Tahadhari… CBE waje kwa kutulia

Muktasari:
- Pia ondoa akilini kuhusu asilimia kubwa walizonazo Yanga katika kutinga hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huu kutokana na rekodi zao nzuri zilivyo dhidi ya Wahabeshi wanapocheza nyumbani.
ACHANA na ushindi wa bao 1-0 ilioupata Yanga nchini Ethiopia na kuweka rekodi mpya ndani ya klabu hiyo katika michuano inayosimamiwa na Shirikisho la Soka Afrika (CAF), na sasa Wananchi wanaendelea kutamba.
Pia ondoa akilini kuhusu asilimia kubwa walizonazo Yanga katika kutinga hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huu kutokana na rekodi zao nzuri zilivyo dhidi ya Wahabeshi wanapocheza nyumbani.
Kuna kitu ambacho kinawapa jeuri kubwa Wananchi juu ya timu yao kwa namna ambavyo wameiona hadi sasa ilichofanya tangu kuanza msimu huu wa mashindano 2024-2025.
Mabingwa hao watetezi wa Ligi Kuu Bara, wamekuwa na mwanzo mzuri msimu huu katika michuano mitatu tofauti waliyoshiriki hadi sasa ambayo ni Ngao ya Jamii, Ligi ya Mabingwa Afrika na Ligi Kuu Bara. Katika michuano yote hiyo, Yanga imepata ushindi kwa asilimia 100 kutokana na kushinda mechi zote sita ilizocheza.
Yanga chini ya Kocha Miguel Gamondi ambaye huu ni msimu wake wa pili akiinoa timu hiyo, tayari kabatini ina Ngao ya Jamii iliyobeba kwa kuichapa Azam 4-1 katika mchezo wa fainali uliochezwa Agosti 11 mwaka huu.
Kabla ya hapo iliwachapa watani wao wa jadi, Simba bao 1-0 hatua ya nusu fainali. Kiburi walichonacho Wananchi ambao ni wana fainali wa Kombe la Shirikisho Afrika msimu wa 2022/2023, ni namna walivyo na safu bora zaidi ya ushambuliaji sambamba na eneo la ulinzi lisilopitika kirahisi.
Takwimu katika mechi sita walizocheza zikiwamo mbili Ngao ya Jamii, Ligi ya Mabingwa Afrika (3) na Ligi Kuu Bara moja, Yanga imefunga jumla ya mabao 18, huku ikiruhusu nyavu zao kutikiswa mara moja.

Aliyefanikiwa kutikisa nyavu za Yanga mpaka sasa ni mchezaji wa zamani wa timu hiyo, Feisal Salum ‘Fei Toto’ ambaye aliitumikia timu hiyo kwa takribani misimu minne kabla ya 2023-2024 kutimkia Azam FC.
DAKIKA ZA HATARI
Kwa namna Yanga inavyocheza msimu huu ni wazi wapinzani wanapaswa kujitafakari zaidi kila wanapokwenda kucheza nao kwani wamekuwa hatari vipindi vyote vya mchezo wakitikisa nyavu za wapinzani kasoro mechi mbili pekee ambazo hawakufunga bao kipindi cha pili. Hiyo ilikuwa dhidi ya Simba na CBE.
Takwimu zinaonyesha kwamba, Yanga katika mechi zote sita, walikwenda mapumziko wakiwa wanaongoza na tano kati ya hizo matokeo yalikuwa 1-0, dhidi ya Simba, Vital’O mara mbili, Kagera Sugar na CBE, moja pekee dhidi ya Azam ilikuwa 3-1. Mbali na hilo, katika dakika tisini ambazo ukizigawa kwa makundi sita kwa maana ya dakika 1 hadi 15, 16 hadi 30, 31 hadi 45, 46 hadi 60, 61 hadi 75 na 76 hadi 90, Yanga imeonekana kuwa hatari zaidi katika kundi la mwisho ambalo ni kuanzia dakika ya 75 hadi 90.
Katika muda huo, Yanga imefunga mabao mengi zaidi ambayo ni matano, huku ikifuatiwa na kipindi cha kati ya dakika 16 hadi 30 ikifunga mabao manne. Muda ambao unaonekana kujirudia kupatikana mabao ni kati ya dakika ya 1 hadi 15, 31 hadi 45 na 46 hadi 60 ambapo kote hapo imefunga mawilimawili, huku kipindi cha kati ya dakika 61 na 75 yakifungwa mabao matatu.

