Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Tunaitaka robo fainali CAF

Robo Pict

Muktasari:

  • Kuanzia kwa walio benchi la ufundi chini ya Kocha Sead Ramovic, wachezaji hadi mashabiki wamekuwa wakisisitiza kwamba mechi wanaitaka.

HAKUNA namna ila ni ushindi tu ambao Yanga inahitaji leo katika mechi ya mwisho ya Kundi A la Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya MC Alger.

Kuanzia kwa walio benchi la ufundi chini ya Kocha Sead Ramovic, wachezaji hadi mashabiki wamekuwa wakisisitiza kwamba mechi wanaitaka.

Na robo fainali wanaitaka sana ili kuweka heshima mjini.Ndio. kama hujui ni kwamba Yanga itakuwa wenyeji wa Mc Alger kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, jijini Dar es Salaam na ushindi utaivusha kucheza robo fainali kwa msimu wa pili mfululizo ikiwa ni historia kwa klabu hiyo kwa miaka ya karibuni.

Lakini Yanga ikipiga hesabu hizo, wapinzani wao wanaomba sare ili waungane na Al Hilal inayoongoza kundi hilo kwenda  robo fainali kwani pointi nane ilizonazo kwa sasa zinaibeba iwapo itavuna sare ugenini.

Hali ikiwa hivyo kwa Yanga leo, watani wao Simba wenyewe wanashuka uwanjani kesho Jumapili kumalizana na timu nyingine kutoka Algeria, CS Constantine inayoongoza Kundi A la Kombe la Shirikisho Afrika, licha ya kwamba zote mbili zimeshafuzu robo fainali.

HIS 01

Kifupi ni kwamba ni wikiendi iliyotawaliwa na mechi nyingi za kusisimua. Ukiachana na Yanga na Simba, pia kuna mechi zingine za michuano hiyo ya CAF za kuvutia zikiwemo pia za kusaka nafasi.

Katika Ligi ya Mabingwa Afrika timu sita zimefuzu robo fainali kati ya nane ambazo ni Al Hilal (Kundi A), AS Far Rabat (Kundi B), Orlando Pirates na Al Ahly (Kundi C) na Esperance na Pyramids (Kundi D).

Mechi za wikiendi hii kwa Kundi B, vinara AS Far Rabat wenye pointi tisa wapo ugenini kwa Mamelodi Sundowns wanaosaka ushindi ili kufikisha pointi 11 kufuzu kisha kuongoza kundi, lakini hata sare inawavusha.

Raja Casablanca ikiwa na pointi tano inahitaji ushindi nyumbani mbele ya AS Maniema ili ifuzu lakini pia ikiombea Mamelodi ipoteze.

HIS 02

Kundi C ni vita ya nafasi ya kileleni, Al Ahly (10) inaikaribisha Orlando Pirates (11). Ushindi kwa Al Ahly utaiweka kileleni lakini sare kwa Orlando itabaki kileleni.

CR Belouizdad dhidi ya Stade d’Abidjan wanakamilisha ratiba. Kundi D Esperance (10) na Pyramids (10) zimeshafuzu, lakini kuna mechi za mwisho kuamua nani akae kieleni. Esperance dhidi ya Sagrada ilhali Pyramids na Djoliba.

Kombe la Shirikisho napo timu sita kati ya nane zimefuzu ambazo ni CS Constantine na Simba (Kundi A), RS Berkane na Stellenbosch (Kundi B), USM Alger (Kundi C) na Zamalek (Kundi D). Mechi za kundi B, RS Berkane dhidi ya Stellenbsch na Stade Malien dhidi ya Desportivo da LS zinakamilisha ratiba kwani haiwezi kubadili chochote timu mbili zilishafuzu.

Kundi C kuna USM Alger dhidi ya Jaraaf na Asec Mimosas dhidi ya Orapa United.

