Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Tanzania inavyojipanga 2027

TANZANIA imeingia kwenye historia barani Afrika ikiungana na Kenya na Uganda kuandaa kwa pamoja fainali za Kombe ya Mataifa ya Afrika (Afcon) 2027, huku mipango ikiwa imeshaanza kuwekwa sawa mbali na michuano hiyo kuonekana ni fursa nzuri kwa nchi hizo katika maeneo ya Afrika Mashariki.

Baadhi ya wadau wa michezo wamezungumzia:

“Kama tutautizama kwa jicho la zaidi ya mpira, ni dhahiri uenyeji huu unakwenda kufungua fursa nyingi katika uchumi wetu kwenye sekta mbalimbali, kinyume na hapo unaweza kutuacha kwenye umasikini,” huu ni mtazamo wa Mchumi, Profesa Abel Kinyondo akiutazama uenyeji huo kwenye fursa nyingi.

Kinyondo anaungana na wadau wengine katika kuuangalia uenyeji wa Tanzania katika mlengo wa kiuchumi, biashara, utalii na fursa nyingine zaidi ya michezo.

Juzi Shirikisho la Soka Afrika (Caf) lilizipa uenyeji nchi za Kenya, Uganda na Tanzania wa fainali za Mataifa Afrika (Afcon) mwaka 2027.

Rais wa Caf, Dk. Patrice Motsepe alitangaza maombi ya pamoja ya nchi hizo za Jumuiya ya Afrika Mashariki yaliyopewa jina la Pamoja Bid yameshinda mchakato wa kuandaa Afcon 2027, yakipiku maombi ya nchi za Algeria, Senegal, Misri na Botswana.

Kwa upande wa Tanzania, serikali imelithibitishia Mwanaspoti kuwa zitachezwa katika Miji ya Arusha, Dar es Salaam na Zanzibar.

“Viwanja vya mashindano ni vinane kwa nchi hizi tatu, Tanzania tulichagua ule wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam, Uwanja wa Amaan, Zanzibar na uwanja mpya ambao utajengwa Arusha,” anasema Mkurugenzi wa Maendeleo ya Michezo, Ally Mayay.

Ujenzi wa uwanja wa Arusha unatarajiwa kuanza kabla ya kuanza mwaka 2024.

“Ni uwanja wa kisasa ambao ni nje ya mji, unajengwa Kata ya Olmoti na utakuwa na uwezo wa kubeba mashabiki 30,000 waliokaa.

“Afcon imeleta neema nyingine, mainjinia wako kazini, ila michoro yake haiko tayari, utajengwa katika kipindi cha miezi 18 hadi kukamilika,” anasema.

Mchumi, Profesa Abel Kinyondo anasema kupata uenyeji ni ni kitu kimoja na kuutumia kwa manufaa ni kitu kingine.

“Kuna nchi zimewahi kuingia kwenye umasikini kwa kuwa na mzigo mkubwa wa kuandaa mashindano ya dunia na kujikita kujenga miundo mbinu.

“Tunapaswa kupanua wigo, uenyeji ni fursa ya kwanza na kuutumia kwa zaidi ya mpira ni kitu kingine,” anasema.


AJIRA KIBAO

Mayay anasema kuna ajira nyingi zisizo rasmi zitazalishwa kipindi kirefu hadi kwenye fainali hizo.

“Kuanzia kwenye ujenzi na ukarabati wa viwanja hadi wakati wa mashindano yenyewe kuna ajira nyingi sana zitazalishwa, hapo,” anasema Mayay.

Anasema pia wakati wa mashindano, misafara ya timu itatumia fedha za kigeni hapa nchini, hivyo hiyo itakuwa ni fursa nyingine nje ya mpira.

“Ajira zisizo rasmi ni nyingi kweli kweli, wageni wanaokuja hapa watahitaji watoaji wa huduma zote, watu wa skauti, vijana wa kuwaongoza na ajira nyingine nyingi zisizo rasmi kwa vijana, hivyo itasaidia kukuza uchumi wa mtu mmoja mmoja.

“Pia, timu zinapokuja kwenye mashindano makubwa kama haya zinalala kwenye hoteli ambazo mtu atalipa Dola 200 hadi 300 kwa siku, hivyo itatuongezea fedha za kigeni,” anasema Mayay.

Hata hivyo, Profesa Kinyondo anasema, kama nchi ikiyatumia mashindano hayo kama kichocheo cha kukuza uchumi, yatakuwa na manufaa makubwa kwa taifa na mtu mmoja mmoja.

“Isiwe kujenga viwanja tu tusema tunaongeza idadi ya hoteli za nyota tano, migahawa na kutengeneza netiweki ya usafirishaji, ili mgeni atakayekuja kwenye Afcon kama siku hiyo timu yake haichezi, aweze kukimbia Serengeti, Ngorongoro, Mikumi na kwenye vivutio vyetu vya utalii.”


