SIO ZENGWE: Tuhuma za kubeti Ligi Kuu ni nyepesi, chafuzi

Muktasari:
- Katika msafara huo alikuwepo mwandishi mmoja kutoka Singapore ambaye kwa bahati tulielewana na tulikuwa tukizungumzia sana masuala ya nchi zetu kulinganisha na kile kilichokuwa kinaendelea katika nchi nyingine na hasa kwa wenyeji hao wa Fainali za Kombe la Dunia la mwaka huo.
KABLA ya Fainali za Kombe la Dunia la 2006 nchini Ujerumani, nilipata bahati ya kuwa mmoja wa waandishi wa habari walioteuliwa kwenda kutembelea viwanja na miji ambayo mechi za fainali hizo zingefanyika.
Katika msafara huo alikuwepo mwandishi mmoja kutoka Singapore ambaye kwa bahati tulielewana na tulikuwa tukizungumzia sana masuala ya nchi zetu kulinganisha na kile kilichokuwa kinaendelea katika nchi nyingine na hasa kwa wenyeji hao wa Fainali za Kombe la Dunia la mwaka huo.
Ilifikia wakati katika mazungumzo yetu tukagusia suala la michezo ya kubahatisha ama kamari kutokana na tuhuma kuwa baadhi ya waamuzi waliingizwa katika mtandao wa kamari na wakawa wakichezesha mechi kwa njia ambayo magenge hayo ya kamari yalitaka.
Kulikuwa na mtandao uliohusisha mechi zilizokuwa zikichezwa Kusini mwa Afrika na hasa mechi za kirafiki baina ya mataifa. Uteuzi wa waamuzi ukawa wa ajabu ajabu, kiasi kwamba mashirikisho ya kimataifa yakastukia na kuchukua hatua.
Kilichonishangaza ni hayo magenge yaliyoko Singapore na nchi nyingine za mbali kufuatilia kwa karibu mechi za Kusini mwa Afrika za Mataifa ambayo si tishio katika soka Afrika.
Lakini yule jamaa akanijibu kuwa; “Si timu za taifa za nchi hizo tu, hata ligi zetu zinahusika katika betting,”€ akaniacha mdomo wazi kwa kuwa wakati huo kamari ya kiwango hicho haikuwa imefika Afrika na hasa Tanzania.
Muda mwingi ulipita hadi kamari hiyo ikafika Tanzania na kuenea karibu kila kona ya nchi ikishirikisha zaidi vijana.
Katika kusakanya habari za michezo wiki hii, nilikutana na mjadala mkubwa uliojaa tuhuma zinazoichafua Ligi Kuu ya Tanzania Bara ambayo kwa sasa inashika nafasi ya sita kwa ubora Afrika.
Mjadala huo wa kituo kimoja cha redio ulijikita zaidi katika tuhuma kwamba wachezaji walio katika klabu zinazoshiriki Ligi Kuu pamoja na waamuzi wa daraja hilo wanashiriki michezo ya kubahatisha (betting) kwa lengo la kujipatia chochote kitu, jambo walilolihusisha na matukio ya ajabuajabu uwanjani.
Ilifikia kiwango kwa wachangiaji kuomba Ligi Kuu ienguliwe katika michezo hiyo ili burudani ya kweli irejee.
Nilishikwa na butwaa. Yaani michezo ya kubahatisha imefikia kiwango hiki cha wachezaji na waamuzi kutabiri matukio ya mechi wanazohusika?
Nilijaribu kusikiliza kama kuna mmoja ana ushahidi wa uhakika anaoweza kuuweka bayana ili jambo hilo lifanyiwe uchunguzi na kuwabaini wahusika, sikusikia kitu zaidi ya maelezo kwamba wanawajua washiriki kwa sababu wako nao katika maisha ya kila siku.
Ni suala zito ambalo halitakiwi liachwe lipite kirahisi kwa sababu linatia mchanga kwenye kitumbua kinachozidi kunoga kila uchao. Ufuatiliaji wa mechi za Ligi Kuu unazidi kuwa mkubwa, si ndani ya nchi tu bali hata nje ya mipaka na sasa inavutia wachezaji wengi nyota kutoka hata mataifa ambayo zamani tuliona kuwa ni ndoto.
