Tunaanza upyaaa!

Friday January 08 2021
SIMBA UPYAAA PICHA
By Charles Abel

SIMBA ni miongoni mwa timu 16 bora za Afrika. Wamesisitiza kwamba wanaingia kwenye hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa nguvu na hamasa mpya na wataweka heshima.

Ofisa Mtendaji Mkuu wa Simba, Barbara Gonzales ameliambia Mwanaspoti kwamba katika mechi ya juzi dhidi ya Platinum walipambana ndani na nje ya uwanja na kuvuka kwa kishindo, na kwenye makundi wataongeza hamasa zaidi hasa kwa wachezaji.

SIMBA UPYA P

Alisisitiza kwamba hata posho zitakuwa ni za maana kwa wachezaji ili kufanya vizuri zaidi msimu huu na kuthibitisha ubora wa Simba.

Lakini habari njema kwa mashabiki wa Simba ni kwamba kwenye mechi zijazo kiungo wao mpya kutoka Uganda, Taddeo Lwanga maarufu kama Mkata Umeme amerejea uwanjani baada ya kupona homa iliyokuwa ikimsumbua na amesisitiza kwamba wataanza kumuona kuanzia mechi za Kombe la Mapinduzi.

“Nimeshapona na naanza rasmi mazoezi nadhani kuanzia kwenye mechi za Mapinduzi Zanzibar wataanza kuniona,” Taddeo ameliambia Mwanaspoti ambalo ndilo lililofichua na kuandika usajili wake Simba kwa mara ya kwanza.

Advertisement

Droo ya hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika itachezeshwa leo huku Simba ikitega sikio kujua itapangwa na timu gani.

SIMBA UPYAAA PIC

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (Caf), droo hiyo itafanyika leo saa 9.00 alasiri kwa saa za Afrika Mashariki katika makao makuu ya shirikisho hilo, Cairo nchini Misri.

“Washindi wa jumla wa hatua ya kwanza ya mashindano ya Ligi ya Mabingwa Afrika watahusika katika droo ya makundi na washindi wa jumla wa hatua ya kwanza ya Kombe la Shirikisho Afrika watashiriki katika droo ya mwisho ya mchujo,” imesema taarifa hiyo ya Caf.

Kutokana na utaratibu wa uchezeshaji droo hiyo ulioainishwa na Caf, upo uwezekano wa Simba kupangwa katika kundi lenye timu vigogo hasa zile za kutoka Kaskazini mwa Afrika ambazo zimekuwa na uzoefu mkubwa na rekodi ya kufanya vizuri katika mashindano ya klabu Afrika, lakini pia zimekuwa na uwekezaji mkubwa wa fedha ambao umeziwezesha kusajili wachezaji bora na wa daraja la juu ambao wanalipwa kiasi kikubwa cha fedha na kuhudumiwa vizuri.

Kutokana na pointi zake ilizokusanya katika viwango vya timu zilizofanya vizuri kimataifa, katika droo hiyo, Simba imepangwa katika chungu cha tatu ambacho kitakuwa pia na timu za Al Hilal/Asante Kotoko, Pero de Luanda ya Angola pamoja na MC Alger ya Algeria.

Kwa kuwekwa katika chungu cha tatu, inamaanisha kwamba Simba haitaweza kukutana na timu nyingine tatu za chungu hicho, bali itapangwa katika kundi ambalo litajumuisha pia timu kutoka chungu cha kwanza, cha pili na cha nne.

VIGOGO WENYEWE

Vigogo 11 ambavyo Simba inaweza kuangukia katika kundi moja na tatu miongoni mwa hivyo ni Wydad Casablanca (Morocco), Esperance (Tunisia), Al Ahly na Zamalek (Misri), TP Mazembe na AS Vita (DR Congo), Mamelodi Sundowns na Kaizer Chiefs (Afrika Kusini), Horoya (Guinea) pamoja na CR Belouizdad ya Algeria. TP Mazembe, Al Ahly, Wydad na Esperance zenyewe zipo chungu cha kwanza na kila moja itapewa uongozi wa kundi, na zilizopo chungu cha pili ni Mamelodi, AS Vita, Zamalek na Horoya.

Chungu cha nne kitakuwa na timu za Belouizdad, Al Merrikh (Sudan), Kaizer Chiefs na Teungueth (Senegal)

Al Ahly ni mabingwa wa kihistoria wa taji hilo wakiwa wamelitwaa mara tisa, wakati Mazembe na Zamalek kila moja imekuwa bingwa mara tano tofauti wa mashindano hayo.

Timu nyingine na idadi ya mataji ya Ligi ya Mabingwa Afrika zilizochukua ni Esperance mara nne, Wydad Casablanca (2), AS Vita (1) na Mamelodi imechukua mara moja.

Lakini Al Hilal imeshawahi kufika hatua ya fainali wakati Kaizer Chiefs imeshawahi kutinga hatua ya nusu fainali.

