Prime
SIO ZENGWE: Injinia Hersi aamshe wenzake kuibadili TPLB

Muktasari:
- Umeonyesha jinsi baadhi ya viongozi wa TPLB walivyolimbikiziwa madaraka, ukiukaji wa kanuni wakati wa kufanya uamuzi, upendeleo wa wazi kwa klabu za Simba na Yanga na ukosefu wa mfumo mzuri wa kufanya uamuzi endapo kutakuwa na dosari.
MGOGORO wa mechi ya mzunguko wa pili baina ya Yanga na Simba ulioibuka baada ya Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB) kuahirisha mechi kinyume cha kanuni, umeweka hadharani udhaifu mwingi kuhusu uendeshaji wa mashindano hayo, usimamizi na ufanyaji wa uamuzi.
Umeonyesha jinsi baadhi ya viongozi wa TPLB walivyolimbikiziwa madaraka, ukiukaji wa kanuni wakati wa kufanya uamuzi, upendeleo wa wazi kwa klabu za Simba na Yanga na ukosefu wa mfumo mzuri wa kufanya uamuzi endapo kutakuwa na dosari.
Lakini kilicho kikuu kati ya yote hayo na TPLB kutokuwa na chombo cha kukisimamia na ambacho bodi hiyo itawajibika. Na Mgogoro huo umeonyesha kuwa TPLB ni kamati tu ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) na si chombo huru kinachomilikiwa na kuwajibika kwa klabu, kama ilivyokuwa malengo ya kuanzishwa kwake.
Ndio maana klabu kama Yanga inaweza kuandika barua kulalamika kuwa haina imani na mwenyekiti wa TPLB, Steven Mnguto pamoja na Ofisa Mtendaji Mkuu (CEO), Almasi Kasongo kwa kuwa wawili hao hawawajibiki kwa klabu zinazounda TPLB, bali kwa TFF kwa hoja kwamba ndiyo yenye mpira.
Wakati klabu duniani zikimiliki ligi zao na hata kuunda umoja wa klabu ili uwe na nguvu dhidi ya uamuzi unaofanywa na vyombo vinavyosimamia mpira, huku klabu zimelala na zinaamini kuwa haziwezi kuwa na nguvu dhidi ya TFF.

Lakini rais wa Shirikisho la Soka Afrika (CAF), Patrice Motsepe ameanza kuzifungua macho klabu za Afrika. Motsepe, ambaye anaimiliki klabu ya Mamelodi Sundowns, anajua machungu ya kuendesha klabu na anajua jinsi ambavyo maamuzi ya vyama na mashirikisho yanavyoumiza klabu.
Kwa kujua hilo, Motsepe na kamati yake ya utendaji wakaamua kuanzisha Chama cha Klabu za Soka Afrika (ACA) ambacho rais wake wa kwanza amekuwa rais wa Yanga, Hersi Said.
Kwa kuwa rais wa ACA, Hersi sasa anaingia kwenye vikao vya Kamati ya Utendaji ya CAF, ambako kazi yake kuu itakuwa ni kuangalia maslahi ya klabu wakati wa kufanya uamuzi kama kuanzisha mashindano mapya, kuunda kanuni za mashindano na mambo mengine kuhusu wachezaji.
Lengo hilo lililomuingiza Hersi katika uongozi wa juu wa soka Afrika halina budi kumfikirisha kuhusu maslahi ya klabu za Tanzania na uendeshaji wa chombo kilichokusudiwa kumilikiwa na klabu, lakini kimegeuzwa mkono wa TFF.

Hersi kwa kutumia uzoefu anaoupata nchi mbalimbali anazotembelea kama rais wa ACA, awazindue viongozi wenzake wa klabu na kuwaeleza umuhimu wa kubadili muundo na umiliki wa TPLB ili iwe ya kisasa, inayowajibika kwa klabu, yenye ufanisi na mfumo mzuri wa kufanya uamuzi.
Kwa chombo ambacho kinawajibika kwa klabu, isingekuwa rahisi kwa rais wa TFF, Wallace Karia kutoka hadharani na kauli kama zile za kukebehi viongozi wa klabu ya Yanga, kulinda viongozi wa TPLB na kusema kutishia kugoma ni kutaka kuiyumbisha TFF, ilhali msimamizi wa ligi ni TPLB.
Wala mwenyekiti wa TPLB asingethubutu kujitokeza hadharani na kusema waziwazi kuwa linapofikia suala la Simba na Yanga inabidi hata kanuni zisifuatwe. Hii ni kuwachukulia viongozi wa klabu 16 za Ligi Kuu kuwa hawana akili na wanaona sawa Simba na Yanga zikipewa upendeleo.