HIS 03

Jaraaf inahitaji sare kujihakikishia nafasi ya pili kutokana na sasa kuwa na pointi nane, wakati Asec inataka ushindi ifikishe pointi nane kutoka tano huku ikiiombea mabaya Jaraaf ili yenyewe ifuzu ikiwa nafasi ya pili nyuma ya USM Alger.

Asec ikifikisha pointi nane itakuwa sawa na Jaraaf, lakini matokeo walivyokutana yanaibeba kwani kwake ilishinda 2-0, Jaraaf nayo ikashinda 1-0, hivyo Asec ina faida ya bao moja.

Kundi D tayari Zamalek imefuzu nafasi imebaki kwa timu tatu ambazo ni Al Masry (6), Enyimba (5) na Black Bulls (4) kila moja inaweza kufuzu.

Vinara Zamalek wanawakaribisha Enyimba, wakati Al Masry wakiwa wenyeji wa Black Bulls. Al Masry inahitaji ushindi pekee kufikisha pointi 9, Enyimba anahitaji kushinda na kuwaombea wapinzani wake watoke sare ili yeye awe na pointi 8, wakati Black Bulls ikiomba kushinda ifikishe pointi 7 ifuzu huku maombi yake yakiwa kwa Enyimba ipate hata sare.


YANGA VS MC ALGER

Ni mechi ambayo inapigwa leo kuanzia saa 10:00 jioni kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam huku mwamuzi wa kati akiwa Patrice Milazare raia wa Mauritius mwenye rekodi ya kuchezesha mechi tatu msimu huu zote zikimalizika kwa matokeo ya 0-0.

Mchezo wa kwanza uliopigwa Algeria, wenyeji MC Alger walishinda 2-0, hivyo Yanga ina ulazima wa kushinda kwanza ili kulipa kisasi, pili kufuzu robo fainali na tatu kukusanya pointi 39 zitakazoipandisha katika chati ya ubora ya CAF kutoka namba 10 hadi sita na kuishusha Simba yenye pointi 38.

HIS 04

“Tunarudi uwanja wa nyumbani kucheza dhidi ya MC Alger, hatutarajii mchezo rahisi utakuwa mgumu na wa ushindani,” alisema kocha wa Yanga, Sead Ramovic.

“Tutaingia kwa kuwaheshimu wapinzani wetu, hawana timu mbovu, ni bora na washindani, kazi kubwa tunayotakiwa kufanya ni kutumia kila nafasi tutakayotengeneza huku tukijilinda kuhakikisha hatufanyi makosa eneo la ulinzi.”

Mshambuliaji Sofiane Bayazid ndiye mchezaji hatari kwenye kikosi cha MC Alger kwani ndiye aliwaadhibu Yanga mechi ya kwanza bao la pili dakika ya 90+5. Pia amewafunga Al Hilal. Kati ya mabao manne ya kikosi hicho, mawili ni yake akiwa kinara wao.

Hata hivyo, Yanga imekuwa imara katika kufunga mabao kwani tangu ipate sare ya 1-1 ugenini kwa TP Mazembe katika mechi ya tatu, mbili zilizofuatia imefunga mabao manne ikishinda 3-1 dhidi ya TP Mazembe na 1-0 dhidi ya Al Hilal jambo linaloashiria kwa sasa Yanga ina uwezo wa kufunga tofauti na mechi mbili za kwanza ilipopoteza 2-0 mbele ya Al Hilal na kichapo kama hicho kwa MC Alger.

Mabadiliko ya kiuchezaji Yanga yameonekana kuwatisha MC Alger ambapo kocha wao, Khalid Bin Yahia alisema: “Algeria hakuna asiyeifahamu Yanga. Huo ndio ukweli, ni klabu yenye wachezaji wapambanaji na imara kimwili dakika zote 90. Wachezaji wetu wanajua ugumu watakaokutana nao Tanzania, lakini jambo jema ni kwamba hata sare inatosha kutupeleka robo fainali.”

Kocha huyo alibainisha kwamba katika mchezo huo atawakosa kiungo Mohamed Zougrana na bek Merwane Khelif kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo za kiafya.