Uwekezaji mkubwa wa kifedha ambao timu za Horoya na Belouizdad zimeufana unaweza kuwa jambo lingine la kuitisha Simba lakini pia inaweza kupangwa katika kundi moja na Teungueth na Al Merrikh ambazo ina msuli wa kupambana nazo.

Wakati hali ikiwa hivyo kwa Simba, ndugu zao Namungo nao watakuwa wakisubiri kuona wanapangwa na timu ipi kati ya 16 ambazo zimetolewa katika Ligi ya Mabingwa Afrika na kuangukia katika Kombe la Shirikisho Afrika.

Ikiwa Namungo watapenya kwenye hatua hiyo, watafuzu kuingia hatua ya makundi ya mashindano hayo.

WAPEWA MAMBO MANNE

Wakati wawakilishi hao wa Tanzania kwenye michuano hiyo ya Afrika wakisikilizia kujua watangazwa na timu zipi katika makundi ya Ligi ya Mabingwa kwa Simba na playoff kwa Namungo, wadau wa soka wameipa mambo manne timu hiyo sanjari na Namungo itakayocheza hatua ya mtoano kwenye kombe la Shirikisho (FA) ili kuendelea kufanya vizuri.

Makocha wa wachezaji wa timu hizo wameshauriwa kukaa na wachezaji na kufanya tathimini, nechi la ufundi kuwajenga wachezaji, menejimenti za timu zijue benchi linahitaji nini na kuwa na maandalizi ya moja kwa moja.

“Wasisimame katika maandalizi, Simba tayari imefuzu maana yake lazima icheze makundi, hawahitaji kuzungumza tena mechi ya Platinum, imeshapita, kilichopo ni kuangalia zinazokuja,” alisema Alex Kashasha ‘Mwalimu Kashasha’.

Kashasha alisema kadri timu inavyosonga mbele ndivyo ugumu wa mashindano unaongezeka, hivyo Namungo na Simba wajipange katika hilo.

Alisema pia kocha anapaswa kueleza nini kinapungua ili aongezewe kwenye timu yake.

“Hata kama ni kambi ya nje ya nchi, aseme, japo kiufundi, Simba haina matatizo zaidi ya kutakiwa kuboresha maeneo machache.”

Alisema kocha anapaswa kuangalia kasoro ya mchezaji mmoja mmoja na kumshepu akitolea mfano wa Clatous Chama ambaye alisema ni mzuri zaidi timu yake ikiwa inamiriki mpira lakini si kukaba.

“Hivyo kipindi hiki anatakiwa kumshepu ili abadilike auone mpira ni mtamu wakati wote bila kujali wanamiriki mpira au la, lakini pia Simba inapaswa kuwa na holding midifidi wa uhakika na kwa beki wa kati kocha amtumie zaidi Ame Ibrahim kwa kuwa ni kijana kulinganisha na wengine na ana uwezo.”

Kauli ya Kashasha imeungwa mkono na nyota wa zamani wa timu hiyo, Zamoyoni Mogella ambaye amesema katika hatua ya makundi, Simba wanapaswa kucheza kwa ushindani wakitafuta pointi.

“Pasi nyingi na kutafuta shoo sio kazi yao, wanapaswa kucheza wafunge na kusonga mbele, ila kikubwa benchi la ufundi likae na wachezaji na kufanya tathimini ya mechi zilizopita ili kubaini ubora na udhaifu.

Alisema wachezaji pia wajengwe ili kujitambua na kuona thamani yao kwamba wana jukumu kubwa mbele yao na uongozi ujue benchi la ufundi linahitaji jiji, kikubwa ni kujipanga tu,” alisema Mogella.

Watakapangwa na Simba

Al Ahly (Misri)

Wydad Casablanca (Morocco)

Espérance de Tunis (Tunisia)

TP Mazembe (DR Congo)

Zamalek (Misri)

Mamelodi Sundowns (Afrika Kusini)

AC Horoya (Guinea)

AS Vita Club (DR Congo)

Al Merreikh (Sudan)

CR Belouizdad (Algeria)

Teungueth (Senegal)

Kaizer Chiefs (Afrika Kusini)

Mziki wa Namungo

Raja Casablanca (Morocco)

1º de Agosto (Angola)

Enyimba (Nigeria)

CS Sfaxien (Tunisia)

Gor Mahia (Kenya)

FC Platinum (Zimbabwe)

Nkana (Zambia)

Asante Kotoko (Ghana)

Jwaneng Galaxy (Botswana)

Gazelle (Chad)

Young Buffaloes (Eswatini)

AS Bouenguidi (Gabon)

RC Abidjan (Ivory Coast)

Al Ahly Benghazi (Libya)

Stade Malien (Mali)

AS SONIDEP (Niger)

Februari 12 hadi 14 ni tarehe za mechi za awali za makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika na playoff (mchujo) ya Kombe la Shirikisho, ambapo Simba na Namungo FC zitaendelea kupeperusha bendera ya Tanzania.  

Advertisement