AINA YA MABAO
Yanga imefunga mabao manne kwa mguu wa kushoto, moja likifungwa na Clatous Chama ambaye alifanya hivyo katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Vital’O iliposhinda 4-0.
Pia Aziz Ki ambaye huo ndiyo mguu wake anaoutumia zaidi, alifunga mabao matatu dhidi ya Azam katika Ngao ya Jamii na mengine mawili Ligi ya Mabingwa dhidi ya Vital’O. Ukiachana na mabao ya mguu wa kushoto, Yanga haijafunga bao la kichwa, lakini mengi zaidi yakionekana kufungwa kwa mguu wa kulia ambayo ni 14 likiwemo lile moja Azam walilojifunga. Pia kupitia mipira ya kutengwa, Yanga imefunga mabao matatu, mawili kwa njia ya penalti kutoka kwa Aziz Ki na Pacome Zouzoua ilipocheza dhidi ya Vital’O mechi ya kwanza na ya pili, kisha Clatous Chama amefunga moja kwa faulo dhidi ya Vital’O katika ushindi wa 6-0.
USIWARUHUSU NDANI YA BOKSI
Kwa aina ya mabao ambayo Yanga imefunga, inaonyesha wazi kwamba timu hiyo ni hatari zaidi ukiiruhusu kuiingia katika boksi lako. Takwimu zinaonyesha kwamba, katika mabao 18, mawili pekee yamefungwa nje ya boksi ambayo ni kutoka kwa Aziz Ki na Clatous Chama ambao wote walifanya hivyo dhidi ya Vital’O. Chama alipiga faulo na Aziz Ki aliachia shuti kali.

Mabao yaliyobaki ambayo ni 16 yote wachezaji wamefunga wakiwa ndani ya boksi la wapinzani. Hapa pia linaingia lile walilojifunga Azam ambapo beki wao Yoro Diaby alijifunga akiwa ndani ya boksi.
WALIOFUNGA HAWA HAPA
Ukiliondoa bao moja pekee ambalo limetokana na wapinzani kujifunga, 17 yaliyobaki yamefungwa na wachezaji saba tofauti huku Prince Dube na Clement Mzize wakiongoza kila mmoja akifunga manne.
Dube katika mabao yake, amefunga mawili dhidi ya Vital’O na moja dhidi ya CBE katika Ligi ya Mabingwa huku lingine ni fainali ya Ngao ya Jamii dhidi ya Azam.
Mzize mabao yake amefunga moja Ngao ya Jamii dhidi ya Azam, mawili dhidi ya Vital’O katika Ligi ya Mabingwa na moja Ligi Kuu Bara mbele ya Kagera Sugar.
Anayefuatia ni Aziz Ki aliyefunga mabao matatu yakiwamo mawili dhidi ya Vital’O katika Ligi ya Mabingwa na moja fainali ya Ngao ya Jamii dhidi ya Azam.

