SPOTI DOKTA: Joto hili Pwani tishio kwa wachezaji

NI mchana uko katikati ya jiji la Dar es Salaam joto liko juu ukiwa katika msongamano pengine unatembea tu unajikuta ukitokwa jasho jingi na baadaye kukupa kiu kali ya maji.
Kumbuka hapo unatembea tu unapata hali hiyo, jaribu kujilinganisha na mchezaji anayeshiriki ligi zenye ushindani au kucheza mchezo wenye ushindani nyakati za alasiri katika hali ya hewa ya sasa katika maeneo ya pwani atakua ana hali gani.
Ushiriki wa michezo kama vile Ligi Kuu Bara au kama mechi za kimataifa zinazochezwa jijini humo au kufanya mazoezi katika maeneo ambayo kwa sasa yana hali ya joto kali inaweza kumweka mchezaji katika hatari kiafya.
Sababu kubwa ya hatari hiyo ni kutokana na mwili kupoteza maji na chumvi chumivi au madini mwilini kwa kiwango kikubwa kuliko kawaida.
Endapo upotevu wa maji mwilini hautadhibitiwa ndivyo hatari ya athari hizo zinavyokuwa juu na pia kadiri hali ya hewa ya joto inapozidi kuwa juu na ndivyo maji hupotea zaidi mwilini.
Maeneo ya ukanda wa Pwani ambayo sasa yanaonyesha kuwa na joto kali ni pamoja na Tanga, Dar es Salaam, Pwani, Unguja na pemba kusini Mtwara na Lindi na kanda ya kaskazini Kilimajaro.
Joto hili katika mikoa hii ya pwani ni tishio kwa wachezaji wa soka ambao mchezo huu unaohusisha kasi na nguvu. Ni vyema kujua athari au madhara yanayoweza kuwapata wachezaji wanaocheza katika mikoa hiyo yenye joto kali.
Wanaweza kuathirika kama hivi
Upungufu wa maji mwilini ni mambo ya jambo ambalo linaweza kujitokeza kipindi hiki cha joto kali na huku ikiwa hewa ni kavu isiyo na unyevu.
Kwa kawaida mwili huitaji maji na chumvu chumvu kwa ajili ya kazi mbalimbali za mwili ikiwamo msukumo wa damu na kazi seli mbalimbali.
Wachezaji wanapokuwa katika mazingira ya joto huku wakifanya mazoezi makali au kucheza mechi zenye ushindani hutokwa na jasho sana hivyo kupoteza maji mengi na chumvi mwilini.
Ikumbukwe kuwa kadiri joto linavyozidi kuwa kali ndivyo mwili unavyotoa jasho zaidi, lengo ni kupunguza joto la ndani ya mwili lisizidi kiwango chake cha mwisho.
Kuvuja jasho sana huwa ni zaidi wakati wa kucheza katika joto kali, wakati huo huo kadiri jasho linavyotoka kwa wingi na ndivyo pia mwili unavyopoteza maji kupita kiasi.
Matatizo mbalimbali ya kiafya yanaweza kujitokeza endapo tu mchezaji atapata upungufu mkali wa maji mwilini na chumvichumvi kutokana na kuvuja jasho sana.
Hali hii inaweza kuambatana na madhara mbalimbali ya kiafya ikiwamo kuuma na kubana kwa makundi ya misuli ikiwamo ya ile ya nyuma ya paja ambayo ni muhimu kwa mchezaji kama wa soka.
Upungufu wa maji na chumvi mwilini usipokabiliwa kwa kuupoza mwili na kurudishia kiwango cha maji kilichopungua inaweza kuleta madhara makubwa kiafya.
Matatizo hayo ni pamoja na kupata mchoko mkali na kiharusi kitokanacho joto kali na kupoteza fahamu, mambo haya yanaweza hata kusababisha kifo kwa mchezaji.
Madhara mengine yanayoweza kutokana na hali ya kutokwa sana na jasho na kupungiwa maji mwilini ni pamoja na kichwa kuuma, kuona mawimbi, mwili kuwa dhaifu, kushindwa kutulia, kukosa umakini mazoezini au mchezoni, kuchanganyikiwa, kichwa kuuma na mwili kuuma.
Tatizo hilo la upungufu wa maji kutokana na joto kali linaweza kumfanya mchezaji akashindwa kucheza kwa kiwango au akacheza lakini akachoka mapema
Hali ikiwatokea wachezaji wanaweza wakadhaniwa kuwa wanafanya makusudi au kwa mazingira yetu ukadhani wamehongwa kumbe tu wana upungufu wa maji mwilini kutokana na kutoka jasho sana.
Mara nyingi wachezaji ambao wanapata madhara haya kirahisi ni wale ambao hawanywi maji ya kutosha kabla ya mechi, na vile vile kutokula vyakula vyenye maji na madini ikiwamo matunda na mboga.
Kinachotakiwa kufanyika ni hiki
Wachezaji wanywe maji mengi siku mbili kabla ya mechi ikiwezekana kwa lita 3-5 za maji kwa siku. Unywaji maji uwe ni utamadani wa wakati wote kwa wachezaji ni si wakati wa joto pekee.
Kwa watu wa kawaida glasi 8-10 kwa siku zinatosha kukabiliana na upungufu wa maji mwilini kipindi cha joto kali.
Usisubiri kiu ije ndo unywe maji na yanywewe mara kwa mara au kunywa kidogo mpaka ufikie lengo linalotakiwa.
Vile vile kula matunda kwa wingi kila baada ya mechi na katika mlo wao kutumia mboga mboga kwa wingi. Matunda na mboga huwa na maji mengi na madini (chumvichumvi).
Ni muhimu mchezaji akatambua umuhimu wa kunywa maji ya kutosha kabla ya kuingia mazoezini au katika mechi na vile vile kunywa maji kila baada ya nusu saa au wakati wa mapumziko na baada ya kumaliza mazoezi au mechi. Si vibaya kwa klabu zenye uwezo kutumia vinywaji maalum kwa ajili ya wanamichezo ambapo ndani yake huwa na wanga na chumvichumvi. Vinywaji hivi kama vinavyojulikana sports drinks ni muhimu kutumia.
Kwa faida ya wote, vinywaji vya kuongeza nguvu na kusisimua au kuchangamsha mwili maarufu kama energy drinks sio vinywaji sahihi kutumia kwa mtu kuongeza maji mwilini.
Pia pombe, soda na kahawa sio mbadala wa maji yaliyopotea kwa mjia ya jasho.
Kipindi hiki wachezaji waepuke kukaa au kutembelea maeneo yenye joto na msongamano, badala yake wakae maeneo ya wazi yenye kivuli hasa kabla ya mechi. Ni muhimu kuupumzisha mwili kwa kulala angalau masaa nane kwa siku.
Kama joto litakuwa ni kali sana ni vizuri kucheza wakati linapokuwa limepungua. Epuka kucheza mchana wakati joto ni kali zaidi.
Tumeona hata katika mechi ya kimataifa iliyochezwa wiki iliyopita katika ya taifa stars na Benin na juzi dhidi ya Sudan ilichezwa jioni kuelekea usiku muda ambao angalau joto linakua limepungua.
Vizuri kutoa mapumziko ya katikati ya mechi ili kutoa nafasi wachezaji kunywa kiasi kidogo cha maji ili kukabiliana na hali hiyo. Joto hili ni tishio kwa wachezaji vizuri watoe taarifa mapema kwa madaktari wa timu mara tu wanapopata dalili na viashiria vya madhara ya joto kali.