye atajua pa kuanzia kama Pablo, kwa timu kubwa aina ya Simba hawawezi kujenga timu mpya bila kushinda mataji, wakati unajeng timu mpya ni lazima ushinde mechi, ni lazima ushinde mataji. Pamoja na kuwa Simba wanalazimika kujenga timu yao lakini, wanataka kuona mwisho wa msimu wakitetea ubingwa wao wa Ligi Kuu na ule wa Kombe la Shirikisho la Azam.

Ndiyo Pablo karudi kuitazama upya ramani ya vita, Simba wamefanya usajili mzuri lakini haujaanza vyema, karibu wote wanahitaji muda, karibu wote bado wana uchanga, wanahitaji kuingia taratibu kwenye mfumo wa Pablo, wanahitaji taratibu kuendelea kuizoea Ligi.

Wakati haya yote yakiendelea, Pablo anahitaji kushinda mechi zake na kupunguza mwanya wa alama baina yake na vinara wa ligi, Yanga, ile Kanuni ya kocha wa Bayern Munich, Julian Nagelsmann ni muhimu sana kwa Pablo, mahusiano mazuri na hasa ya wachezaji waandamizi ndani ya Simba, yatambeba sana kama atafanikiwa.

Hakuna mchezaji hasa ‘Senior’ atakayemfurahia kocha kumuweka Benchi, kila mchezaji mkongwe anataka kucheza, akifanikiwa kuleta furaha kwa wachezaji, atakuwa na wakati mzuri sana pale Msimbazi.

Pale Simba kuna mitihani mikubwa mitatu ambayo Pablo lazima aifaulu, kwanza ni kuipeleka Simba hatua ya makundi kwenye Kombe la Shirikisho Afrika. Najua hayakuwa malengo ya Simba msimu huu lakini baada ya kutolewa Ligi ya Mabingwa Afrika, hili ndiyo eneo lililobaki la kujipoza machungu. Simba anahitaji walau kufika Robo fanili ambapo Pablo akiwafika hapo, atakuwa na mwanzo mzuri .

Mtihani wa pili ni kumfunga mtani, Desemba 11, ni bora Pablo akaambiwa mapema tena ikiwezekana wamtafutie mkalimani ili ambiwe umuhimu wa Derby ya Kariakoo kwake hata kama ni kwa Lugha ya Kihispania. Kwa Tanzania unaweza kuwapa watu kila kitu, lakini kufungwa kwenye mechi hii hakuna anayekuelewa.

Pablo lazima ashinde kwa sababu mechi ya Ngao ya Jamii, tayari Mnyama alichezea vitasa kuanzia kwa Yanga, unaweza kuwa unaongoza ligi, unaweza kuwa timu umeifikisha Robo Fainali ya Afrika lakini kichapo kwenye Kariakoo derby kikaondoka na wewe. Hapa lazima aambiwe ukweli, mwishoni, Pablo anatakiwa kuyarudisha Mataji msimbazi.

Ni kweli Simba amekuwa Bingwa wa Tanzania mara nne mfululizo lakini, msimu huu kuna ugumu mkubwa. Yanga wa msimu huu, ni tofauti na wale wa miaka minne iliyopita, walau sasa wana timu ya kushindania ubingwa wamejaza wanaume haswa kikosini na huu sio mtihani mdogo kwa Pablo.

Hakuna mwenye njaa tena pale Jangwani, hakuna anayedai tena mshahara lakini, itoshe tu kusema kuwa Pablo ameanza vizuri, akidumisha mahusiano yake na wachezaji, atafanikiwa kuijenga Simba imara.

Advertisement