Ubinde; Meneja aliyewabeba kina Abdi Banda
Muktasari:
- Ni meneja aliyemtengeneza Abdi Banda na vipaji vingine vilivyoipa heshima Coastal Union na ni miongoni mwa watu wenye mchango mkubwa wa kukuza vipaji vya vijana wadogo.
UKITAJA mafanikio ya Coastal Union ya vijana huwezi kukosa jina Abdulrahman Ubinde.
Ni meneja aliyemtengeneza Abdi Banda na vipaji vingine vilivyoipa heshima Coastal Union na ni miongoni mwa watu wenye mchango mkubwa wa kukuza vipaji vya vijana wadogo.
Coastal ni moja ya klabu zilizowekeza kwa vitendo katika soka la vijana kwa muda mrefu na imekuwa na mwendelezo wa kupandisha vijana hadi timu ya wakubwa.
Katika mafanikio hayo ya kupandisha vijana, ndipo Ubinde anapohusika kutokana na kujitoa kwake bila kuchoka na safari yake imejaa simulizi nyingi ikiwamo nidhamu, kujituma na mapenzi na soka.
HAJACHEZA SOKA
Anasema ingawa hakucheza soka la ushindani, lakini alipenda sana mchezo huu na alipata bahati ya kutua Coastal na kupewa kazi maalumu ya kusaka vipaji hadi kuwa meneja wa timu ya vijana U17 na U20, akiwa pia mwanachama wa klabu hiyo kwa muda mrefu.
“Nilikuwa naupenda soka lakini sikucheza levo ya ushindani kama vijana wengine, Coastl nilipata nafasi ya kuwa meneja baada ya kuwa mwanachama wa muda mrefu, nikaanza na kutafuta vipaji kila kona ya Handeni (Tanga) na nikisikia kuna mechi naenda kuangalia kisha nachukua wachezaji baadhi ninaoona wanafaa na kuwasajili timu za vijana.”
AIFAIDISHA COASTAL
Anasema mwaka 2010 ulikuwa msimu bora na timu ilitengenezwa kutokana na wachezaji wengi waliotokea timu ya vijana aliowatafuta yeye.
“Wachezaji wengi wamepita kwangu nikiwa meneja wa timu za vijana wakati ule tulikuwa na mikakati na mipango madhubuti na timu kubwa baadae ilifaidika na vijana hao,” anasema Ubinde na kuongeza;
“Kwa wakati ule nilipata sifa nyingi na nikaaminiwa zaidi na timu kwa sababu wachezaji walikuwa wengi wazuri kama kina Banda, Mwaita Gereza, Mohamed Banka na Ally Nassor Ufudu.”
ANAKOTOA VIPAJI
Anasema vipaji vingi alivyoviibua ni kutokana na kutembelea viwanja mbalimbali kila anaposikia kuna mechi.
“Mimi ni ‘blader’ wa mpira kwa sababu kabla sijapandishwa kuwa meneja wa timu kubwa nilikuwa nakwenda viwanja tofauti kama Handeni, Tanga Mjini na sehemu nyinginezo za mkoa wa Tanga,” anasema na kuongeza;
“Kwa hiyo kila ninapopita nilikuwa naangalia vipaji vya vijana, tunakuja tunawasajili timu ya vijana tunawatengeneza wakae kiushindani kisha tunawapandisha timu kubwa na hapo ndio ilipokuwa siri kubwa ya kutoa wachezaji wengi wazuri wakati ule.”
WANACHAMA, VIONGOZI
Anasema siri ya Coastal kuwa moja ya timu inayofanya vizuri kwa madaraja ya kati ni pamoja na ushirikiano mzuri wa wanachama, mashabiki pamoja na viongozi.
“Mkoa wa Tanga watu wanapenda mpira, kuna wanachama wengi wanaoipenda klabu hii na hadi leo wako tayari kujitolea kuhakikisha timu inafanya vizuri, nafikiri hiyo ndiyo sababu mnaposhirikiana basi mambo yanakwenda vizuri.”
