Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

TAOUSSI: Fei Toto anastahili kucheza kule!

Muktasari:

  • Kocha huyo aliyeajiriwa hivi karibuni kutoka Morocco ili kuchukua nafasi ya Youssouf Dabo, amefichua hayo wakati wa mahojiano maalumu na Mwanaspoti akisema anamshangaa sana nyota huyo wa kimataifa wa Tanzania kuendelea kusalia Azam kwa kiwango alichonacho.

WAKATI kukiwa na mjadala kuhusu hatima ya kiungo mshambuliaji wa Azam FC, Feisal Salum 'Fei Toto', kutokana kiwango alichonacho na timu anayoichezea kwa sasa, kumbe hata kocha wa timu hiyo, Rachid Taoussi amegundua na kusema ukweli.

Kocha huyo aliyeajiriwa hivi karibuni kutoka Morocco ili kuchukua nafasi ya Youssouf Dabo, amefichua hayo wakati wa mahojiano maalumu na Mwanaspoti akisema anamshangaa sana nyota huyo wa kimataifa wa Tanzania kuendelea kusalia Azam kwa kiwango alichonacho.

Pia amefunguka mambo kadhaa tangu ajiunge na timu hiyo na namna alivyojipanga kwa ajili ya michuano ya Ligi Kuu Bara na Kombe la Shirikisho na anavyoiona Azam ikifika wapi ikiwa chini yake. Endelea naye...


MIEZI MIWILI TU

Taoussi ameomba muda wa miezi miwili ili kuifanya Azam iwe moja ya timu tishio nchini na kurejea katika michuano ya CAF ikiwa kivingine baada ya kutolewa raundi ya kwanza msimu huu katika Ligi ya Mabingwa Afrika iliyoshiriki kwa mara ya pili baada ya awali kuishiriki mwaka 2015.

Azam ilipata nafasi ya kucheza Ligi hiyo kwa mara ya kwanza baada ya kubeba ubingwa wa Ligi Kuu Bara msimu wa 2013-14 na msimu huu ilipata kwa kumaliza katika nafasi ya pili kwenye msimamo wa Ligi Kuu ya msimu uliopita, lakini ikaishia kung'olewa kwa jumla ya mabao 2-1 na APR ya Rwanda.

Azam iling'oka ikiwa chini ya Dabo, ambaye alijikuta akitemeshwa kibarua chake na kuletwa Taoussi ambaye amekiri Azam ina wachezaji bora na akipata muda huo wa miezi miwili ili kulisha mbinu kwa mastaa wa timu hiyo, Azam itarudi katika makali iliyozoeleka miaka michache iliyopita ilipovisumbua vigogo nchini.

"Nimefika nchini nikiwa na siku chache na timu ilicheza mechi ya ligi na kunipa mwanga wa wapi pa kuanzia na ndani ya muda tumeanza kuona mwanga, licha ya kupoteza 2-0 mbele ya Simba," anasema Taoussi ambaye hakufurahishwa na uamuzi katika mechi ya Simba akidai mabao yote mawili ya Wekundu wa Msimbazi yalikuwa ni ya kuotea na akataka VAR ianze haraka nchini.

"Ninahitaji muda zaidi kwa lengo la kujenga timu ya ushindani nafikiri kutokana na mfululizo wa mechi za ligi miezi miwili inanitosha kujenga timu ya ushindani na bora ukanda wa Afrika."

Anasema ana wachezaji ambao wanajituma na kucheza soka la kasi ambalo ndilo linalotumika na timu nyingi za Afrika hivyo anaamini akiwajenga wachezaji wake kuwa timamu na washindani atakuwa na kikosi kizuri.

LIGI YA MABINGWA

Ni ndoto ya kila kocha kufikia malengo kwenye klabu anayopata nafasi ya kufundisha lakini sio wote wanaweza kufanya hivyo kutokana na kutimuliwa mapema kabla ya muda wa makubaliano ya kimkataba, lakini Taoussi licha ya ugeni wake kwenye ligi ya Tanzania ametamba kuirudisha timu hiyo katika Ligi ya Mabingwa Afrika msimu ujao.

