Taifa Stars ijipange Kombe la Dunia 2026

FAINALI za Kombe la Dunia ni za 22, zinaendelea nchini Qatar zikishirikisha mataifa 32, huku Watanzania kwa mara nyingine wakiwa watazamaji.

Hizi zinakuwa fainali za kwanza kufanyika katika nchi ya Kiarabu, zinatarajiwa kufikia tamati Desemba 18.

Tanzania ilikuwa ni moja kati ya nchi zilizosaka tiketi tano za Bara la Afrika, lakini ilikwama katika kundi lake na kuziacha Senegal, Cameroon, Ghana, Morocco na Tunisia zikitinga Qatar kuwakilisha bara.

Tanzania imekwama kwa sababu mbalimbali na hapa chini ni baadhi na mikakati ya kujipanga kwa fainali zijazo za 2026 zitakazoshirikisha nchi 48...


UWANJA WA NYUMBANI

Katika mechi tano ambazo Timu ya Taifa ya Tanzania “Taifa Stars” ilicheza, tatu ilicheza nyumbani na kukusanya pointi tatu pekee kwa kuifunga Madagascar 3-2.

Mechi mbili imepoteza nyumbani dhidi ya Benin (0-1) na DR Congo (0-3).

Ukiangalia katika mechi hizo tatu, timu haikuwa vizuri kwenye kulinda lango lake kwani iliruhusu mabao sita, huku ikifunga matatu.

Ugenini, Taifa Stars ilicheza mechi tatu, imekusanya pointi nne, imeshinda (0-1) dhidi ya Benin na sare ya 1-1 dhidi ya DR Congo na kufungwa na Madagasca 2-0.

Kwa takwimu hizo, inaonekana Taifa Stars ugenini ilikuwa vizuri kuliko nyumbani, lakini shida kubwa iko kwenye ufungaji wa mabao. Ili kufanya vizuri, inatakiwa kujenga utamaduni wa kushinda michezo yake ya nyumbani.

Siku zote timu inayotumia vizuri uwanja wake wa nyumbani ndiyo inayokuwa na nafasi kubwa ya kufanya vizuri. Inaaminika, timu nyingi zinapokwenda kucheza ugenii huwa zinakutana na vikwazo vingi na kuwa na nafasi ndogo ya kupata ushindi. Lakini inapocheza nyumbani inayajua mazingira ikiwemo na kubebwa na haliya hewa, ikipoteza inaonekana kutokuwa makini.

Hiki ndicho kilichoifanya Taifa Stars kushindwa kusonga mbele katika vita ya kufuzu fainali za Kombe la Dunia la Qatar. Ukiiangalia Congo DR iliyokuwa vinara katika Kundi J, mechi zake tano ilizocheza, imeshinda tatu, sare mbili na kupoteza mmoja.

Kwa maana hiyo tukijipanga tunaweza kushinda mechi zetu tatu na kuingia kwenye hatua ya mwisho ya kufuzu Kombe la Dunia.


SHIDA YA WASHAMBULIAJI

Kingine kilichoifanya Stars kushindwa kusonga mbele ni kukosa washambuliaji wa kuipambania timu kufikia mafanikio hii ni kutokana na mwendelezo wa viwango vya kawaida vya wachezaji wanaocheza eneo hilo.

Tumezoea kumuona nahodha Mbwana Samatta akitumika zaidi eneo hilo na tayari ameonekana kutofanya vizuri hadi kwenye timu yake kutokana na kutumika sana lakini bado taifa liliendelea kumwamini na kumpa nafasi.

Stars inatakiwa kuanza kufanya marekebisho makubwa kwenye eneo hilo.


STARS YA MAZOEA

Pamoja na vipaji vingi kuibuka kila msimu lakini Stars imeendelea kuwa ileile ya siku zote. Ilijaa wachezaji wakongwe kwenye kila mashindano hadi kwenye mechi za kirafiki.

Hakuna mabadiliko kwa wachezaji hata wakiwa na viwango vibovu kwenye timu zao bado wataonekana kwenye timu ya taifa.


AINA ZA MAKOCHA

Stars ni miongoni mwa timu za taifa zilizofundishwa na makocha wengi zaidi.

Hii ni kutokana na timuatimua baada ya kupata matokeo mabaya.

Pamoja na kufundishwa na makocha wengi lakini kwa bahati mbaya makocha hao hawakuwa na rekodi nzuri kwenye mashindano pia wengine wamekuwa bora kwa timu za vijana zaidi.

Mfano ni Mdenishi, Kim Poulsen aliyeondolewa hivi karibuni kutokana na matokeo mabaya ikiwemo kushindwa kuipeleka timu Kombe la Dunia.

Kuna tofauti kubwa kati ya rekodi za makocha wa timu pinzani na Stars.


KIKOSI KIPYA

Ili Stars iweze kufuzu Kombe la Dunia 2026, inatakiwa kutorudia makosa kwa kuandaa kikosi mapema ikizingatiwa kuandaa mashindano ya vijana kwa wingi.

Isitegmee sana wachezaji wakongwe, iwajenge vijana kuanzia sasa kwenye mashindano mbalimbali ndio wanaopaswa kuandaliwa mapema. Stars iwe na sura mpya kwa vijana walioshiriki fainali za Afcon U17 za 2017 na 2019 vipaji vyao viendelezwe kwa kujengwa kwa ushindani na kocha atakayepewa timu awekewe malengo ya nchi inatakiwa kufuzu fainali za Afcon na Kombe la Dunia.