Tutatoboa hamtaamini

New Content Item (1)

HISTORIA ya soka imeandikwa nchini baada ya timu mbili kutinga hatua ya robo fainali ya Kombe la Shrikisho Afrika na Ligi ya Mabingwa.

Timu ya Yanga, juzi Jumapili ilitinga hatua ya robo fainali baada ya kuichapa US Monastir ya Tunisia mabao 2-0 na siku moja nyuma Simba ilifuzu kwa kuishushia Horoya ya Guinea kichapo kizito cha mabao 7-0 kwenye Uwanja wa Mkapa.

Awali, Tanzania iliweka rekodi ya kuwa na timu hizo mbili zilizofuzu hatua ya makundi, lakini kwa muda mchache tumefanikiwa pia kuweka rekodi mpya ikiwa ni mara ya kwanza kwenye historia ya soka la nchi hii kupeleka timu mbili kwa pamoja robo fainali.

Pamoja na mafanikio hayo, timu hizo pia zimeweka rekodi kadhaa, huku Simba ikiwa na rekodi ya kuifunga timu mabao mengi zaidi kwenye hatua ya makundi, lakini Yanga ikiweka rekodi ya nchi hii kwa mara ya kwanza kufika hatua ya robo fainali na kuongoza kundi lake kabla ya mchezo wa mwisho.

Hata hivyo, michuano ya mwaka huu imeweka rekodi nyingine kwa Simba baada ya mchezaji wake Clatous Chama kuwa kileleni kwenye chati ya ufungaji hadi sasa wakati hatua hii bado haijamalizika.

Hata hivyo, kabla hatua hii haijafika ukingoni tayari rekodi zimeshatengenezwa kwa timu zote mbili, lakini pia michuano yote miwili msimu huu, lakini ukweli ni kwamba Yanga ina nafasi kubwa ya kutoboa kwenda nusu fainali kilaini sana, shuka nayo.SIMBA NGOMA NZITO

Simba ambayo imefika hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa mara ya tatu ndani ya miaka minne, ilianza kwa kusuasua kwenye michuano ya mwaka huu lakini baadaye ilibadili gia na kuanza kufanya vizuri kwenye michezo mitatu mfululizo, miwili dhidi ya Vipers na mmoja dhidi ya Horoya na kukusanya pointi tisa ambazo zimeipeleka hatua hiyo muhimu.

Hata hivyo, bado Simba itamaliza nafasi ya pili kwenye michuano hii na italazimika kukutana na kigogo mmoja kwenye soka la Afrika.

Timu inayomaliza kwenye nafasi ya pili inalazimika kukutana na kinara wa kundi ambapo kwa upande wa Simba ambayo mafanikio yake makubwa kwa miaka ya hivi karibuni ni kufika hatua ya robo itaweza kuwakwepa Raja Casablanca tu ambayo ipo nayo kundi moja.

Kuna uwezekano mkubwa ikakutana na JS Kabylie kutoka nchini Algeria ambayo ndiyo vinara wa Kundi A.

Hawa kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika walifanikiwa kutwaa ubingwa mara mbili mwaka 1981, 1990 au wanaweza pia kukutana na Wydad ambayo ndio bingwa mtetezi, kwa sasa inasomeka ikiwa nafasi ya pili kwenye Kundi A lakini ikiwa imelingana pointi na Kabylie na inaweza kumaliza kileleni, kwenye michuano hii imetwaa ubingwa mara tatu, mwaka 1992, 2017na 2022 na ni timu ambayo ni tishio zaidi.

Kama Simba itawakosa hawa, inaweza kukutana na kinara wa Kundi B, Mamelodi Sundowns ambayo msimu huu imeonyesha kiwango cha juu sana tofauti na misimu mingine iliyopita.

Mamelodi ambayo imeshatwaa ubingwa huu mara moja, mwaka 2016 na kushika nafasi ya pili 2001 ni kati ya timu ambazo zinapewa nafasi kubwa ya kufanya vizuri msimu huu na hata kutwaa ubingwa.

Timu hii imekusanya pointi 11, ikiwa kundi gumu pamoja na Al Hilal, Al Ahly na Coton Sport lakini ni katika kundi hili pia, Al Hilal inaweza kusogea kileleni endapo itaichapa Al Ahly kwenye mchezo wa mwisho utakaopigwa, Cairo, Misri mwishoni mwa mwezi huu.