Simba iliweza kumsajili kipa Ayoub Lakred kutoka Morocco, jambo ambalo zamani lilionekana haliwezekani. Singida Big Stars ilisajili nyota wawili kutoka Brazil, Azam imesajili wachezaji kutoka Colombia, wakati Yanga ilisajili kiungo kutoka Afrika Kusini na mwingine Ivory Coast, wote ni ndoto kuwaona wakiosakata soka katika klabu za Tanzania.
Sifa ya ligi yetu bado inazidi kukua na kampuni zinawekeza mabilioni zikitegemea kuona thamani ya fedha kutoka moja ya Ligi 10 Bora Afrika.
Lakini kama ndani ya ubora huo kuna suala la wachezaji kushiriki michezo ya kubahatisha ya mechi ambazo wanashiriki, kuna uwezekano wa viwango vyote vya ubora kuporomoka kirahisi.
Katika ligi ambayo kila mechi zinapoisha kasoro za waamuzi ndio hutawala mijadala; katika ligi ambayo kasoro za wachezaji na hasa makipa huhusishwa na miamala au uzembe uliopindukia; katika ligi ambayo kipigo cha timu hakichukuliwa kuwa kilitokana na udhaifu wa timu au uzuri wa wapinzani; katika ligi ambayo kushuka kwa kiwango cha mchezaji mmojammoja hakikubaliwi kuwa ni hali ya kawaida ambayo humtokea mchezaji wakati wowote, tuhuma hizi za kushiriki kamari kwa wachezaji na waamuzi zinaweza kuwa kubwa zaidi ya ilivyo sasa.
Kwa hiyo si jambo lelemama kunapoibuka tuhuma kama hizo kwa sababu zinachafua mpira, zinaondoa Ladha, zinaondoa raha ushindi, zinafariji wanaoshindwa kwamba kufanya kwao vibaya kuna mkono zaidi ya uwezo wao.
Katika hali ambayo ingeweza kutia uzito suala hilo, kungekuwa na taarifa kamili ya uchunguzi ambayo ingeibuka bila shaka yoyote tuhuma, ikiwaelezea wahusika wachache, maana hawawezi kuwa wengi, jinsi walivyohusika na mechi zilizoathirika kutokana na ushiriki wao katika kubeti.
Hiyo ingekuwa ni habari kubwa ambayo ingeivuta dunia nzima hapa Tanzania na kulazimisha wahusika kuchukua hatua ikiwa ni pamoja na kufanya uchunguzi wa kina ambao kama ungewatia hatiani, wangeadhibiwa kwa mujibu wa kanuni.
Pamoja na tuhuma hizo bado nyepesi hadi sasa na hazijaweza kuzalisha ushahidi unaoweza kutikisa nchi, kuna jambo ni lazima lifanyiwe kazi mapema kabisa kabla ya Ligi Kuu kugeuka kuwa karaha mbele ya Watanzania na watu wengine duniani,
Nilitegemea uongozi wa Bodi ya Ligi (TPLB) ingetoa tamko siku iliyofuata baada ya mjadala huo ama kukiri kuwa, tuhuma kama hizo zipo na zinafanyiwa kazi au kujisafisha kwa kukanusha jambo hilo au, kuelezea jinsi mifumo yake inavyoweza kudhibiti wachezaji kushiriki kamari hiyo na kutoa matokeo yanayowanufaisha washiriki.
Ingeweza hata kumuomba ofisa katika kampuni hizo za kubeti akutane na waandishi na kuelezea jinsi michezo hiyo inayofanya kazi na inavyoweza kung’amua iwapo mchezaji anabeti kwenye mechi anayohusika, au mwamuzi kuhusika kutabiri matukio ya mechi anayochezesha.
Pamoja na tuhuma hizo kuwa nyepesi hakuna shaka yoyote kuwa zinatia dosari Ligi Kuu na zinaichafua michuano hiyo hata kama hakuna ushahidi dhahiri kuwa kuna waamuzi na wachezaji wanahusika.
Ni kwa mantiki hiyo nilitegemea kuona kiongozi wa Bodi ya Ligi akiibuka kwa ukali kukemea vitendo vyovyote vinavyoweza kuichafua ligi.
Pamoja na yote, hadi sasa tuhuma hizo ni nyepesi kwa kuwa hazijaweza kuthibitishwa kwa ushahidiwa wazi na hazijavuta magenge makubwa yanayoweza kuamua hadi waamuzi wa mechi, lakini zinachafua Ligi Kuu na zinachangia kuondoa ladha.
Ni muhimu zifanyiwe kazi mapema.