SIO ZENGWE: TFF isifurahie ujinga wa Simba, Yanga kuhusu uamuzi mbovu

Ndio! Mahakama zipo kwa ajili ya kushughulikia vitendo vyovyote vya uvunjaji wa sheria. Ndio, na sheria zipo kwa ajili ya kuelekeza ni hatua gani zinafaa kuchukuliwa kwa vitendo fulani vya ukiukaji sheria kwa kuangalia jinsi shauri lilivyojionyesha katika mwenendo wa kesi.

Na zaidi, yapo magereza kwa ajili ya kuhifadhi wale wote ambao wataonekana adhabu yao pekee ni kuishi ndani ya vyumba vyenye nondo na kupoteza uhuru wao kwa kipindi walichopimiwa na mahakama.

Lakini hayo pekee yanatosha kusema serikali isichukue hatua wakati makosa ya aina fulani yanapoongezeka? La hasha. Serikali haiwezi kukaa kimya inapoona mauaji ya watu wa aina fulani yanaongezeka katika jamii. Haiwezi kukaa kimya ikasema watafutwe wakipatikana wapelekwe mahakamani na sheria ichukue mkondo wake! La hasha.

Ni lazima itachukua hatua kwanza kwa kiongozi wake kutoa tamko kali dhidi ya vitendo vya mauaji hayo na kutaka vyombo vinavyosimamia sheria vifanye kazi yake ipasavyo. Na inapoona hali inazidi kuwa mbaya ndipo inafanya uchunguzi kujua sababu za mauaji hayo na ndipo inapogundua kuwa kumbe adhabu pekee hazitoshi kukomesha mauaji hayo, bali kujua chanzo ndio kunaweza kuelekeza dawa halisi ni nini.

Hakuna siri tena kwamba uamuzi, hasa katika Ligi Kuu ya Bara unazidi kuporomoka siku hadi siku. Na maendeleo ya teknolojia yanatupa uwezo wa kujua udhaifu mkubwa wa waamuzi wetu.

Ndio, bado hatujafikia uwezo wa kutumia teknolojia za kisasa kama Video Assistant Referee (V.A.R) ili kuwa na uamuzi sahihi zaidi, lakini ukweli ni kwamba yule mwamuzi wa fainali za Mataifa ya Afrika aliyechezesha dakika 120 bila ya kuitwa kwenda kuangalia marudio ya tukio, unatufanya tuamini kuwa teknolojia ni ziada baada ya ubora wa mwamuzi.

Hakuna mechi inaweza kuisha bila ya V.A.R ya Kitanzania kugundua makosa. Watazamaji wa televisheni, wakiongozwa na wachambuzi, ndio V.A.R ya Kitanzania. Mechi ikiisha tu, unasikia “Ile ilikuwa penalti halali kabisa” au “Ile haikuwa penalti” au “Kosa lilifanyika nje ya eneo la penalti” au “Ule mpira ulishatoka nje” au “Alikuwa kwenye eneo la kuotea kabla ya kufunga” au “Haikuwa offside” au “Kabla ya bao mfungaji alifanya faulo” na mengine mengi.

Bahati mbaya sana, V.A.R yetu haiwezi kumuita mwamuzi aje aangalie marudio ya tukio kutoka pande zote ndipo afanye uamuzi sahihi. Lakini macho yao na maoni yao yanaibua zile kelele za “mbeleko”.

Kila baada ya mechi, wapenzi wa Simba na Yanga huingia mitandaoni, husaka picha za matukio ambayo yanafanana na yale yaliyotokea siku iliyotangulia kwa moja ya timu hizo na “kubalance”. Yaani kama mashabiki wa upande mmoja wanaona timu yao ilinyimwa ushindi kwa kutopewa penalti ya wazi, basi mashabiki wa timu nyingine wataibuka na video za tukio la kunyimwa penalti katika mechi yao iliyopita. Hapo hoja zinakuwa zimeisha.

Hakuna anayekwenda mbali kubaini kuwa kumbe tatizo si kubebwa bali ni ubovu wa waamuzi. Leo Zaka Zakazi, ambaye aliwahi kusema redioni kuwa Azam FC haiwezi kulalamikia matatizo ya uamuzi, anatumikia adhabu ya kutojishughulisha na shughuli zozote zinazohusiana na mpira baada ya matukio ya uamuzi mbovu kufikia kiwango ambacho asingeweza tena kukaa kimya.