Wakati MC Alger ikiwakosa nyota hao, Yanga haitakuwa na huduma ya beki wa kulia, Yao Kouassi ambaye amefanyiwa upasuaji wa goti na enka akitarajiwa kuwa nje ya uwanja kwa takriban wiki nne hadi sita.

Hata hivyo, kutokana na MC Alger kuwa na uhitaji zaidi wa sare kuliko ushindi, itaifanya Yanga kuwa makini zaidi na mbinu chafu za kiuchezaji ambazo timu za Ukanda wa Kaskazini mwa Afrika zimekuwa nao.

Mbinu hizo ni za kupoteza muda ambapo inapotokea faulo, mpira wa kurusha, goal kick au hata kufanya mabadiliko ya wachezaji, hutumia muda mwingi kutekeleza jambo hilo.

Kitu kingine ni kwa wachezaji kujiangusha mara kwa mara uwanjani ili tu kupoteza moja. Hapa lazima Yanga wawe macho ikiwezekana kutangulia kufunga bao, wakiruhusu kufungwa wao, mlima utakuwa mrefu na kazi rahisi kwa MC Alger.

HIS 06

Yanga ikitinga robo fainali, inaweza kukutana na timu mojawapo kati ya hizi; AS Far Rabat (Morocco) au Mamelodi Sundowns (Afrika Kusini) kutoka Kundi B, Orlando Pirates (Afrika Kusini) au Al Ahly (Misri) za Kundi C, Esperance (Tunisia) au Pyramids (Misri) zilizopo Kundi D.

Huku Ligi ya Mabingwa timu moja pekee ambayo ni Al Hilal ndiyo imejihakikisha kukaa kileleni lakini zingine licha ya kufuzu robo fainali, bado hazina uhakika wa kukaa kileleni mpaka mechi za mwisho wikiendi hii.


SIMBA SC VS CONSTANTINE

Mechi hii itachezwa bila ya mashabiki baada ya CAF kuifungia Simba kutokana na vurugu zilizotokea Desemba 15, 2024 ilipoifunga CS Sfaxien mabao 2-1. Adhabu hiyo ya kutocheza mechi moja ya nyumbani bila ya mashabiki imeendana na faini ya dola 40,000. Awali Simba ilitakiwa icheze mechi mbili za nyumbani bila mashabiki lakini adhabu imepunguzwa.

Kocha wa Simba, Fadlu Davids ameona kucheza bila ya mashabiki ni adhabu kubwa sana kwao kwani anafahamu nguvu ya mashabiki ya timu hiyo katika kusaka matokeo mazuri.

“Tulitarajia kuujaza uwanja lakini haiwezekani kwa sababu ya adhabu tuliyopewa ambayo naona haikuwa ya haki kwetu,” alisema Fadlu.

Hata hivyo, Fadlu alisema adhabu hiyo haijamtoa katika malengo kwani anachotaka mchezo huo utakaochezwa kuanzia saa 10:00 jioni kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa ni kushinda ili kuongoza kundi.

HIS 05

“Tuna shauku kubwa ya kushinda mechi hii na kuingia raundi inayofuata kama vinara wa kundi. Ni bora kwetu kujaribu kushinda iwe kuna mashabiki au hakuna. Kwa mapenzi ya Mungu tutafanikiwa,” alisema Fadlu ambaye ana mtihani mwingine baada ya kufaulu ule wa kwanza wa kufuzu robo fainali akifuata nyayo za watangulizi wake waliofanya hivyo katika kipindi cha misimu sita nyuma ambapo timu hiyo imefuzu robo fainali ya CAF hii ikiwa ni mara ya saba ndani ya muda huo.