"Sio rahisi, tunahitaji kuwekeza nguvu zaidi ili kuweza kufikia malengo, kama msimu uliopita tuliweza kumaliza katika nafasi ya pili nyuma ya Yanga ambayo ndio ilitwaa taji la Ligi Kuu Bara, msimu ujao tunaweza kufikia lengo la kutwaa ubingwa na kuiwakilisha nchi kwenye michuano hiyo mikubwa," anasema na kuongeza;

"Hakuna kinachoshindikana kama tutajenga umoja mzuri na kutumia miundombinu mizuri iliyopo kwa kujenga kikosi shindani ambacho kitatoa matokeo chanya kwa timu pinzani naamini hili litawezekana msimu huu."

Taoussi anasema mwanzo mbaya kwenye mechi za mwanzo hauwezi kuwatoa mchezoni kwani ligi ina mechi 30 hivyo wakiwekeza nguvu na umoja wanaweza kufikia malengo na hatimaye kuipeleka timu hiyo kimataifa kwa mara ya pili mfululizo kwenda kujenga uzoefu.

KIKOSI BORA

Licha ya kutokuwa na muda mrefu tangu amejiunga na kikosi cha Azam FC, Taoussi amefurahishwa na aina ya wachezaji wa timu hiyo ambao ameweka wazi kuwa watamsaidia kufikia malengo yake ya kujenga CV nzuri kwenye soka la Afrika.

"Sina muda mrefu niliokaa na wachezaji, lakini kuna mambo mengi mazuri wamenionyesha, kwanza wanacheza mpira wa kasi ambao ndio umekuwa ukichezwa na timu nyingi na wamenionyesha ni namna gani kila mmoja anatamani kuingia katika kikosi cha kwanza," anasema kocha huyo na kuongeza;

"Azam imekamilika kila idara, najivunia kufanya kazi na timu hii, kuna mambo mengi mazuri yanakuja kwani hapa kuna vijana wengi ambao pia wana uchu wa mafanikio, naamini uwepo pia wa academy ya timu ya vijana ambao pia wana vipaji itasaidia kuwa na mwendelezo wa kuibua na kukuza vipaji."


KILA MCHEZAJI AFUNGE

Achana na Azam kushindwa kupata bao kwenye mechi mbili za mwanzo na Alhamisi kukwama mbele ya Simba, Taouassi anasema hilo wala halimpi shida ambapo amekiri  pamoja na kukosa nafasi ya kukwamisha mpira nyavuni bado ana imani na timu yake hasa eneo la ushambuliaji kwani wanatengeneza nafasi.

"Suala sio kufunga, mpango unaanza kwenye kutengeneza nafasi na baadaye kumalizia kwa kukwamisha mipira nyavuni, hilo nina muda nitalifanyia kazi haraka iwezekanavyo ili kujihakikishia wastani mzuri wa kupachika mabao kwenye kila mchezo," anasema Taoussi na kuongeza;

"Nataka timu ambayo haitakuwa inamtegemea mtu mmoja kwenye kufunga kila mmoja akipata nafasi anatakiwa kutumia nafasi ili kuepusha presha kwa washambuliaji waliopo hakuna mchezaji ambaye anafundishwa kufunga."


BLANCO APEWE MUDA

Licha ya Jhonier Blanco kutajwa kuwa mshambuliaji tisho baada ya kusajiliwa na Azam kocha huyo amemkingia kifua na kuwaomba mashabiki na wadau wa mpira kumpa muda mchezaji huyo ili aweze kuzoea mazingira na kuingia kweye mfumo.

"Ni kweli timu ina wachezaji wengi wazuri na wenye uwezo mkubwa lakini ni mapema sana kuwatwisha mzigo wa kuhakikisha wanafanya vizuri kwani bado ni mapema kutokana na upya wao kwenye kikosi kwani wanatakiwa kuzoea mazingira na kuingia kwenye mfumo," anasema Taoussi.

