Pablo: Tumeshinda ila sijaridhika

Monday November 22 2021
pablo pic
By Clezencia Tryphone

KOCHA Pablo Franco ana mbwembwe huyo, kwani licha ya kuiongoza Simba kwa mara ya kwanza na kushinda kwa kishindo mabao 3-1 dhidi ya Ruvu Shooting, amesema hajaridhika na soka lililopigwa na timu yake kwa ukubwa iliyonayo.

Simba ilipata ushindi huo kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, jijini Mwanza huku ikiupiga mwingi tofauti na ilivyokuwa chini ya Didier Gomes aliyeajiriwa timu ya taifa ya Mauritania.

Licha ya ushindi huo ulioipa Simba pointi tatu muhimu na kufikisha 14 baada ya kucheza mechi sita katika ligi hiyo kwa msimu huu, Kocha Pablo alisema katika mchezo huo kuna mapungufu mengi ameyaona kwa vijana wake na sasa anaenda kuyafanyia kazi kabla ya michezo yao ijayo ukiwamo wa Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Red Arrows ya Zambia watakaocheza nao Novemba 28, jijini Dar es Salaam.

“Nimefurahishwa na matokeo, lakini kwa ukubwa wa Simba tulistahili kupata zaidi ya hiki tulichokipata, naenda kuyafanyia kazi mapungufu niliyoyaona,” alisema Pablo.

Hata hivyo, kocha huyo kutoka Hispania alisema ushindi huo utazidisha morali kwa wachezaji wake kuelekea michezo ijayo ya ligi sambamba na ile ya Kombe la ASFC na CAF.

Pablo alisema aliongea na wachezaji wake kabla ya mchezo hivyo kwa namna ambavyo wamefanya kipindi cha kwanza ndicho kitu alichokuwa anakihitaji, kabla ya kupungua makali kipindi cha pili kilichotawaliwa zaidi na wenyeji wao.

Advertisement

Naye Kocha Msaidizi Hitimana Thiery aliwapongeza wachezaji wote kwa namna ambavyo walipambana kuhakikisha timu unapata matokeo katika uwanja wa ugenini.

“Wote wamefanya vizuri kusema kweli siwezi kusema mchezaji mmoja mmoja, wote wamepambana timu imepata matokeo tunamshukuru sana Mungu kwa hilo,” alisema Hitimana, aliyeshindwa kujizuia kwa kumpokea kipa Ruvu,Mohamed Makaka kwa namna alivyopambana kuokoa michomo mingi.

“Yule kipa anajua majukumu yake amewasaidia sana bila ya hivyo zilikuwa bao nyingi sana tungeshinda, nampongeza kwa juhudi zake binafsi kuusaidia timu yake,” alisema.

Kwa upande wake Makaka alisema mchezo huo ulikuwa mgumu kwao kutoka na namna Simba walivyokuwa wakilishambulia lango lao.

Alisema Simba walimsumbua sana na ndio maana akili yake ilikuwa uwanjani kuhakikisha anapunguza idadi ya mabao.

“Mechi ilikuwa ngumu, Simba walikuwa na kasi kubwa wanapanda na kushuka wote wanazuia na kushambulia hivyo ilinifanya hata mimi kuzidisha umakini zaidi,” alisema Makaka aliyeokoa penalti ya Erasto Nyoni ambayo ingeipa Simba bao la nne juzi.

Juu ya penalti hiyo alisema “Kazi yangu ni kuhakikisha lango langu halitikiswi lakini sina namna inapotokea nafungwa ni sehemu ya mchezo tu, tunajipanga mechi zijazo.

Advertisement