SPOTI DOKTA: Sababu za Yacouba kuwa nje miezi mitano

MSHAMBULIAJI wa Yanga, Yacouba Songne ambaye alirejea wiki iliyopita akitokea nchini Tunisia katika matibabu ya upasuaji wa goti lililojeruhiwa atakuwa nje ya uwanja kwa miezi mitano.

Itakumbukwa kuwa mshambuliaji huyu ambaye anatokea nchi ya Burkina Faso aliumia katika mechi dhidi ya Ruvu Shooting baada ya kucheza kwa dakika 31 tu za mchezo huo.

Kwa mujibu wa daktari wa viungo wa Yanga, Youssef Mohmed ambaye alifuatana na Yacouba kule Tunisia katika matibabu hayo alisema kuwa mchezaji huyo atakuwa nje kwa miezi mitano.

Mchezaji huyu alifanyiwa upasuaji huo na daktari nguli wa upasuaji wa magoti nchini humo Profesa Jaleleddine ambaye anajulikana sana kwa kuwatibu kwa mafanikio nyota mbalimbali wa Afrika.

Ilielezwa kuwa upasuaji huo ulikwenda vizuri kwa mafaniko na inatarajiwa katika programu ya uponaji ya miezi mitano kupita atakuwa tayari amerudi kuanza mazoezi.

Katika jicho la kitabibu, aina hii ya majeraha ya goti ni kawaida kuchukua muda mrefu hasa kwa wanasoka ambao wanacheza mchezo huo ambao unahusisha kugusana kimwili na kutumia nguvu na kasi.

Mtakumbuka hata beki wa kimataifa wa Liverpool, Virgil Van Dijk aliwahi kukumbwa na mkasa wa kuumia goti katika msimu uliopita kiasi cha kutakiwa kuwa nje kwa mwaka mzima.

Lakini alipona baada ya kufanyiwa upasuaji wa kisasa na hatimaye kupona na hivi sasa anaendelea kucheza kama hapo awali.

Wachezaji wengine wakubwa duniani ambao nao wamewahi kuumia na kukaa nje ya uwanja kwa zaidi ya miezi 6 na hatimaye kupona na kurudi uwanjani ni pamoja na Alex OxladeChamberlain wa Liverpool, Eden Hazard akiwa Chelsea, Luke Shaw wa Manchester United na Edinson Cavani akiwa PSG.

Mara nyingi aina ya majeraha wanayoyapata mara kwa mara wachezaji wa soka ni kukatika kwa nyuzi ngumu za ligamenti za eneo la katikati ambazo zinajulikana kama Anterior Cruciate Ligament kifupi ACL.

Sababu kubwa ya kitababu ambayo imeonekana kusabababisha majeraha ya ligamenti za goti kuchukua muda mrefu kupona ni kutokana na kamba hizi ngumu kutokuwa na vimishipa vya damu vingi.

Yaani kwa maneno mengine ni kuwa tishu hizi hazina mishipa mingi ya damu ili kupeleka mahitajio ya seli, hivyo hali hii inasababisha tishu hizi kuunga na kupona taratibu.

Ili tishu iliyojeruhiwa mwilini iweze kupona kwa haraka moja ya jambo la msingi ni eneo hili kuwa na mishipa ya damu ya kutosha ambayo hubeba damu yenye vitu muhimu kwa seli kuweza kufanya kazi zake.

Kiasili ilivyoumbwa tishu za ligamenti hazina mishipa ya damu ya kutosha ukilinganisha na tishu kama mishipa.

Mara nyingi aina hii ya majeraha kama yamehusisha mchaniko wa ligamenti huwa yanaweza kuchukua miezi 9 kupona tangu kutibiwa.


Majeraha ligament ya ACL yako hivi

Kazi kubwa ya kamba za ligamenti ni kuunganisha mfupa mmoja na mwingine, katika goti zipo aina kuu nne za nyuzi zinazounganisha mifupa iliyopo katika ungio la goti.

Inawezekana jeraha la Yacouba halikuwa mchaniko mkubwa wa kuchanika vipande viwili ambalo aina hii ya jeraha huangukia daraja la tatu.

Kwa namna alivyoumia katika mchezo ule wa Ruvu kuna kila ishara kuwa alipata aina hii ya jeraha la nyuzi ya ligamenti ACL ambalo huweza kuchanika au kukwanyuka kutoka katika mfupa uliojiunga.

Ligamenti ya ACL ndiyo mhimili mkuu wa ungio la goti ikiwa eneo la katikati ya goti ikiunganisha mfupa mkubwa wa paja na wa chini ya goti.

Jeraha alilopata la Ligamenti linaainishwa kama daraja la tatu ambayo nyuzi hiyo hukatika pande mbili na kuachana au kukwanyuka katika mfupa uliojipachika.

Kwa kawaida majeraha ya ligamenti huanishwa katika aina tatu za majeraha, aina ya kwanza huwa ni kujivuta kupita kiwango na aina ya pili ni kuchanika pasipo kuachana pande mbili.

Daraja la tatu huwa ni jeraha baya linalohitaji upasuaji kama sehemu ya matibabu jambo linalochagia mchezaji kukaa nje ya uwanja muda mrefu akiuguza jeraha la upasuaji.

Jeraha hili huwa ni kubwa na huambatana na maumivu makali ambayo yanaweza kuanza ghafla baada ya kujeruhiwa au kidogo kidogo na inaweza kuambatana na mlio usio wa kawaida katika goti.

Aina hii ya majeraha huweza kuchukua muda mrefu kupona na kurudi tena uwanjani, jeraha hili linaweza kumweka nje kwa zaidi ya miezi 9 mpaka mwaka.

Nyuzi ngumu za ACL ziko kama herufi ‘X’, kazi yake ni kuzuia mifupa inayounda ungio la goti kutulia katika eneo lake na isiteleze kwenda upande wa nyuma ya goti na vile vile kuwezesha goti kujizungusha. Ikumbukwe kuwa goti lina mijongeo mikuu mitatu ikiwamo kunyooka, kupinda kutoka mbele kuja nyuma na kujizungusha. Hivyo basi uelekeo mwingine wowote nje ya hii huweza kusababisha jeraha.

Ukiacha vipimo mbalimbali, kipimo muhimu ni cha MRI ndicho kinatoa taswira nzuri juu ya vitu vilivyomo katika ungio la goti na kubaini kwa kina ukubwa wa jeraha. Majeraha ya michaniko au kukwanyuka katika mfupa yanayohusisha daraja la tatu huwa yanahitaji upasuaji kwa lengo la kuikarabati nyuzi hiyo na kuirudishia na kuipachika mahali pake.

Daktari wa upasuaji hivi sasa wanafanya upasuaji wa kisasa wa matundu na huku wakichukua tishu nyingine na kuipandikiza katika eneo hilo lililojeruhiwa. Hivi sasa Yacouba ataendelea kuwa katika uangalizi wa madaktari wa timu hiyo na watakuwa wakituma taarifa za maendeleo yake ya uponaji kwa daktari wake nchini Tunisia.