SIO ZENGWE: Somalia, Comoro wametufikia, kuna nini?

Tuesday August 02 2022
zengwe pic
By Angetile Osiah

JUMAMOSI Timu ya Taifa ya wachezaji wanaoshiriki ligi za ndani ilifanikiwa kuvuka hatua ya kwanza ya michuano ya Ubingwa wa Mataifa ya Afrika (CHAN) kwa kuiondoa Somalia kwa jumla ya mabao 3-1.

Tanzania ilishinda kwa bao 1-0 katika mchezo wa kwanza uliofanyika Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam ikiwa mgeni kutokana na Somalia kwa kuwa haina mazingira mazuri ya kutumia viwanja vya ndani kutokana na mazingira mabovu ya kisiasa ya muda mrefu.

Katika mchezo wa pili, Tanzania ilishinda mabao 2-1, lakini baada ya Somalia kupata bao lao pekee hali ilionekana tete kwa kuwa ingefanikiwa kufunga bao la pili ingeweza kusonga mbele kwa sheria ya bao la ugenini.

Lakini Sopu, ambaye alifunga bao pekee katika mchezo wa kwanza, kufunga bao la utangulizi Jumamosi, akasababisha penalti iliyozaa bao la pili lililoivusha Tanzania.

Matokeo ya 3-1 yanaweza kuonekana kuwa ni kazi rahisi, lakini hali haikuwa nyepesi hivyo. Ni juhudi binafsi za Sopu zilizoipa Tanzania ushindi huo.

Wakati Tanzania ikihangaika, Afrika Kusini pia ilikuwa na kibarua kigumu mbele ya Comoro, ambayo miaka michache iliyopita ilikuwa ni kama baraka kupangwa nayo hatua za mtoano. Huko ndiko hata Mrisho Ngassa alikopata nafasi ya kujulikana Afrika kwa kufunga mabao.

Advertisement

Comoro iliistaajabisha Afrika katika fainali zilizopita za Afcon, ilionekana kama ni juhudi binafsi za kocha wao kusaka Wacomoro wanaosakata soka barani Ulaya kujenga kikosi kilichosumbua fainali hizo, ikiwa ni pamoja na kuibwaga Ghana.

Lakini matokeo ya kikosi hiki cha wachezaji wa ndani walioisumbua Afrika Kusini ni ushahidi tosha kuwa kuna shughuli kubwa zaidi za maendeleo zinafanyika ndani ya taifa hilo la pembe ya Afrika.

Nani zaidi? Wapo Madagascar waliosumbua fainali za Afcon nchini Misri na ambao nao tulidhani mafanikio yao yalitokana na kusaka raia wao walilowea barani Ulaya na kiuwashawishi kurudia uraia wao na hivyo kujenga kikosi bora. Lakini maendeleo yao yanatupa picha tofauti. Leo hii huwezi kuzungumzia Djibout kama ilivyokuwa miaka mitano iliyopita. Alex Song, Ambaye alichezea Arsenal na Barcelona, leo yuko Djibout akichezea timu ya daraja la juu, lakini akiwa na kazi kubwa ya kuwanoa vijana.

Kwa Djibouti, mafanikio katika miaka michache ijayo hayatakuwa zari‚ bali ni maono ya mbali ya viongozi sa soka. Wameamua kujenga misingi ya maendeleo. Ndivyo ilivyo kwa Comoro na Somalia.

Hiyo inamaanisha kuna sehemu ambayo taifa letu lilisimama.

Pengine mafanikio ya klabu kama Simba yanatubwetesha na kutufanya tuyaoanishe na maendeleo ya nchi. Hii si sawa kabisa.

Hata kama Simba imefanikiwa kufika mbali katika michuano ya Afrika ndani ya miaka minne, haimaanisha kuwa soka letu limekua. Ni vipimo tofauti kabisa. Ni sawa na kiongozi wa Chama cha Soka cha Morogoro (MRFA) kujivunia mafanikio ya Mtibwa Sugar kuwa Ligi Kuu kwa fikra kwamba ni maendeleo ya soka mkoa, hali kadhalika kiongozi wa Singida, Mara, Mbeya au Mtwara.

Tunahitaji mikakati ya uhakika kuhakikisha soka la ndani ya nchi linakua badala ya kuhisi kuwa mafanikio ya klabu ni mafanikio ya nchi. Mafanikio ya timu za Comoro, Djibout na Madagascar yanaweka swali kubwa kuhusu maendeleo ya soka la nchi yetu; kwamba tuko palepale hadi walio chini wanatufikia na pengine kutupita au mazingira ya wenzetu yanaruhusu wao kukua?

Tafakari, chukua hatua. Haki elimu!

Advertisement