Kama Simba itakutana na Hilal inaweza kuwa na unafuu kidogo kutokana na timu hiyo kutokuwa na historia kubwa kwenye michuano ya Afrika ikiwa ilishika nafasi ya pili mwaka 1987 na mwaka 1992.

Kundi D, kinara wake ni Esperance ya Tunisia ambayo kwenye michuano ya mwaka huu imefanikiwa kutoka sare mchezo mmoja tu kati ya mitano iliyocheza hadi sasa.

Ni timu yenye mafanikio makubwa kwenye soka la Afrika ikiwa imeshatwaa ubingwa huo mara nne mwaka 1994, 2011, 2018, 2019, siyo timu ambayo Simba inatakiwa kukutana nayo kwa sasa.


NAFASI YA PILI

Pamoja na Simba inakwenda kumaliza mchezo wa mwisho nchini Morocco dhidi ya Raja lakini bado inaonekana hata ikishinda itamaliza ikiwa nafasi ya pili na kanuni zinaonyesha timu ya pili itakuwa ikianzia michezo yake ya robo nyumbani na kwenda kumalizia ugenini jambo ambalo siyo zuri hata kidogo kwa Simba.


TAKWIMU

Kwenye hatua ya makundi hadi sasa timu moja tu ndiyo inasubiriwa huku nyingine saba zikiwa zimeshafuzu kwa hatua ya robo, Kundi B Mamelodi imeshafuzu lakini kuna nafasi moja itakayoamuliwa kwenye mchezo wa mwisho kati ya Al Ahly na Al Hilal.

Timu za Simba, Raja Casablanca, CR Belouizdad, Esperance, JS Kabylie Mamelodi na Waydad hizi zimeshafuzu kwenda hatua inayofuata.


MABAO KWA TIMU

Raja Casablanca hadi sasa ndiyo wanaongoza kwa kufunga mabao mengi ikiwa imefunga 14 ikifuatiwa na Mamelodi ambayo imefunga mabao 12, Al Ahly ina mabao 11 na Simba inashika nafasi ya nne ikiwa na mabao 9.

Vinara wa mabao

Clatous Chama wa Simba ambaye aliweka rekodi ya kuwa mchezaji pekee kufunga mabao matatu na kutoa pasi ya bao kwenye mchezo dhidi ya Horoya na Makabi Lilepo wa Al Hilal ndiyo wanaongoza kwa kupachika mabao kwenye michuano hii hadi sasa wakiwa na mabao manne kila mmoja.

Wenye mabao matatu ni Cassius Mailula wa Mamelodi Sundowns, Hamza Khabba wa Raja Casablanca, Peter Shalulile pia wa Mamelodi na Kahraba wa Al Ahly.


SIMBA KUPENYA HAPA

Hakuna kinachoshindikana kwa kuwa hadi Simba inafika hapa pia ilionekana ni jambo gumu, lakini ukweli ni kwamba inaweza kutimiza malengo ya kufika nusu fainali mwaka huu.


KOMBE LA SHIIKISHO AFRIKA

Yanga inaongoza kwenye kundi lake baada ya kukusanya pointi 10 sawa na washindani wao wakubwa Monastir ambao nao wana idadi hiyo ya pointi.

Lakini hii inaufanya mchezo wa mwisho wa kundi hili kuwa mgumu kwa timu zote mbili kwa kuwa idadi ya mabao ya kufunga na kufungwa ndiyo inaweza kutumika hapa endapo timu zote zitapata ushindi micheo yao ya mwisho.

Iko hivi, Yanga inakaa kileleni kwa tofauti ya bao moja tu, wakati Yanga inaongoza kwa bao 1-0 kwenye Uwanja wa Mkapa bado ilikuwa inaonekana ipo nafasi ya pili kwenye kundi lake lakini baada ya kufunga bao la pili ilipanda juu kwa tofauti na bado moja dhidi ya Monastir.

Kanuni inaonyesha Mashindano ya Caf jambo la kwanza ambalo wanaangalia ni pointi, la pili ni idadi ya mabao mliyofunga wakati mmekutana wenyewe na jambo la tatu ni idadi ya mabao ya kufunga na kufungwa.

