Sven anapomfundisha Aussems kuishi na sisi

Thursday January 14 2021
sven picha mkataba
By Khatimu Naheka

KUISHI na Mtanzania kama mimi hasa ukiwa umetokea sehemu ambayo wamestarabika zaidi ni kazi ngumu ambayo inahitaji ujasiri kuweza kufanikiwa,wakati mwingine ukiwa na roho nyepesi maisha yako na Mtanzania unaweza kujikuta safari yako ikiishia njiani.

Nasema hivi kwasababu sisi Watanzania wengi tunapenda kuishi maisha ambayo sio halisi kwetu tunachozungumza ni tofauti na tunachomaanisha au wakati mwingine msimamo tunaoonyesha ni tofauti na kile kinachoendelea kwenye mioyo.

Wiki iliyopita kuna matukio mawili yalijiri hapa, moja likiwa la furaha lakini lingine lilikuwa na mshtuko ambao wengi hatukutegemea kusikia au kuona kitu kama hicho kikitokea na bahati mbaya zaidi matukio yote staa wa filamu alitoka katika familia moja.

Jumatano kama ya jana wiki iliyopita Tanzania ilifurahia tukio la Simba kutinga hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika wakiupiga mpira mwingi na wakionyesha ukomavu mkubwa wakipata mabao ambayo yaliwavusha kwenda hatua hiyo muhimu wakiwachapa FC FC Platinum kwa mabao 4-0.

Ushindi huo wa Simba ulikuwa umesimamiwa na kocha Mbelgiji Sven Vandenbroeck akiwa kama kocha mkuu, lakini akionyesha kazi hiyo bora akimtangulia Mbelgiji mwenzake Patrick Aussems ambaye mwaka mmoja uliopita katika uwanja huohuo alifanya tukio kama hilo.

seven pic
Advertisement

Kabla ya mchezo huo wengi tulidhani kwamba haitakuwa rahisi kwa Simba kumvumilia Sven endapo wangeng’olewa na Platinum, na uvumi kama kawaida yetu ulienea kwamba tayari mabosi wakubwa wa Simba walishaanza kutafuta mbadala wake wakijiweka sawa na maamuzi yao.

Huwezi kuupuza sana uvumi huo hasa katika soka letu na Zaidi klabu hizi kubwa mbili mara nyingi linalosemwa sana hutokea ndani ya muda mfupi baadaye kutokana na aina ya amsiha tunaishi.

Wakati uvumi huo ukiishi ghafla Sven akapindua meza akiiongoza Simba kushinda kibabe na kuwaondoa Wazimbabwe hao ambao kabla walionekana kuwa na timu imara,na Simba kushinda kwa mabao hayo kasha mawindo ya kumng’oa yakaishia hapo na hata wale waliotaka kumng’oa nao walionekana kushangilia ushindi.

Siku moja baadaye wakati mashabiki na hata taifa likifurahia ushindi wa Simba ghafla jamaa anatangaza kuondoka akidai anataka kwenda kukaa na familia yake kwa karibu taarifa ambayo sio tu kushtua bali ilichanganya kidogo kuamini kocha anaweza kuacha hatua nzuri kama ile ambayo aliifanya katika ajira yake. Hakika lilikuwa ni jambo la kimyakimya sana Sven alituonyesha Watanzania lakini saa chache tena yaani siku inayofuata tu Sven akatuchekesha zaidi akituonyesha familia ambayo anakwenda kukaa nayo kwa karibu akitua klabu kongwe ya FAR Rabat ya Morocco akisaini mkataba wa miaka miwili.

Hapa nikapata picha kwamba kumbe Watanzania hatujashindokana kwa unafiki, lakini kuna watu wametuzidi na wanaweza kuishi na sisi kwa sura tunazotaka kuishi nazo.

Picha halisi ambayo naipata hapa ni kwamba Sven alikutusoma vyema na ina maana alijua wazi kipi kinasubiriwa kwake na anatakiwa aishi vipi na sisi. Hakutaka kufanya makosa ambayo kama mtangulizi wake Aussems aliyafanya akiondoka nchini kwenda kufanya mazungumzo na klabu nyingine. Badala yake Sven alifanya mambo yake kimyakimya na wakati Simba wakidiwa kumuwinda naye aliwawinda kivyake na mwisho wa siku mshindi akabaki yeye akitunza heshima yake kwa maamuzi ya kibabe. Tangu anafika hapa Sven siku zote alionekana mtu mkimya ambaye hakutaka kuonyesha uhalisia wa kipi kipo ndani ya akili yake na hivi ndivyo mwanadamu anatakiwa kuishi ni kama alijua makosa ambayo Aussems aliyafanya ambayo mwisho wa siku yaliwapa ushindi Simba kwa kumtimua.

Ni vigumu Simba kumrudia Aussems kuwa kocha tena ingawa kila kitu chini ya jua kinawezekana na hili linatokana na hakutaka kuweka akiba yake ya kesho kwa jinsi alivyoachana na klabu hiyo. Katika hatua hiyo hiyo naona ipo siku Sven anaweza kurejea kuwa kocha wa Simba na wakaishi naye kwa adabu kwa kuwa wanajua jeuri yake jinsi alivyowapiga chenga ya mwaka akiwaacha kituo cha basi kisha yeye akichukua usafiri mwingine wa haraka kuwahi anakotaka kwenda.

Tunaweza kujifunza hapa kupitia elimu ya Sven kila la heri kocha mwenye misimamo ya kipekee.

Advertisement