SIO ZENGWE: Ni sahihi Clement Mzize kutokimbilia Wydad

Muktasari:
- Kila mtu alitaka azungumze japo neno fupi kuonyesha furaha yake kwa kijana wa Kitanzania kupata fursa kwenye ligi ambayo inafuatiliwa na sehemu kubwa duniani, na hasa hapa Tanzania ambako ligi ya soka ya England ni kama ya pili baada ya Ligi Kuu ya Bara.
WAKATI Mbwana Samatta anasajiliwa Aston Villa ya England nchi ilisimama kwa shangwe kuona kijana wake akipata nafasi katika moja ya ligi kubwa duniani na maarufu.
Kila mtu alitaka azungumze japo neno fupi kuonyesha furaha yake kwa kijana wa Kitanzania kupata fursa kwenye ligi ambayo inafuatiliwa na sehemu kubwa duniani, na hasa hapa Tanzania ambako ligi ya soka ya England ni kama ya pili baada ya Ligi Kuu ya Bara.
Hakuna aliyeonyesha kusita au kuhoji muda ambao Samatta alikubali kuhamia England, kwa sababu ilionekana kama ilikuwa ni fursa ya kipekee ambayo kama angeipoteza, asingeweza kuipata tena.
Ndio, inawezekana maana wanasema bahati haiji mara mbili.
Lakini mimi niliona haukuwa muda mzuri kwake kwenda Aston Villa kuziba nafasi ya mshambuliaji wao aliyekuwa ameumia. Kwenda kuziba nafasi maana yake ni kwa muda mfupi wakati mwenye namba akiuguza jeraha. Kuna kazi ngumu ya kumpoteza mara anapopona.
Mwenye namba akishapona na akarudi kwenye makali yake, maana yake yule aliyemshikia nafasi anakuwa ziada na siku zote kinachofuata ni kuonyeshwa njia ya kutokea. Ndivyo ilivyokuwa kwa Samatta.

Hakuwa na jinsi bali kufuata mipango ambayo waajiri wake walimuwekea, yaani kwenda kwa mkopo sehemu nyingine huku wakiweka kipengele cha kununuliwa kama itawapendeza waliomchukua.
Kwa kawaida dirisha dogo la Januari ni la kuziba upungufu uliojitokeza nusu ya kwanza ya msimu, na si kuchukua wachezaji kwa ajili ya mikakati ya muda mrefu kama tunavyofanya huku.
Angalia timu zote barani Ulaya (watu hawapendi kutumia mifano ya Ulaya), utaona ni sehemu ndogo ya wachezaji wanaosajiliwa Januari ambayo hubakizwa na kuwa tegemeo, na hasa wale wanaochukuliwa wakiwa na umri mdogo.
Mchezaji anayesajiliwa na kuwekwa kwenye mpango wa muda mrefu wa timu ni yule anayesajiliwa msimu unapoisha. Pale ndipo klabu inapojipanga kwa ajili ya msimu mzima na hivyo haijasajili kwa ajili ya kuziba mashimo kwa sababu hicho ni kipindi cha usajili mkubwa.
Wachezaji wote nyota duniani husajiliwa wakati wa kipindi hicho, maarufu kwa jina la kipindi cha majira ya joto, au kwa wenzetu huita summer.

Inawezekana wengi wanaona mshambuliaji nyota wa Yanga kwa sasa, Clement Mzize amekoseshwa fursa ya kipekee kwenda kuwa mchezaji wa kwanza wa Tanzania kushiriki michuano ya Klabu Bingwa ya Dunia iliyo katika muundo mpya ambayo itakafanyika Marekani baada ya Yanga kukataa kumuuza wakati huu kwa klabu ya Wydad Casablanca.
Samatta alishaandika historia hiyo ya kushiriki michuano hiyo mikubwa duniani kwa ngazi ya klabu wakati alipokuwa mmoja wa wachezaji wa TP Mazembe waliotwaa ubingwa wa Afrika na kwenda Klabu Bingwa ya Dunia wakati huo ikishirikisha timu nane.
Pamoja na habari kwamba klabu hiyo ya Morocco imeweka dau ambalo halikufikia kiwango kilichowekwa na Yanga, bado viongozi walikuwa sahihi kumzuia Mzize kuondoka wakati huu kwa kuwa hiki si kipindi cha kumuuza mchezaji ambaye ni lulu kwao.
Kimpira, Mzize, kama mmoja wa wachezaji wakubwa nchini kwa sasa, anatakiwa aondoke wakati wa usajili mkubwa ambao utamhakikishia anakuwamo kwenye mipango ya muda mrefu ya mwalimu na klabu kwa ujumla.

Hii itaweza kuwalazimisha Wydad kumvumilia pale watakapoona mchezaji hafikii matarajio yao na badala yake kumweka kwenye programu ya kumnoa afikie kiwango anachokitaka.
Ndivyo ilivyokuwa kwa Emmanuel Okwi alipokwenda Tunisia ambako alishindwa kufikia matarajio ya waajiri wake na hivyo kuhamishiwa timu ya vijana kwa ajili ya kupata uzoefu zaidi kabla ya kurejeshwa kikosi cha kwanza.
Mkataba wa mchezaji anayesajiliwa wakati wa usajili mkubwa huzingatia mambo mengi na humlinda mchezaji tofauti na wale wanaochukuliwa katikati ya msimu tena kwa ajili ya shindano kubwa halafu baada ya hapo kuangalia kama waendelee naye au la.
Uamuzi wa Wydad kumchukua mshambuliaji mwingine Mtanzania, Seleman Mwalimu, unaonyesha jinsi walivyokuwa wanahitaji mshambuliaji katika kipindi hiki. Pengine kwa sababu Seleman ni kinda kwa Mzize anaweza kukaa Wydad kwa muda mrefu iwapo waajiri wake wataona kuona mwanga mbele.
Ni muhimu sana kwa wachezaji na wasimamizi wao kuzingatia mambo mengi wakati fursa kubwa kama hiyo ya Wydad inapotokea na si kufikiria kukamilisha usajili kutokana na dau au nafasi kama hiyo ya kuwa Mtanzania wa kwanza kucheza Klabu Bingwa ya Dunia iliyo katika muundo mpya.
Kama mchezaji ana uwezo na uhakika huo upo, hakuna haja ya kukurupukia mikataba ambayo haitamlinda. Na kibaya zaidi ni nadra sana timu za kanda ya kaskazini kuwa na mchezaji kutoka kanda nyingine kwa muda mrefu, hasa Misri na Morocco.
Tumeshuhudia jinsi wachezaji kutoka kanda hii walivyokatizwa mikataba yao au kuamua kuondoka. Kwa uchache Simon Msuva, Clatous Chama na Tuisila Kisinda wamekumbana na utamaduni huo.
Hata Percy Tau ambaye alisajiliwa kutoka Ligi Kuu ya England, bado ameishi kwa kusakamwa na kunyanyasika, ni vile tu makocha tofauti waliridhika naye, lakini wale wachezaji wa zamani wa Al Ahly walikuwa wakimsakama kila uchao hadi ameondoka zake.
Tunataka sana wachezaji wetu wavuke mipaka, lakini wavuke kwa tahadhari ili watumie vizuri vipaji vyao ambavyo hudumu kwa muda mfupi kwenye ajira inayolipa vizuri tofauti na kazi nyingine.