Wakati Yanga ilipokutana na Monastir ilichapwa mabao 2-0 ugenini iliporudi kwenye Uwanja wa Mkapa Yanga ikashinda 2-0, hivyo ilipokutana hakuna aliyomzidi mwenzake.

Baada ya kulingana kwenye mambo yote hayo, ziliangalia idadi ya jumla ya mabao ambapo Yanga ilionekana kuwa juu kwa tofauti ya mabao ya kufunga na kufungwa, ambapo Yanga inatofauti na manne na US Monastir matatu.

Hali hii inazalisha vita kubwa kwenye mchezo wa mwisho ambapo atakayepata mabao mengi ndiye atakayemaliza kileleni kwenye kundi hilo.

Yanga ambayo itachezana TP Mazembe itatakiwa kuhakikisha inamtazama pia Monastir inafanya nini wakati ambapo itakuwa uwanjani kuvaana na Bamako. Timu zote mbili kwenye kundi hili zimeshafuzu, na mbili za chini zimeshaondoka kabisa hivyo ni mchezo ambao unaonekana Monastir na Yanga zina nafasi kubwa ya kuibuka na ushindi, lakini shida ni idadi ya mabao.

Ili Yanga iweze kujiweka katika nafasi nzuri ya kwenda nusu fainali ya Kombe la Shirikisho ni lazima ishinde dhidi ya TP Mazembe kwa idadi ya mabao ya kutosha.

Ikiongoza kundi itakutana na mshindi wa pili wa makundi mengine.


WAMEFUZU

Kombe la Shirikisho Afrika kama ilivyo kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika ni makundi mawili tu ndiyo hayajakamilika hadi sasa.

Kundi C na A ndiyo timu zake mbili hazijapata nafasi ya kufuzu kwa hatua ya robo fainali, zingine zilizofuzu zikiwa vinara kwenye kundi ni Rivers United, Marumo Gallants na ASFAR ambao bado haijafuzu kwenye kundi lake ikiwa inapambana na Pyramids pamoja na Future kuwania nafasi za kundi hilo, hivyo Yanga inaweza kukutana na mmoja kati ya hao kama atamaliza akiwa nafasi ya pili.

Lakini ikimaliza wa kwanza, inaweza pia kukutana na Pryamids, Future au ASFAR Rabat, mmoja wao kutoka kwenye kundi hili au timu ya zamani ya kiungo wao, Aziz KI yaani ASEC Mimosas ambayo imefuzu wa pili kutoka Kundi B na USM Alger ambayo bado haijafuzu lakini inashika nafasi ya pili kutoka Kundi A ikiwa na point nane.


YANGA WAKIKOMAA WANAPENYA NUSU...

Timu nyingi zinazoongoza kwenye makundi ya michuano hii hazina rekodi kubwa sana kwenye soka la Afrika.

AS Rabat imefanikiwa kuchukua ubingwa huo mara moja tu mwaka 2005 ikiongoza Kundi C, Rivers ya Nigeria inaongoza Kundi B lakini ikiwa haijafuzu bado, haina makali ikiwa ni timu changa zaidi kwenye michuano hii na haijawahi kufika hatua hii ya robo fainali.

Mwingine ambaye anaweza kukwea juu ni Asec ambayo nayo inalingana pointi na Rivers lakini ikiwa imeishia Nane Bora kwenye michuano hii ikiwa haina makali sana.

Timu nyingine ambayo haina makali lakini ipo kileleni ni Marumo ya Afrika Kusini ambayo inaonekana imeanzishwa mwaka 2021 ikiwa ndiyo mafanikio yake makubwa, zote ni kati ya timu ambazo zikikutana na Yanga inaweza kuzichapa na kwenda hatua ya nusu fainali.


MABAO

Kinara wa mabao kwenye hatua ya makundi ni Timu ya Rabat ambayo imefunga mabao 10, lakini ikifuatiliwa na Rivers mabao tisa na Marumo mabao tisa, huku Yanga ikifuatia ikiwa na mabao manane.


VINARA WA MABAO

 Paul Acquah wa Rivers anaongoza kwa mabao akiwa na manne sawa na Aubin Kramo Kouamé ASEC Mimosas. Wenye mabao matatu ni Fiston Mayele wa Yanga, Ranga Chivaviro wa Marumo Gallants, Boubacar Traoré wa Monastir na Mostafa Fathi wa Pyramids.