Tumewasha mitambo, Pablo aanza na mzuka

Kocha mkuu wa Simba Pablo Franco. Picha | Simba

MWANZA. MASHABIKI wa Simba jana walipata raha, baada ya kushuhudia chama lao likirudi kwenye Ligi Kuu Bara kwa kishindo chini ya kocha mpya, Pablo Franco kwa kuinyoosha Ruvu Shooting kwa mabao 3-1 katika mchezo mtamu uliopigwa kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, jijini hapa.

Ikicheza soka tamu lililokuwa limepotea katika mechi tano zilizopita za ligi hiyo, Simba iliwakimbiza Ruvu waliokuwa wenyeji wa mchezo huo, huku mkongwe Meddie Kagere ‘MK14’ akiwasha moto kwa kufunga mara mbili na Kibu Denis akifunga bao lake la kwanza akiwa na kikosi hicho cha Msimbazi.

Kocha Pablo aliye na siku 10 tu tangu ajiunge na timu hiyo alijitofautisha na mtangulizi wake, Didier Gomes, kwa namna timu yake ilivyocheza soka la pasi na maelewano makubwa kwa wachezaji wa timu hiyo, tofauti na ilivyokuwa kwenye mechi zao tano zilizopota.

Katika mchezo huo, Kocha Pablo alimuanzisha Pascal Wawa sambamba na Joash Onyango katika beki ya kati, huku akiwaanzisha viungo wanne wakiongozwa na Jonas Mkude, Hassan Dilunga, Mzamiru Yassin na Bernard Morrison waliowasaidia Kibu na Kagere eneo la ushambuliaji.

Tofauti na ilivyocheza katika mechi yao iliyopita dhidi ya Yanga, Ruvu ilianza kwa kusuasua na kuruhusu mashambulizi ya Simba langoni mwao kwa muda mrefu na kumpa kazi kipa wao, Mohammed Makaka kuokoa michomo mikali kama alivyofanya dhidi ya Yanga.

Ndipo katika dakika ya 17, Kagere alifungua karamu ya mabao kwa kuunganisha kona ya Morrison na kuufanya mchezo kuchangamka kabla ya Kagere kutupia bao la nne kwake msimu huu na la pili kwa jana akimalizia mpira uliotemwa na Makaka aliyeokoa shuti kali la pembeni la Kibu dakika ya 37. Kagere sasa amemfikia Vitalis Mayanga wa Polisi Tanzania kama vinara wa mbio za ufungaji bora.

Sekunde chache kabla ya mapumziko Simba iliandika bao lake la tatu kupitia Kibu na kuifanya timu hiyo iende mapumziko ikiwa mbele kwa mabao 3-0.

Katika kipindi hicho cha kwanza, Morrison alionyesha soka tamu na kuwasumbua mabeki wa Ruvu, licha ya mara kadhaa kuchezewa madhambi ambayo yalionwa vyema na mwamuzi Ahmed Aragija.

Kipindi cha pili timu zote zilifanya mabadiliko yaliyoongeza kasi ya mchezo, huku Simba ikionekana kuimarika zaidi na dakika ya 63 Elius Maguli alifumua shuti kali la mbali na kumtungua Aishi Manula ambaye alikuwa ndiye kipa pekee aliyekuwa hajaruhusu bao langoni mwake katika Ligi Kuu kwa msimu.

Ruvu pia ndiyo timu iliyotibua rekodi ya kipa wa Yanga, Diarra Djigui aliyekuwa hajafungwa baada Shaban Msala kumtungua kwenye mechi ambayo Ruvu ilipoteza kwa mabao 3-1, huku mchezaji wao mmoja akilimwa kadi nyekundu na kutolewa penalti iliyowekwa kimiani na Mukoko Tonombe.

Jana, kKatika dakika ya 72, Simba ilipata penalti baada ya Kibu kuchezewa faulo, lakini mtokea benchini, Erasto Nyoni alishindwa kuukwamisha wavuni baada ya kipa Makaka kuupangua na kuwa kona ambayo haikuzaa matunda. Hiyo ilikuwa ni penalti ya pili kukosa kati ya tatu walizopata Simba katika Ligi ya msimu huu, ya kwanza ikiwa ni ile dhidi ya Biashara United iliyopotezwa na John Bocco.

Ushindi huo wa jana ni wa kwanza mkubwa kwa Simba msimu huu, kwani katika mechi zake tano za awali ilishinda mechi tatu kwa bao 1-0 dhidi ya Dodoma Jiji, Polisi Tanzania na Namungo.

Matokeo hayo yameifanya Simba kufikisha pointi 14, moja pungufu na walizonazo vinara Yanga ambao leo wanavaana na Namungo mjini Lindi.


MAKOCHA KUSHUHUDIA

Makocha wa Simba leo watakuwa na muda wa kutosha kuishuhudia kwa kina Yanga ikicheza katika mechi yao ya ugenini dhidi ya Namungo.

Kocha Pablo ataitumia mechi hiyo na nyingine ile inayofuata baada ya hii ya leo, ambayo Yanga watacheza ugenini pia dhidi ya Mbeya Kwanza kuwasoma wapinzani wao kabla ya kukutana nao Wanajangwani katika dabi yake ya kwanza ya Kariakoo itakayopigwa Desemba 11..


POLISI YAFA TENA

Katika mchezo mwingine uliopigwa jioni sambamba na pambano la Mwanza, Polisi Tanzania ikiwa nyumbani mjini Moshi, ilikubali kichapo cha bao 1-0 kutoka kwa Coastal Union.

Bao hilo pekee lililoizamisha Polisi kwenye Uwanja wa Ushirika, Moshi liliwekwa kimiani na Benedictor Jacob dakika ya 46 na kuifanya Coastal kupata ushindi wake wa kwanza msimu huu na kufikisha pointi 7 baada ya kucheza mechi sita na Polisi kusaliwa na alama 10.

Vikosi vilivyoanza;

RUVU: Makaka, Chilambo, Ngalema, Ponera, Masinda, Dabi, Kombo, Buswita, Maguli, Maganga na Msala

SIMBA: Manula, Kapombe, Tshabalala, Onyango, Wawa, Mkude, Dilunga, Mzamiru, Kagere, Kibu na Morrison.