Fadlu amebakisha mtihani wa kuivusha Simba kutoka robo kwenda nusu fainali - nafasi ambayo timu hiyo imekuwa ikiisaka kwa muda mrefu bila ya mafanikio. Msimu huu tusubiri tuone. “Ni muhimu kwetu kumaliza hatua ya makundi tukiwa vinara, kwa sababu itatuepusha na baadhi ya timu kubwa kama Zamalek ambao wana uzoefu mkubwa, lakini hata Al Masry hivi sasa inafanya vyema na inaonekana ni timu ngumu na yenye nguvu, lakini kama unataka kushinda mashindano haya lazima uwe tayari kujiandaa na kufanya mambo iwe rahisi kwako.

“Kumaliza kundi ukiwa wa kwanza hii itafanya mambo kuwa rahisi kwetu katika hatua inayofuata. Ukiangalia kwa sasa timu yoyote itakayokutana na Simba itapambana kujaribu kushinda iwe ya kwanza au ya pili katika kundi, hivyo kuna ugumu,” alibainisha Fadlu.

Kocha huyo raia wa Afrika Kusini, anafahamu kumaliza kinara hatua inayofuata ya robo fainali timu itaanzia ugenini na kumalizia nyumbani, hivyo ukichanga vizuri karata inaweza kukuvusha kirahisi kucheza nusu fainali. Wakati Yanga inashiriki Kombe la Shirikisho Afrika 2022/2023, ilikwenda hadi fainali kwa mtindo huo.

Ilimaliza kinara wa Kundi D, ikaanzia ugenini robo fainali ikaichapa Rivers United 2-0, nyumbani ikaja kumaliza kazi kwa 0-0. Nusu fainali ikaanzia nyumbani dhidi ya Marumo Gallants ikashinda 2-0 na ugenini pia ikashinda 2-1 kabla ya fainali kuanzia nyumbani na kufungwa 2-1 dhidi ya USM Alger, licha ya ugenini ikaenda kushinda 1-0 lakini faida ya bao la ugenini ikawabeba USM Alger wakawa mabingwa.

Lakini Simba itakumbuka msimu wa 2020-2021 katika Ligi ya Mabingwa Afrika ilianzia ugenini dhidi ya Kaizer Chiefs ikafungwa 4-0, nyumbani ikaja kushinda 3-0 lakini haikutosha kuwavusha kwenda nusu fainali kutokana na tofauti ya mabao. Hilo liwe somo kwao katika hesabu zao za msimu huu kwani ukiachana na msimu huo pekee katika mara tano nyuma ilizocheza robo fainali, nne ilianzia nyumbani na kwenda ugenini kutolewa.

Katika mchezo wa kesho dhidi ya Constantine, yale makosa ya safu ya ulinzi yasiwepo ili kutimiza malengo.

Ilishuhudiwa mchezo wa kwanza ugenini kwa Constantine, Simba ilianza kufunga bao kupitia Mohamed Hussein, lakini makosa ya safu ya ulinzi yakawapa faida wenyeji wakaibuka na ushindi wa mabao 2-1 likiwemo la beki Abdulrazack Hamza kujifunga likiwa ni la kusawazisha kwa Constantine dakika ya 46 kabla ya Brahim Dib naye kutumia udhaifu wa safu hiyo kuweka la ushindi dakika ya 50. Ndani ya dakika tano Simba iliruhusu mabao mawili.

Che Malone Fondoh ambaye amefanya makosa mawili yaliyowapa faida wapinzani hatua ya makundi, anapaswa kujirekebisha kwa kuboresha kiwango chake kama hapo awali kwani ni beki anayetumainiwa pale kati akisimama na Hamza.

Endapo Simba itamaliza kinara wa kundi A katika Kombe la Shirikisho Afrika, mpinzani wake anaweza kuwa Stellenebosch (Afrika Kusini), ASC Jaraaf (Senegal) au ASEC Mimosas (Ivory Coast), Al Masry (Misry), Enyimba (Nigeria) au Black Bulls (Msumbiji). Timu hizo mojawapo itakutana na Simba.

Lakini ikiwa nafasi ya pili, inaweza kucheza dhidi ya RS Berkane (Morocco), USM Alger (Algeria) na Zamalek (Misri).