UTALII

Katika sekta ya utalii, ambayo mbali na michezo, inatajwa kwa jicho la kufungua fursa zaidi na kuongeza watalii wapya katika sekta hiyo.

Batiho Herman, Naibu Kamishna wa Uhifadhi TANAPA, anasema uenyeji wa Afcon ni fursa mtambuka katika sekta mbalimbali ikiwamo ya utalii.

“Tumesikia taarifa hizi jana (juzi) itabidi tukae sasa tuyawekee mikakati mashindano haya, haitaishia michezo watakaokuja watembelee mbuga, tutakaa kuweka mikakati ya hili.

“Hii ni fursa kubwa, kama nilivyosema, tutakaa na kupanga na wenzetu Afcon sio mpira tu, kwenye utalii tutajipanga kwenye mambo mengi, ikiwamo kuvutua wawekezaji kwenye maeneo yetu,” anasema.

Kwenye Utalii, Profesa Kinyondo anasema wageni watakaokuja nchini hawapaswi kuchukuliwa kama mashabiki, wale ni wateja na watalii.

“Tukiwachukulia kama mashabiki ni kupata hasara, hili tukio litoke kwenye michezo, liunganishwe kwenye utalii, liunganishwe kwenye viwanda, biashara, kilimo na fursa nyingine.

“Tukiyaunganisha kwenye hayo kuna uwezekano wa kupata faida kubwa na kuongeza uchumi na kutengeneza aina mpya ya watalii.

“Hawa mashabiki, wachezaji na wote watakaokuja nchini kwa ajili ya Afcon ni dhahiri hawatakuja nchini kwa ajili ya kutalii, lakini tutakapowapa huduma bora, watarudi tena.

“Ili ni eneo la zaidi ya michezo, Wizara za Utaliu, Viwanda na nyinginezo zione namna ya kutumia uenyeji huu kuwa fursa, pia kuna uhamiaji kwenye kutoa visa, polisi wahakikishe hao watu hawasumbuliwi, tukiwahudumia vizuri ni dhahiri watarudi tena baada ya mpira na watatufanyia matangazo ya vivutio vyetu na nchi yetu bila gharama.

“Kinyume na hapo, tukichukulia ni mpira tu itatugharimu kwani zipo nchi zimeingia kwenye umasikini  baada ya kupewa uenyeji na kuishia kwenye mpira tu bila kwenda mbali zaidi ya mpira.”


USAFIRISHAJI

Mkurugenzi Latra, Habibu Saluo alisema: “Siku zote sisi tunaendana na uhitaji. Na sasa angalau miundombinu ni mizuri lakini magari bado hayako vizuri sana kwenye kutoa huduma.”

Salu anasema viwanja vilivyotangazwa kutumika ni vitatu ikiwemo cha Dodoma ambako tayari reli ya kisasa ya SGR imefika hivyo anaamini mpaka itakapofika wakati huo reli hiyo itakuwa inafanya kazi na kurahisisha suala la usafiri kwa wenyeji na wageni kwa ujumla.

“Tulimepokea kwa furaha na tunaamini ni fursa ya uwekezaji kwa wenzetu wanaotoa huduma za usafiri na tukapata mabasi mazuri zaidi na kuboresha miundombinu kama barabara,” anaisema.

Aliongeza sio tu kwenye mashindano ya Afcon lakini pia kwenye utalii ambapo tayari uko mpango kujenga njia za magari ya kupita kwenye waya kwenda Mlima Kilimanjaro akiamini usafiri huo unaweza pia kujengwa maeneo mengine ili kurahisisha usafiri wakati wa mashindano hayo.

“Tunaamini mpaka wakati huo tutakuwa tayari tumefanikiwa. Tutaangalia maeneo ya uwekezaji kama vile utalii kwani tunafahamu mashindano hayo ni fursa pia kwa utalii wetu,” alifafanua.

Pia, alisema iko haja kwa wawekezaji hususanai katika usafiri kuungana ili kuhakikisha wanatoa huduma bora zaidi.


MAWASILIANO

Naibu Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhandisi Kundo Mathew anasema mashindano hayo ni fursa katika sekta hiyo, pia ni changamoto kwao katika kuhakikisha wanafanyakazi kwa kasi ili kuhakikisha suala la uimara katika mawasiliano linakamilika kabla ya mashindano hayo.

Anasema tayari wizara hiyo inafanyia kazi maagizo ya Rais ya kuhakikisha baadhi ya maeneo yanakuwa na mtandao wa kasi yakiwemo maeneo ya wazi kama vile kwenye mabasi na vituo vya viwanja vya ndege na vya michezo.