"Mfano mzuri ni Blanco ni mchezaji ambaye amesajiliwa katika dirisha kubwa la usajili na amekuja ukanda ambao ni tofauti na nchi aliyotoka hivyo anahitaji muda zaidi ili aweze kutupa kile tunachotarajia kutoka kwake," anaongeza.

Pamoja na kocha huyo kuomba mchezaji huyo apewe muda tayari ameifungia Azam bao moja kwa penalti katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika ilipokuwa ikitolewa na APR kwa jumla ya mabao 2-1, Azam ikishinda nyumbani 1-0 na kulala ugenini 2-0.

KUHUSU FEI TOTO

Taoussi anakiri kama kuna mchezaji anayemshangaza kwa kipaji kikubwa cha soka basi ni Feisal Salum 'Fei Toto', ambapo anasema kwa kiwango chake hakustahili kuendelea kucheza Tanzania.

"Sijamuona akicheza kwenye mechi nyingi, lakini bahati niliyoipata kushuhudia akifanya kazi nzuri katika timu ya taifa, Taifa Stars, nimefurahi kuwa na mchezaji wa aina yake na atakuwa ni sehemu ya wachezaji watakaonipa matokeo," anasema Taoussi na kuongeza;

"Ni mchezaji ambaye anaweza kufunga, kutengeneza nafasi na hata kukaba, aina ya wachezaji kama yeye ndio natamani kuwa nao wengi zaidi kwani ili uweze kutwaa mataji, unatakiwa kufunga mabao mengi yatakayozalisha pointi na kama hatafunga nina uhakika atatengeneza nafasi.

"Kwa kiwango alichonacho anastahili kucheza zaidi na hapa Tanzania, kokote anacheza hata kule Ulaya. Bahati nzuri hata umri wake unamruhusu. Ila nafurahia kuwa naye hapa," anafafanua Taoussi.


NIDHAMU KWANZA

Mafanikio ndani ya timu yanazingatia vitu vingi sana kuanzia ubora wa kikosi, nidhamu nzuri nje na ndani ya uwanja lakini pia uwekezaji wa timu kuanzia benchi la ufundi, wachezaji na uongozi kwa ujumla kama ambavyo anakiri Taoussi.

"Mafanikio ni sehemu ya mipango na kila kitu kinawezekana lakini kubwa zaidi la kuzingatiwa ni nidhamu kwa wachezaji, benchi la ufundi na viongozi kwa ujumla ili kuwa na muunganiko mzuri ndani ya uwanja hadi nje," anasema na kuongeza;

"Nidhamu ndio kipaumbele muhimu kwangu nje ya uwanja hadi ndani kama kuna wachezaji watashindwa kufuata matakwa yangu kwenye eneo hili hatuwezi kwenda sawa kwani hatutafikia malengo."

Anasema mipango ikiwa ni kukutana muda fulani kila mmoja anatakiwa kuwa eneo la tukio kwani jambo hilo ndio litachangia kwa kiasi kikubwa wao kufikia malengo.

ATAJA MBINU ZA DABI

Azam imemaliza dabi ya Mzizima na sasa ina mtihani wa Dabi ya Dar na kocha huyo anasema ni mzoefu wa mechi kama hizo, japo alipoteza mbele ya Simba akitoa lawama zaidi kwa waamuzi waliolichezesha pale visisiwani Zanzibar na Azam kulala 2-0.

Msimu huu tayari Azam imeshacheza na Yanga katika fainali ya Ngao ya Jamii na kuchakazwa 4-1, lakini katika ligi inatarajia mambo yatakuwa tofauti.

"Kila nchi ina mechi za aina hizo na nimekutana nazo sana nikiwa mwalimu sijawahi kuhofia wala sina wasiwasi kwa sababu ni mechi ambazo hazitakiwi kuumiza kichwa sana kwa kumfundisha mchezaji mbinu zaidi ni kumuandaa tu," anasema na kuongeza;

"Dabi sio mchezo wa kutumia mbinu sana zaidi ni kuwajenga wachezaji kisaikolojia na kuwapa mambo muhimu ya kuzingatia kabla ya mchezo hivyo sina wasiwasi sana kuhusiana na hilo."