Sunderland klabu zenye historia kubwa soka la Afrika

Muktasari:
- Klabu ya Simba ya Tanzania iliyoanzishwa 1936 kwa jina la Queens, labda kuonyesha mapenzi kwa Malkia Elizabeth Angela Marguerite Bowes-Lyon, aliyekuwa mke wa Mfalme wa Uingereza, George VI, babu wa Charles ambaye ni mfalme wa sasa.
KUANZIA mwanzoni mwa miaka ya 1930 moja ya klabu za soka duniani zilizopata umarufu na hata timu za Afrika, Asia na Carribbean nazo kujipa jina hilo ni Sunderland ya England.
Klabu ya Simba ya Tanzania iliyoanzishwa 1936 kwa jina la Queens, labda kuonyesha mapenzi kwa Malkia Elizabeth Angela Marguerite Bowes-Lyon, aliyekuwa mke wa Mfalme wa Uingereza, George VI, babu wa Charles ambaye ni mfalme wa sasa.
Hata hivyo, timu hiyo ambayo wanachama na mashabiki wake walikuwa vijana na wazee wa Kariakoo, Jangwani, Gerezani, Magomeni Mapipa na Ilala - Dar es Salaam ilipofaulu kuwa moja ya timu zitazocheza Ligi ya Kwanza iliyoanzishwa ukanda wa pwani 1948 ilibadili jina na kuitwa Sunderland.
Jina la Simba lilianza kutumika 1971 pale klabu zote nchini zilipotakiwa kutumia majina yenye asili ya Tanzania. Wakati ule klabu nyingi Bara na Zanzibar zilikuwa na majina ya timu za Uingereza.
Miongoni mwa klabu zilizokuwa na majina ya aina hiyo ni Manchester (Tanga), Liverpool (Dar es Salaam) na Wolverhampton Wanderers (Zanzibar).
Miongoni mwa nchi ambapo klabu zenye jina la Sunderland hadi leo zipo ni pamoja na Sunderland FC ya Auckland (New Zealand) na Sunderland ya Naivasha (Kenya).
Sunderland ambayo ilipoundwa ilikuwa ni timu ya walimu wa shule hivi karibuni ilirudi katika Ligi Kuu England (EPL), baada ya kushuka na kusota ligi za chini kwa miaka minane. Timu hiyo ilikata tiketi kwa kufunga bao lilioipandisha daraja katika dakika za majeruhi na kuibuka na ushindi wa mabao 2-1 ilipokutana na Sheffield United.
Sunderland haina mashabiki wengi Afrika Mashiriki kama ilivyo kwa Manchester United, Chelsea, Liverpool, Arsenal na kwa kiwango kidogo Newcastle United na Tottenham Hotspurs.
Lakini, ukichunguza utaona kama ipo klabu ya England na Ulaya kwa ujumla iliyo karibu sana na kusaidia kukuza michezo, hasa kandanda katika nchi za Afrika ni Sunderland.
Klabu hiyo ni moja ya timu kongwe za England iliyoundwa 1876 katika mji wenye bandari wa Sunderland wenye wakazi takribani 280,000.
Mji huo ni maarufu kwa ujenzi wa meli, uchimbaji wa makaa ya mawe na kutengeneza vioo. Wakazi wenye asili ya Afrika ni wachache na unatajwa kuwa miongoni mwa maeneo yasiyowabagua Waafrika na Wahindi.
Miongoni mwa wachezaji maarufu wa Afrika walioichezea klabu hiyo ni Ahmed Elmohamady (Misri), Asmoah Gyan, John Mensah na Sulley Muntari (Ghana), Stephane Sessegnon (Benin), Benjani Mwaruwari (Zimbabwe), Patrick Mboma (Cameroon), El Hadji Diof (Senegal) na Reuben Agboola (Nigeria).
Sunderland imepanda daraja pamoja na Leeds United na Burnley kuchukua nafasi za timu tatu zilizoporomoka – Leicester City, Ipswich Town na Southampton.
Kama nilivyoleza hapo juu mashabiki wa nchi mbalimbali za Afrika wana kila sababu ya kufurahia Sunderland kupanda daraja kwa vile imekuwa ikijali kusaidia nchi mbalimbali za bara hili kukuza michezo.
Kwa mfano, hapa Tanzania inashirikiana na Bodi ya Utalii kutangaza vivutio vya utalii kupitia mchezo wa kandanda.
Vilevile imesaidia kujenga kituo cha kisasa cha michezo cha vijana kilichopewa jina la Rais mstaafu Jakaya Kikwete kilichopo Kidongo Chekundu, Dar es Salaam.
Kituo hicho kilichofunguliwa miaka minne iliyopita kinalea wanamichezo tangu wakiwa na umri mdogo.
Kituo hicho kinachotoa mafunzo ya michezo mbalimbali ambacho ujenzi wake uligharimu Dola 2 milioni kilijengwa na Sunderland kwa kushirikiana na kampuni ya Symbion Power ya Marekani na Taasisi ya Grasshoper Soccer ya Australia.
Kituo hicho pia kinatoa mafunzo kwa makocha wa michezo mbali mbali.
Sunderland ina miradi kama hii Zambia, Ghana na Afrika Kusini na baadhi ya vijana waliopata mafunzo katika vituo hivyo sasa wanachezea klabu kubwa na timu za taifa za nchi zao.
Chuo Kikuu cha Sunderland pia kinapokea wanafunzi wengi kutoka nchi za Afrika.
Sunderland imewahi kuwa bingwa wa Ligi ya Daraja ya Kwanza ya England mara sita na mara tano kama mshindi wa pili kuanzia 1892 hadi 1936. Vilevile ilibeba Ngao ya FA 1937 na 1973.
Mtani wa jadi wa klabu hiyo yenye uwanja unachochukua watazamaji 50,000 ni Newcastle United na wengi wanasubiri hali itakuwaje tumu hizo zitakapopambana katika Ligi Kuu England EPL msimu ujao.
Newcastle United ilishika nafasi ya tano katika ligi ya msimu uliopita.
Pambano kati ya timu hizo huwa kali, lakini Newcastle United haitasahau kipigo cha mabao 9-1 ilichokipata Desemba 5, 1908 na mashabiki wake siku zote wamekuwa wakisubiri kulipiza kisasi cha aina hiyo au angalau ushindi unaokaribiana na huo.
Sunderland ni mojawapo wa timu tatu ziliokuwa katika madaraja ya chini kushinda Kombe la FA. Ilifanya hivyo mnamo mwaka 1973 ilipoifunga Leeds United bao 1-0 katika fainali.
Klabu nyingine mbili zilizokuwa zinacheza madaraja ya chini kuwahi kubeba Kombe la FA ni Southampton (1976) na West Ham United (1980).
Mashabiki wa Klabu ya Sunderland wanasifika kwa kupenda nyimbo za mapenzi. Miongoni mwa nyimbo hizo ni ule wa mwanamuziki wa zamani wa Marekani, Elvis Presley usemao ‘Can’t Help Falling in Love’, yaani Siwezi kujizuia kupenda, na mashabiki wake hupenda kuuimba timu yao inapoingia uwanjani.
Kauli mbiu ya timu hiyo ya mgambo ni “Sisi ndio klabu kubwa duniani, upende usipende”.
Klabu hiyo ina matawi ya mashabiki zaidi ya 70 England na zaidi ya 30 katika nchi za Afrika, Uarabuni na Asia.