Song, Kalou kumbe wana jambo la Dar

Song, Kalou kumbe wana jambo la Dar

KAMA hujui ndio ujue sasa. Si unakumbuka kwenye tamasha la Simba Day, kuna sura zilizowahi kutamba katika Ligi Kuu mbalimbali barani Ulaya zilikuwa kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa!

Ndio, kulikuwa na Alexandre Song na Solomon Kalou waliowahi kuwika na klabu za Arsenal na Chelsea zinazokimbiza kwenye Ligi Kuu ya England (EPL).

Sasa kama hujui nyota hao wapo nchini wakiwa na kikosi cha timu yao wanayoichezea kwa sasa ya AS Arta Solar 7, iliyojichimbia katika kambi yao iliyopo hoteli ya CBD mitaa ya Kamata Kariakoo, jijini Dar es Salaam na watakuwa hapa si chini ya kipindi cha mwezi mmoja.

Arta iliwanasa mastaa hao wawili wakubwa kwa ajili ya michuano ya Ligi Kuu ya Djibouti na ile ya Ligi ya Mabingwa Afrika inayosimamiwa na Shirikisho la Soka Afrika, CAF.

Kalou aliwahi kucheza soka la kulipwa katika timu kubwa duniani kama Chelsea ya England na Lille ya Ufaransa.

Staa huyo raia wa Ivory Coastal kabla ya kujiunga na Arta amewahi kupita Botafogo ya Brazil, Hertha, Lille, Chelsea msimu wa 2006-12 na hapa ndio alitambulika zaidi duniani kutokana na uwezo wake wa soka kabla ya hapo alipita Excelsior na Feyernood.

Katika kucheza kwake Kalou ameonyesha ni mchezaji mkubwa kutokana na mafanikio aliyoyapata katika timu mbalimbali akiwa na Chelsea alichukua ubingwa wa Ligi Kuu ya England mara moja msimu wa 2009-10.

Kalou akiwa na Chelsea amechukua ubingwa wa Kombe la FA mara nne msimu wa 2006-07, 2008-09, 2009-10 na msimu wa 2011-12, ubingwa wa kombe la ligi mara moja 2006-07 na alikuwa kwenye kikosi kilichotwaa ubingwa wa UEFA 2012.

Akiwa na timu ya taifa ya Ivory Coast amechukua ubingwa wa Mataifa ya Afrika 2015, mbali ya hivyo amechukua tuzo mbili binafsi, Mchezaji Bora wa msimu wa CAF mwaka 2008 na tuzo ya Johan Cruyff 2005.

Kwa upande wa nahodha wa zamani wa Arsenal ya England, Alexandre Song ambaye baada ya dunia kumfahamu zaidi akiwa na The Gunners, amepita katika timu mbalimbali kubwa Ulaya kama FC Barcelona 2012-16, West Ham United, Rubin Kazan na sasa kuibukia Arta aliyojiunga nayo mwaka 2020.

Song amecheza kwenye kikosi cha timu ya taifa ya Cameroon kwa kiwango bora na akiwa na Arsenal walikuwa washindi wa pili wa Kombe la Ligi 2010-11. Alipokwenda Barcelona alichukua ubingwa wa Ligi Kuu ya Hispania 2012-13 na walikuwa washindi wa pili katika mashindano ya Supercopa na Copa Del Rey.

Msimu uliopita akiwa na kikosi cha Arta amefanikiwa kuchukua nao ubingwa wa Ligi Kuu nchini Djibouti wakati mafanikio katika timu ya taifa Cameroon alianza kuyapata 2003 alipochukua ubingwa wa vijana.

Katika timu ya taifa ya wakubwa Song alikuwepo kwenye kikosi kilichokuwa washindi wa kombe la Mataifa Afrika 2008 na msimu huo huo alichaguliwa katika kikosi bora cha mashindano hayo.


AS ARTA SOLAR 7

Klabu hii ya Association Sportive d’Arta (ambayo kwa sasa inajulikana kama Arta Solar 7 kwa sababu za udhamini) ni klabu ya soka kutoka Arta, Djibouti ambayo inacheza Ligi Kuu ya Djibouti. Wao ndio mabingwa kwa msimu uliopita.

Uwanja wa nyumbani, kwa timu zote za Djibouti, ni Uwanja wa El Hadj Hassan Gouled Aptidon wenye uwezo wa kuchukua watazamaji 20,000 hasa moja kati ya timu za taifa hilo zinaposhiriki michuano ya kimataifa.

Klabu hii ilianzishwa kama AS Compagnie Djibouti-Ethiopie mwaka wa 1980.

Baadaye ikaanza kufahamika kama AS CDE/Arta The Fairy Mountaineers baada ya kufadhiliwa na Shirika la Reli la Ethio-Djibouti (C.D.E.), Arta/SIHD na Jumuiya ya Kimataifa ya Hydrocarbon.

Kufikia 2018, klabu hiyo ilianza kujulikana kama Arta Solar 7, kutokana na udhamini wa kampuni ya Solar Power yenye makao yake makuu nchini Djibouti, Solar 7. Inaelezwa kuwa udhamini huo umewafanya kuwa na nguvu kubwa kifedha.

Mara ya kwanza kupata nafasi ya kucheza mashindano ya kimataifa ilikuwa msimu 2019 Kombe la Shirikisho Afrika iliishia hatua ya awali kama ilivyokuwa misimu miwili mbele 2020 na 2021 waliishia hatua hiyo hiyo.

Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huu ndio unakuwa wa kwanza kwao kucheza baada ya kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu ya Djibouti na wataanza katika hatua ya awali.


WASIKIE KINA SONG

Mwanaspoti lilifika mpaka katika hoteli iliyofikia timu hiyo na kupata dakika moja ya kuzungumza na wachezaji hao kwa uchache kutokana na ulinzi mkubwa uliowekwa hapo pamoja na katazo la mratibu wa timu hiyo.

Song anasema Tanzania ni nchi nzuri, amefurahi kuwa hapa kwani watu wake ni wakarimu na amevutiwa napo.

“Kama ningepata muda wa kuzungumza zaidi ingekuwa vizuri ila nimevutiwa na nchi hii, tumekuja kuweka kambi mahali salama,” anasema Songo.

Kalou yeye anasema: “Tutaendelea kuwa hapa mpaka Septemba, leo (jana) kama imeshindikana kuzungumza ipo siku tutafanikiwa kuna mazuri mengi nitawaeleza, wala msijali.”

“Binafsi natamani kuongea vitu vingi kuhusu ambayo mnahitaji kwani naelewa umuhimu wake na sina shida ila natakiwa kupata kwanza ruhusa kutoka kwa mratibu wetu.”

Mratibu wa timu hiyo, Michel Ayuk anasema bado wapo na wanaweza kutoa kibali maalumu cha kuruhusu kufanya mahojiano kamili katika wiki moja ya mwisho kabla ya kuondoka hapa nchini na kurejea kwao.

“Leo ruksa kusalimiana na wachezaji hawa wawili wakubwa lakini tupo hapa kwa ajili ya maandalizi ya msimu mpya wa kimashindano ya ndani na yale ya kimataifa tunahitaji umakini ili kupata muda wa kutosha kujiandaa vizuri. Kabla ya kuondoka hapa tutaruhusu waandishi kuja,” alisema Ayuk.