Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

SPOTI DOKTA: Kwa nini mabasi ya timu hupata ajali?

Muktasari:

  • Ajali hiyo inaelezwa ilitokana na basi walilokuwa wakisafiria wachezaji na baadhi ya maofisa wa timu hiyo kutoka makao makuu ya nchi, Dodoma, kupinduka wakati likiwa njiani kwenda Dar es Salaam kuwahi pambano jingine la ligi dhidi ya Simba ambalo hata hivyo liliahirishwa.

FEBRUARI 10, mwaka huu, medani ya soka ilipata mshtuko baada ya Dodoma Jiji kupata ajali barabarani ikitokea Lindi ilikoenda kucheza mechi ya Ligi Kuu Bara dhidi ya wenyeji wake, Namungo na mchezo kuisha kwa sare ya mabao 2-2.

Ajali hiyo inaelezwa ilitokana na basi walilokuwa wakisafiria wachezaji na baadhi ya maofisa wa timu hiyo kutoka makao makuu ya nchi, Dodoma, kupinduka wakati likiwa njiani kwenda Dar es Salaam kuwahi pambano jingine la ligi dhidi ya Simba ambalo hata hivyo liliahirishwa.

Katika ajali hiyo hakuna aliyepoteza maisha, isipokuwa wachezaji saba kati ya 37 walilazimika kuwahishwa hospitali na kushonwa nyuzi kadhaa kutokana na majeraha ya michaniko iliyotokana na kukatwakatwa na vioo.

Jicho la kitabibu la Mwanaspoti Dokta limeona kuna la kujifunza katika ajali hiyo ambayo ilitishia uhai wa wachezaji, japo tayari timu hiyo imerejea katika mechi za ligi kwa juzi usiku ikiwa nyumbani Uwanja wa Jamhuri kushinda mabao 3-2 mbele ya Tanzania Prisons.

Hatua ya awali ya kuipumzisha timu hiyo katika ligi kiafya ni muhimu ili kuwapa muda wa kuwa timamu kimwili na kiakili wachezaji. Ikumbukwe ni kawaida baada ya ajali wachezaji kuathirika kiakili ikiwamo hofu.

Usalama wa wachezaji 37 ulibebwa na dereva mwendesha basi, hivyo hakuna budi kuhakikisha kuwa madereva kama wapo wanaopokezana wote wapo timamu kiafya kuendesha.

Takwimu zinaonyesha kuwa hiyo ni ajali ya tatu katika miaka mitano iliyohusisha klabu za mpira wa miguu hapa Tanzania.

Itakumbukwa Oktoba 26 mwaka jana, msafara wa JKT Tanzania ulipata ajali na Julai 9, 2021 kikosi cha Polisi Tanzania kilipata ajali kikitokea mazoezini kwenye Uwanja wa CCP Moshi.

Katika ajali hiyo ilimsababishia ulemavu wa kudumu mshambuliaji wa timu hiyo, Gerald Mdamu na kushindwa kurudi katika soka uwanjani.

Tukio hilo, Mwanaspoti Dokta iliandika majeraha yake na sababu za kuwa katika hali hiyo. Pamoja na kuwa na takwimu chache za mabasi ya timu kupata ajali, lakini lazima tahadhari zichukuliwe kwa kuzingatia miongozo ya kitabibu na kushikamana na sheria zote za barabarani.

Kwa mujibu wa taarifa ya ajali ilielezwa kuwa ilitokana na dereva kuwa katika mwendo mkali akiwa anashuka katika mteremko hakuona vizuri, hivyo kuacha njia na kuporomokea mtoni.

Hivyo basi ni muhimu kupata ufahamu kupitia tukio hilo ili kuweza kuchukua tahadhari na hatimaye kupunguza hatari ya kupata ajali.


HALI YA KIFYA YA DEREVA

Kwa mujibu wa takwimu za dunia za ajali za barabarani mara nyingi huwa ni makosa ya kibanadamu. Sina hakika kwa timu zetu za dunia ya tatu kama zina utaratibu wa kuzingatia usalama.

Moja ya mambo muhimu yanayohusisha usalama wa wasafari hasa kwa magari ya usafirishaji ni kutazama hali ya afya ya dereva kwa kuzingatia miongozo ya tiba na usalama wa vyombo hivyo.

Dereva anayebeba abiria mara kwa mara kusafiri umbali mrefu ni muhimu kutazamwa afya kabla ya kuanza mwendo huo. Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na vyombo vya habari, ajali hiyo ilitokea saa tatu asubuhi katika eneo la Nangurukuru na Somango ambalo lina mtetereko mkali.

