SIO ZENGWE: Kwa nini KMC iwe ya Ruvuma, Ruvu ya Mwanza?

KUMEIBUKA mtindo wa klabu kubadilisha makazi yake kwa sababu ambazo bado hazijaeleweka sana, na ile ya juujuu imekuwa ni kueneza mpira, au kufuata viwanja vizuri na siasa nyingine za ajabuajabu.

Bodi ya Ligi (TPLB), imeweka bayana kwamba klabu za Ligi Kuu Bara zimepwa nafasi ya kuhamisha mechi zao mbili za nyumbani katika mikoa mingine, ndio maana KMC waliipeleka Yanga Majimaji Songea na Ruvu kuihamishia Simba CCM Kirumba, Mwanza kwa mara ya pili mfululizo.

Ni ajabu sana kuona klabu iliyoanzishwa kwa Kodi za Walalahoi wa Manispaa ya Kinondoni, imehamishia mechi zake za nyumbani mjini Songea, Rukwa, yaani imeacha wafadhili wake Kinondoni jijini Dar es Salaam na kwenda kuwaburudisha wakazi wa Arusha!

Vivyo hivyo, Ruvu Shooting ambayo ni klabu ya Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) ambayo imelazimika kusingiziwa kuwa ni ya wananchi wa Ruvu mkoani Pwani ili kukwepa kanuni kali za Leseni ya Klabu, sasa imehamishia makazi yake mkoani Mwanza. Si kwa wananchi wanaosingiziwa kuwa ni yao wa Ruvu, ambao inaelezwa wanaichangia kiasi fulani.

Hiyo haiishii kwa Ruvu na KMC tu, bali klabu nyingi, baadhi zikiwemo za Ligi Daraja la Kwanza, ambayo siku hizi imebadilishwa jina na kuitwa Championship kama wenzetu wa Uingereza baada ya daraja moja kuongezwa bila ya kuwa na kipindi cha mpito.

Hata ile Prisons, ambayo ilianzishwa kama Mbeya Prisons, lakini umiliki wake sasa ni wa jeshi zima la Magereza, sasa imeachana na historia yake na kuhamishia mechi zake za nyumbani mkoani Rukwa. Na hii tabia haiwezi kusimamia hapo; tegemea mabadiliko zaidi kadri siku zinavyokwenda.

Nimejaribu kutafakari sababu hasa za timu kupuuza historia yake na kwenda kuzurura mikoa mingine, ikidharau mashabiki waliokuwa nayo wakati mwingi wa kupambana kupanda daraja au waliounga mkono kwa muda mrefu.

Uwanja wa nyumbani ni moja ya vitu muhimu sana kwa klabu katika kujenga na kuimarisha utamaduni wake, ambao kwa kiasi kikubwa hutengeneza chapa ya klabu na kuifanya ionekane na upekee ambao kwa sehemu fulani huongeza mashabiki na wanachama na hata kuvutia kampuni kuwekeza fedha zake. Utamaduni wa Coastal Union ni tofauti na African Sports na tofauti hiyo ndiyo inayotengeneza ushindani mkubwa kati ya klabu hizo mbili za jijini Tanga.

Ni kama tusi kumwambia shabiki wa Coastal kuwa amehamia African Sports kwa kuwa anajua hawezi kuendana na utamaduni wa klabu hiyo pinzani.

Ndivyo ilivyo kwa mashabiki waliokuwa wa Pan African wanapolinganishwa na wa Yanga, au wa Simba wanapolinganishwa na Red Star, ambayo ilikuwa inaonekana kama tawi la Simba.

Na huwezi ukajenga ushabiki huu kwa timu kutokuwa na uwanja wake wa nyumbani wa kihistoria. Kama Ruvu Shooting inahangaika mikoa tofauti kuchezea mechi zake za kirafiki, haitaweza kujenga wigo mpana wa mashabiki hata kama inashinda vipi au hata ikitwaa ubingwa. Wapenzi wa mpira hawataona kitu fulani ndani ya Ruvu wanachopaswa kujivunia zaidi ya kusikia matokeo ya mechi zake bila ya kujua ipi ilikuwa ya nyumba na ipi ya ugenini.

Ndio wapenzi wa soka wa Mwanza watafurika uwanjani siku Ruvu ikicheza na Yanga au Simba, lakini uwingi huo utatokana na ukubwa wa vigogo hao wakongwe ambao mashabiki wake watajitokeza ama kuona mpinzani wao akiadhibiwa au timu yao ikipata ushindi mnono.

Mechi itakayofuata—labda dhidi ya Mtibwa Sugar—uwanja utakuwa mweupe kwa kuwa hakuna mpenzi wa mpira anayejihusisha na Ruvu Shooting zaidi ya kuishabikia inapocheza na Yanga au Simba, ambazo zimeshajenga utamaduni mkubwa wa kujivunia nyumbani kwao.

KMC, ambayo ni timu ya Manispaa ya Kinondoni imeingia katika utamaduni huo ikichezea fedha za walalahoi wanaokatwa mishahara yao au mapato ya biashara zao.

Ni muhimu kwa klabu kutambua kuwa sehemu ambayo imezaliwa au ilianzishiwa ni muhimu katika historia na utamaduni wake. Kukimbia eneo hilo kwa sababu ya aina yoyote ile ni kukata sehemu ya historian a utamaduni wake na kuanzisha mpya ambao ni vigumu kushika vichwani mwa watu.

Isitoshe timu inalazimika kutumia fedha nyingi kucheza uwanja wa nyumbani na pengine hata kuchelewa kufika kuliko mgeni, hali ambayo nusura iikute Ruvu Shooting wiki iliyopita ilipokuwa mwenyeji wa Simba.

Viongozi wa klabu hawana budi kufikiria kwa kina kabla ya kuamua kwa mihemko kuhamishia mechi za nyumbani kwenye viwanja vya mikoa mingine.

Ni muhimu sana kuheshimu mashabiki, hata kama ni wachache kwa kuwa kufanya hivyo kutawajengea heshima na kuvutia wapenzi wengine wa soka.