Kwa hiyo ni lazima kutafutwe muundo ambao utawafanya viongozi wa TPLB wawajibike kwa klabu, ambazo kama chombo hicho kingeshafikia hatua ya kuwa kampuni kama ilivyokusudiwa mwanzo, wangekuwa wanahisa wake kama ilivyo kwa ligi nyingine kubwa duniani.
Klabu hazina budi kusimama imara kuibadilisha TPLB ili iwe na mfumo unaowalazimisha viongozi wake waone wana-wajibika kwa klabu na si kwa TFF ambayo haina klabu kwenye ligi hiyo. Na mfumo pekee utakaoweka uwajibikaji wa aina hiyo ni klabu kuwa na sauti sawa katika umiliki, sauti ambayo itazisaidia kuhoji mambo mengi pindi kunapotokea dosari na pale itakapoonekana kuna makosa yanayojirudia basi vyombo husika ndani ya TPLB viweze kuwawajibisha mara moja.
Klabu zikiwa ndio wamiliki wa chombo hicho ni vigumu TPLB kutuhumiwa kuwa inapendelea klabu moja na ni vigumu kutumiwa na klabu moja kama ambavyo kumekuwa na tuhuma kuwa kuna mpango wa kuibeba timu moja msimu huu na kwamba kuna viongozi waliitwa Dubai kwenda kusuka mkakati huo.

Haitakuwa rahisi kwa viongozi wa TPLB kuingia kwenye kashfa kama hizo kwa kuwa itajulikana mapema.
Ligi Kuu ya England kuna kampuni inaiendeshwa ambayo bodi ina wajumbe watano. Wajumbe hao ni mwenyekiti, ambaye siku hizi hutafutwa kwa kuangalia mtu mwenye uzoefu mkubwa katika uendeshaji mashirika makubwa na rekodi nzuri. Zamani uenyekiti ulikuwa ukienda kwa viongozi wa klabu kubadilishana.
Wengine katika bodi hiyo ni Ofisa Mtendaji Mkuu (CEO), ambaye pia huangaliwa sana sifa zake katika uendeshaji wa taasisi kubwa na si mtu kuteuliwa tu kutokana na mapenzi ya kiongozi mmoja wa TFF.
Wajumbe wengine watatu kwenye bodi hiyo ni wakurugenzi wasiohusika kwenye menejimenti (non-executive directors) ambao huingizwa kwenye chombo hicho kwa ajili ya usimamizi na mipango.
Kwa maana hiyo CEO anakuwa anaongoza menejimenti au sekretarieti yenye watu sita, ambao ni wakurugenzi wa nyanja tofauti kama fedha, masoko, mashindano na kwa siku hizi teknolojia ya habari na mawasiliano ambayo imekuwa ni kitu muhimu sana katika uendeshaji taasisi.

Hapa huwezi kumkuta eti mwenyekiti wa bodi akawa ndio mwenyekiti wa Kamati ya Uendeshaji na Usimamizi wa Ligi, bali mkurugenzi anayehusika na mashindano kwa kushirikiana na watu wengine.
Menejimenti inawajibika moja kwa moja kwa bodi, ambayo kutokana na kuwa na wajumbe huru wasiohusika katika uendeshaji, wanakuwa na uwezo wa kuhoji masuala mengi, ikiwa ni pamoja na mambo kama ongezeko kubwa la ‘makosa ya kibinadamu’ kwa marefa, tuhuma za kuibeba timu moja, ufujaji wa fedha na kama viashiria vya ufanisi vilivyowekwa vimefikiwa kwa kipindi ambacho bodi inakutana.
Na bodi inawajibika moja kwa moja kwa klabu 20 zinazoshiriki Ligi Kuu ya England, ambazo ni wanahisa wa bodi. Hawa ndio wanaoamua kila kitu kuhusu mambo kama kupitisha mdhamini mkuu wa ligi, kuuza haki za matangazo ya televisheni na redio, mgawanyo wa mapato pale taasisi inapoingiza faida.
Kwa hiyo muundo huo wa chombo kama TPLB unaweka uwajibikaji mkubwa katika kila sehemu na kuondoa TFF kuwa na mamlaka hadi ya kuajiri watendaji, kazi ambayo ingefanywa na bodi yenye wajumbe huru na wasioshiriki katika kufanya uamuzi wa kila siku wa uendeshaji ligi.
Hersi hana budi kuwaamsha viongozi wenzake na kuwafikirisha kuhusu muundo uliopo sasa ambao unaweka mazingira ya upendeleo, kutowajibika, kutokuwa na ubunifu, kubweteka na mambo mengine ambayo siku hizi yanapigwa vita katika uendeshaji taasisi.
Ni muhimu Hersi na wenzake waanzie kwenye mgogoro huu kuunganisha nguvu na kuipigania TPLB ili irudishwe mikononi mwao kama ilivyokusudiwa na kuiboresha ili iendeshwe kisasa zaidi.