“Tunaamini mabasi yetu ya mwendokasi yatatumika sana, tunataka kuondoa changamoto ya mtandao ili iwe rahisi watu kuhabarishana na kuwasiliana,” anasema Mathew.

Anasema wizara imejiwekea malengo ya kuhakikisha huduma ya mkongo wa taifa inafika katika wilaya zote 139 hadi kufikia mwaka 2025 ambapo huduma nyingi za kijamii zitaweza kutumia mtandao kwa urahisi kama vile kwenye shule, hospital, hoteli na vituo vya polisi.

“Tunaamini hadi kufikia kipindi hicho, wananchi watakua wakilipia huduma ya mtandao badala ya kulipia vifurushi kama ilivyo sasa jambo ambalo litakuwa ni rahisi zaidi,” anasema Mathew na kuongeza;

“Sisi kama serikali tunahitaji kuwa na sera safi, sheria safi na miundombinu ambayo itawasaidia watoa huduma kufikisha huduma zao vizuri, lakini na wawekezaji wawekeze vizuri ili huduma zao ziendane na teknolijia iliyopo.”

Ili kuhakikisha kasi ya mtandao inakuwepo Mathew anasema wako katika mkakati wa kuhakikisha majiji makubwa yanakuwa na teknolojia ya 5G huku Dar es Salaam, Dodoma, Arusha, Mwanza na Mbeya yakipewa kipaumbele.


HOTELI

Mkurugenzi Mkuu wa Chama cha Wamiliki wa Hoteli Tanzania (HAT), Kenedy Edward mashindano hayo ni fursa ya kukuza uchumi kwa si kwa upunde wao peke yao bali katika sekta nyingine pia.

“Kwa upande wa hoteli tuko tayari kwa asilimia kubwa kuwapokea na kuwatunza wageni. Nina imani tunao uwezo huo ukizingatia ziko hoteli za kutosha zikiwemo za nyota tano. Mgeni ataamua ni hoteli gani anataka kulingana na kipato chake,” anasema Edward.

Anasema ipo haja ya wamiliki wa mahoteli kujitathmini katika maeneo ya uboreshaji wa mapungufu madogo ili kuondoa changamoto zozote ambazo huenda wageni wakakutana nazo.


MARAIS WATATU

Yote hayo yasingewezekans, bila wakuu wa nchi hizi tatu, za Jumuiya ya Afrika Mashariki, Rais Samia Suluhu Hassan (Tanzania), Yoweri Museveni (Uganda) na William Ruto (Kenya).

“Bila garantii ya viongozi kuonyesha serikali zetu zipo tayari tusingeweza kupata fursa hii, shukrani kubwa ni kwao, nakumbuka wakati mchakato umeanza, wakaguzi wa Caf walikuja Dar es Salaam, wakaenda Kampala (Uganda) na Nairobi (Kenya) walithibitisha kweli tuna utayari,” anasema Mayay.

Anasema, walikuta mikataba ya ujenzi wa viwanja vipya na ukarabati kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Amaan, Moi Kasarani na ule wa Kampala unaendelea.

“Hii imetusaidia pia kupata fursa, ushindani ulikuwa mkali  wa kugombea uenyeji wa kuandaa mashindano hayo,” anasema.

Mbali na viwanja vitatu kutumika nchini kwenye mechi za mashindano hayo, lakini vile vya mazoezi pia vitakuwa ni fursa nyingine za kuingiza kipato kwa wamiliki wake.

Miongoni mwa viwanja vinavyokidhi kutumiwa kwa mazoezi kwa hapa Dar es Salaam ni Gymkhana, Hopac, IST na wa Azam Complex.

Mayay anasema kuna uwezekano mkubwa ufunguzi wa mashindano hayo ukafanyika jijini Dar es Salaam.

“Japo Uganda watacheza nyumbani mechi zao za awali, Kenya vivyo hivyo na Tanzania pia kila timu itacheza mechi hizo za awali nyumbani kwake, lakini ufunguzi inawezekana ikawa hapa Dar es Salaam.

“Hata hivyo kitendo cha kupewa uzinduzi wa African football League inaweza kuwa kigezo cha Caf kutupa ufunguzi hapa japo kwenye zile za robo, nusu na fainali ratiba bado, kuna kamati ya Caf inaandaa ratiba hiyo,” anasema Mayay.

Hii ni mara ya kwanza kwa fainali za Afcon kuandaliwa kwa pamoja na nchi za Kenya, Uganda na Tanzania ambayo mwaka 2019 ilikuwa mwenyeji wa mashindano hayo kwa vijana chini ya umri wa miaka 17 (Afcon U17).

Mwaka 1996, Kenya ilikuwa iandae fainali hizi lakini ilishindikana na hatimaye zikahamia Afrika Kusini.