Mashuhuda wanaeleza kuwa eneo hilo liliharibiwa na mvua za kimbunga, hivyo kwa ambaye si mpitaji wa mara kwa mara ni vigumu kubaini au kuona hatari iliyopo.

Kwa kawaida madereva wa vyombo vikubwa vya moto vya abiria kwenda umbali mrefu hufanyiwa uchunguzi wa jumla wa afya angalau kwa miezi sita mara moja au kwa mwaka mara moja.

Pia kuna uchunguzi wa kabla ya kuendesha chombo ambapo hata tabibu wa kawaida anaweza kuzungumza na dereva na kumuuliza maswali mawili matatu na kubaini viashiria vya tishio la kiafya. Mfano mtaalamu wa afya kwa kuzungumza tu na dereva anaweza kubaini kuwa jana yake hakulala vizuri na pengine amelala saa nne na huku pia akiwa katika mazingira ya kusumbuka kwa usingizi. Dereva wa chombo ambaye amelala chini ya saa nane katika usiku mmoja anakabiliwa na mchoko au uchovu.

Hali hiyo ikiwepo inavuruga utendaji kazi wa ndani ya mwili katika mifumo mbalimbali ikiwamo mfumo wa fahamu wenye kuhusisha ubongo.

Dereva ambaye ana uchovu mkali au ambaye amelala saa chache au ambaye jana yake alikunywa pombe au kutumia dawa za kulevya, utendaji kazi wa mfumo fahamu yaani ubungo unavurugika.

Kazi za ubongo kama kupokea na kusafirisha taarifa, kufikiri, kufanya uamuzi sahihi haraka, umakini, kutunza kumbukumbu au kukumbuka kwa usahihi huathirika.

Hali kama hiyo utendaji wa akili unapoingiliwa na mambo kama uchovu ni mojawapo ya sababu ya kutokea kwa ajali ambazo ndizo huangukia katika makosa ya kibinadamu.

Ingawa ni kweli miundombinu mibaya ya barabara ni moja ya vitu vinavyochangia kutokea kwa ajali, lakini makosa ya kibanadamu hayakwepeki ambayo yanaweza yakachangiwa na mambo binafsi, eneo la kazi na mazingira yake. Pengine kutoona vizuri kwa dereva kulichangiwa na uoni hafifu wa macho. Lakini pengine angekuwa anafanyiwa uchunguzi wa afya ikiwamo macho ingewezekana kujua tatizo.

Vilevile ni muhimu sana kuwapatia haki za msingi madereva ikiwamo malipo ili kuwapa hamasa, likizo au mapumziko, maslahi na uhuishaji mafunzo ya udereva.

Ikumbukwe pia dereva aliyesoma chuo dhaifu na kupata leseni kwa njia ya mkato huku pia sheria za ukaguzi zikiwa hazizingatiwi, ni rahisi kufanya makosa ya barabarani.


Dereva akibainika kuwa na haya asiendeshe gari

1. Kama dereva ametumia pombe jana yake saa chache kabla ya kuendesha hatakiwi kuendesha gari. Pombe inaingilia utendaji kazi wa mwili ikiwamo mfumo wa fahamu wa ubongo.

2. Dereva ambaye ni mgonjwa hatakiwi kuendesha gari kwani kuumwa kunaingilia utendaji kazi wa mwili katika mifumo.

3. Matumizi ya dawa za matibabu. Zipo baadhi ya dawa ambazo dereva akitumia zinaweza kumlevya au kumsababishia usingizi au kizunguzungu. Hivyo akiwa katika matibabu asiendeshe.

4. Dereva mwenye viashiria vya shinikizo la akili yaani stresi hatakiwi kuendesha kwani tatizo linaweza kumfanya kuwa na uamuzi mbovu na kukosa umakini.

5. Mvurugiko wa hisia ikiwamo kukosa furaha au kuwa na furaha iliyopitiliza. Hisia yaani emotions zikienda mrama zinavuruga utendaji wa mwili.

6. Uchovu kitabibu ni fatigue. Hali hiyo inaweza kuwa ya wastani, sugu au uchovu mkali wa muda mrefu. Hivi ni vitu vinavosababisha madereva kusababisha ajali.

Ndio maana inahitajika madereva kupewa kazi kwa kipimo, huku wakipewa muda wa kupumzika, kulala na kuburudika.


CHUKUA HII

Wataalamu wa afya wanaweza kuchunguza, kutibu na kuboresha afya za waendesha vyombo vya moto ikiwamo madereva wa mabasi ya klabu, hivyo ni muhimu kuwatumia.