Clatous Chama amefunga mabao mawili yote dhidi ya Vital’O katika Ligi ya Mabingwa sawa na Maxi Nzengeli ambaye moja alifunga nusu fainali ya Ngao ya Jamii dhidi ya Simba, lingine Ligi Kuu dhidi ya Kagera Sugar. Waliofunga mojamoja ni Mudathir Yahya na Pacome Zouzoua ambao wote wamefanya hivyo dhidi ya Vital’O katika Ligi ya Mabingwa.
ASISTI ZIPOJE?
Hapa anayeongoza kwa kutengeneza mabao ni Chama ambaye alitisha zaidi katika mchezo wa pili wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Vital’O na alikuwa nazo nne. Jumla Chama ana asisti tano nyingine akitoa katika fainali ya Ngao ya Jamii dhidi ya Azam. Aziz Ki ana asisti mbili alizotoa katika Ligi Kuu Bara dhidi ya Kagera Sugar na CBE katika Ligi ya Mabingwa.
Prince Dube ana asisti moja aliyoitoa katika nusu fainali ya Ngao ya Jamii dhidi ya Simba.
Mudathir Yahya ana asisti moja aliyoipiga katika fainali ya Ngao ya Jamii dhidi ya Azam kama ilivyo kwa Pacome aliyefanya kwenye mchezo huo.
DIARRA MZEE WA CLEAN SHEET
Katika mechi zote hizo sita ambazo Yanga imecheza msimu huu katika mashindano, kipa namba moja wa kikosi hicho, Djigui Diarra amekaa langoni na kuondoka uwanjani akiwa hajaruhusu nyavu zake kutikiswa mara tano ‘cleansheet’, akiruhusu mara moja kufungwa na Azam.

Wakati Diarra akipata sifa za kukomba clean sheet tano, analindwa na mabeki imara zaidi ambao ni Yao Kouassi, Dickson Job, Ibrahim Bacca, Bakari Mwamnyeto, Chadrack Boka na Nickson Kibabage. Kati ya mabeki hao, waliocheza mechi kwa dakika zote ni Job na Bacca pekee huku wengine wakiingia na kutoka.
MCHANGANUO DAKIKA ZA MABAO
DAKIKA: 1-15
MABAO: 2
WAFUNGAJI: Prince Dube dakika ya 5 dhidi ya Vital’O na Pacome Zouzoua dakika ya 13 dhidi ya Vital’O.
DAKIKA: 16-30
MABAO: 4
WAFUNGAJI: Prince Dube dakika ya 18 dhidi ya Azam, Maxi Nzengeli dakika ya 25 dhidi ya Kagera Sugar, Yoro Diaby wa Azam alijifunga dakika ya 27 na Aziz Ki dakika ya 30 dhidi ya Azam.
DAKIKA: 31-45
MABAO: 2
WAFUNGAJI: Maxi Nzengeli dakika ya 44 dhidi ya Simba na Prince Dube dakika ya 45+1 dhidi ya CBE.

DAKIKA: 46-60
MABAO: 2
WAFUNGAJI: Clement Mzize dakika ya 48 dhidi ya Vital’O na Clatous Chama dakika ya 50 dhidi ya Vital’O
DAKIKA: 61-75
MABAO: 3
WAFUNGAJI: Clatous Chama dakika ya 68 dhidi ya Vital’O, Prince Dube dakika ya 71 dhidi ya Vital’O na Clement Mzize dakika ya 74.
DAKIKA: 76-90+
MABAO: 5
WAFUNGAJI: Aziz Ki dakika ya 78 dhidi ya Vital’O, Mudathir Yahya dakika ya 86 dhidi ya Vital’O, Clement Mzize dakika ya 88 dhidi ya Kagera Sugar, Aziz Ki dakika ya 90 dhidi ya Vital’O na Clement Mzize dakika ya 90+2 dhidi ya Azam.
SIMBA, AZAM, COASTAL
Wakati Yanga ikifunga mabao 18 na kuruhusu moja msimu huu, inaonekana kuwafunika top 4 wenzake wa ligi msimu uliopita ambao ni Azam, Simba na Coastal Union ambao wote wameshiriki Ngao ya Jamii, Ligi Kuu Bara na kimataifa.
Takwimu za Azam zinaonyesha kwamba, katika mechi sita ilizocheza imefunga mabao saba na kuruhusu nane, ikishinda mechi mbili, sare (2) na kupoteza (2).
Simba imecheza mechi tano, imefunga mabao 8 na kuruhusu moja, ikishinda mechi tatu, sare moja na kupoteza moja, wakati Coastal Union mechi sita ilizocheza imefunga mabao manne na kuruhusu kumi ikishinda moja, sare mbili na kupoteza tatu.