“Huwa tunawashirikisha mipango ya timu hadi wale mashabiki wetu ambao hata tuende wapi tupo nao, wanatupa ushauri wapi tufanyie kazi na tunafanya kweli kwa sababu wao pia ni sehemu ya timu.”
MSIMU HUU
Anasema msimu uliopita hawakufanya vizuri ila huu wamejipanga vilivyo kuhakikisha ile Coastal yenye ushindani inarudi na kuleta sura mpya kwenye ligi.
“Msimu uliopita tulikosea hatukufanya vizuri lakini tunashukuru Mungu tulisalia ligi kuu. Tulikaa kama viongozi na kuangalia wapi tumekwama ili turekebishe tukasahihisha na bado maboresho yataendelea kuwepo.”
TAWI LA SIMBA
Anafafanua Coastal ni timu inayojitegemea na wala siyo tawi la Simba kama watu wanavyofikiria au kuona.
“Watu huwa wana mawazo tofauti, sisi sio tawi la Simba ni timu inayojitegemea na labda wanasema kutokana na ushindani tunaouonyesha kwa timu hizo kubwa.”
DABI YA TANGA
Ubinde anaongeza miongoni mwa vitu anavyotamani pamoja na viongozi wengine wa timu ni kuona dabi ya Tanga inarejea kwani ilikuwa inachangamsha mkoa huo.
“Tunaumizwa kuona wenzetu African Sports wanafanya vibaya kwa sababu tunatoka mkoa mmoja. Tunawaombea wafanye vizuri na kurejea ligi kuu ili ule mshikemshike urejee tena Tanga,” anasema Ubinde.
“Kusema ukweli tumeimisi dabi ya Tanga. Ilikuwa ikitoka Kariakoo Dabi basi ile inafuata, uwanja huu ulikuwa unajaa, mashabiki na wanachama walikuwa wanatishiana nje ya uwanja yaani ilikuwa amsha amsha sana na jiji lilikuwa linapendeza.”
“Hakukuwa na mambo ya uchawi vile vilikuwa vitisho tu kutoana mchezoni, ukijichanganya imekula kwako na unasahau kufanya mazoezi unaamini kweli lakini kusema mambo yale yapo, hapana.”
MAFANIKIO
Anasema mwaka 2010/11 timu ya vijana kwa mara ya kwanza ilishiriki mashindano ya Rolling stone yalifanyika Burundi na Coastal Union iliibuka mshindi wa pili.
“Hayo ndiyo mafaniko makubwa niliyoyapata nikiwa meneja wa timu za vijana ukiachana na kutengeneza vipaji vikubwa, tuliwahi kuchukua ubingwa Burundi,” anasema Ubinde.
“Msimu wa 2013/14 tulifika tena fainali ya mashindano ya Uhai Cup na tukachukua ubingwa kwa hiyo hayo ni mafanikio makubwa ambayo niliyapata, tulikuwa na wachezaji nawakumbuka Fikirini Bakari, Abdallah Waziri, Nzara Nzara, Ayubu Semtawa, Banka na wengineo.”
VIJANA CHANGAMOTO
Anasema kuna changamoto kubwa ya kupewa kazi ya umeneja wa timu za vijana kutokana na wengi wao wanakuwa kwenye kipindi cha ukuaji ambacho kinahitaji kuwa makini kuwaelekeza ili wasipotee.
“Nilikumbana na changamoto nyingi kusimamia wachezaji hao kwa sababu nilikuwa naenda kuwatafuta, hivyo lazima wazazi wao wanikabidhi, sasa inakuwa unawalea kama watoto huku unawasimamia kimichezo.”
“Kipindi hicho wengi ndio wanachipukia na kuna vitu vingi vya anasa wanakutana navyo wengine wanashindwa kuendelea kucheza, sasa nakuwa na kazi ya ziada.”