Na wapo wengine kadhaa wanaotumikia adhabu kwa kuwakosoa waamuzi. Ingawa wanaoadhibiwa wanatakiwa wawe ni wale wanaowatuhumu waamuzi kuwa uamuzi wao mbovu unatokana na kupewa chochote. Hapo ni kuuchafua mchezo na iwapo wanashindwa kuthibitisha tuhuma zao, basi sheria inatakiwa ichukue mkondo wake.

Lakini kukosoa uamuzi si kosa.

Leo sitaki kutoa mifano kuonyesha jinsi uamuzi unavyozidi kuwa kichefuchefu. Nimeshaandika sana kuhusu ukosefu wa uzoefu kwa waamuzi wetu waliopewa majukumu kabla ya kukomaa kwenye ligi za chini kwa muda wa kutosha.

Ni ajabu kwamba leo hii katika Ligi Kuu unaona mwamuzi msaidizi hawezi kabisa kutafsiri sheria ya kuotea! Kwenye Ligi Kuu? Ligi ambayo ni kioo cha nchi? Ni aibu sana.

Leo hii unamuona mwamuzi anafokeana na wachezaji, amekodoa macho kumuiga Perluigi Colina ambaye ni maumbile yake, anazozana na wachezaji kiasi cha kufikia hatua ya kuwasukuma? Huyu ni mwamuzi kweli? Ni kweli mwamuzi msaidizi kazi yake ni kumsaidia mwamuzi wa kati kuamua, lakini hata tukio lililotokea karibu na mwamuzi wa kati bado asubiri msaada?

Kwa kifupi, hali ya uamuzi ni mbaya na inazidi kuwa mbaya, hasa katika Ligi Kuu ambayo ni kioo cha nchi. Kama katika Ligi Kuu hali ya uamuzi ni hii, vipi huko madaraja ya chini? Kuna haki kweli huko?

Hapo ndipo unapoona kuwa kuna haja ya mamlaka za juu kabisa kuibuka na kuonyesha kutofurahishwa na hali inavyoendelea. Uamuzi mbovu si unawanyima haki waliostahili, bali unapoteza ladha ya mchezo wenyewe, unapunguza heshiamya mchezo, unapunguza hamasa, unakatisha tamaa wawekezaji kama ilivyoonekana kama alivyosema mmiliki wa Gwambina kuwa ni afadhali atumie uwanja wake kufugia ng’ombe kuliko kuendelea kuwa na timu.

Hizi si ishara nzuri. Kamati ya Utendaji ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) haina budi kujitokeza na kutoa tamko kuhusu hali ya uamuzi ili wahusika waanze kuchukua hatua kwenye maeneo yao. Tusisubiri adhabu wanazopewa waamuzi wanaoboronga kuwa zitarekebisha hali hii. La hasha. Kunahitajika hatua za ziada kujua sababu ya ubovu huu wa uamuzi na hatimaye kutafuta dawa sahihi.

Tutawaadhibu sana waamuzi, tutawafungia, lakini watakapomaliza adhabu watarejea wakliwa walewale. Kama matatizo si makubwa, yatosha kuwapeleka kwa kamati yao kujadiliwa na kuchukuliwa hatua zinazofaa ikiwa ni pamoja na programu ya kuwarekebisha.

Lakini kama maamuzi mabovu yamekuwa sehemu ya mechi za kila siku, basi hapo kuna tatizo. Kunahitajika, kwanza tamko la chombo cha utendaji, pili uchunguzi kujua sababu halisi za matatizo hayo.

Tamko la kamati ya utendaji litashtua waamuzi na chombo chao, litarudisha imani angalau kidogo kwa mashabiki kuwa “kumbe huu uamuzi mbovu si maelekezo ya wenye mamlaka” na mzigo kuhamia kwingine.

TFF isibweteke na ujinga wa mashabiki wa Simba na Yanga kubalansi ubovu wa maamuzi katika mechi zinazohusu klabu hizo kongwe.

Uamuzi mbovu uko zaidi kwenye mechi zisizohusisha vigogo hao. Na kwa maana nyingine, mpira unazidi kuharibiki kwa kasi mbaya.

Kwa hiyo ni lazima TFF ianze kuchukua hatua sasa badala ya kubakia ikilalamika kuwa kila kitu kibaya kinaelekezwa kwa rais. Ni kwa sababu mashabiki wanaona pengine rais hakerwi na uamuzi mbovu kwa kuwa hatoi hata tamko kuonyesha hali si nzuri na anapenda uozo huo uishe mara moja.

TFF ikifanya hivyo, mtaniambia kitakachofuata. Mimi niko palee nasubiri!