SIO ZENGWE: Bila mwongozo, uofisa habari utakuwa blabla tu

Muktasari:

ZAMANI ilikuwa inaonekana kama katiba ndio tatizo kubwa la klabu zetu na hata Chama cha Soka nchini, enzi hizo kikiitwa FAT kabla ya kubadilishwa na kuwa Shirikisho la Soka nchini (TFF).

ZAMANI ilikuwa inaonekana kama katiba ndio tatizo kubwa la klabu zetu na hata Chama cha Soka nchini, enzi hizo kikiitwa FAT kabla ya kubadilishwa na kuwa Shirikisho la Soka nchini (TFF).

Hivyo, wimbi la mabadiliko lilipokuja, hoja kubwa ilikuwa ni kubadili Katiba ili iende na wakati, pia kuongeza wigo wa wafanya maamuzi kwa lengo la kupunguza uwezo wa watu kutoa rushwa kwa wajumbe wote wa Mkutano Mkuu.

Ndivyo ilivyofanyika baada ya mkutano mkuu kukubali kuongeza idadi ya wajumbe kwa kushirikisha vyama vya Waamuzi, Makocha, Wanasoka wa zamani na Soka la Wanawake.

Pia kuliongezeka wajumbe wengine ambao ni wawakilishi wa klabu kutoka kila mkoa na wajumbe wa mkutano mkuu, hivyo idadi ya kuongezeka kutoka 70 hadi 140 kama sikosei.

Na uchaguzi uliofuata, Alhaji Muhidin Ndolanga, aliyekuwa amekalia kiti hicho tangu mwaka 1992 na Michael Wambura, aliyeibukia kuwa na nguvu kubwa ndani ya mkutano huo wakaanguka.

Kipindi kilichofuata kilikuwa cha Leodegar Tenga kujenga taasisi ndani ya soka kwa kuanzisha vyombo mbalimbali vya maamuzi, kutengeneza michakato ya kufanya maamuzi, kutengeneza sekretarieti na kuelimisha majukumu ya kila chombo katika eneo lake na mengine mengi.

Hapa tuliona kama tumeshafika, lakini safari ilikuwa bado ndefu kwa kuwa mpira unabadilika kila siku, teknolojia inabadilika, tabia za watu zinabadilika na hivyo kulihitajika kazi kubwa zaidi. Katiba yenyewe haikutosha kuuweka mpira wetu kwenye njia sahihi, bali pia kulihitajika utayari wa watu kuiheshimu na kuwa wabunifu zaidi katika kuunda sharia zinazotokana na ibara za Katiba ili kutengeneza mazingira mazuri zaidi.

Kilichofuata baada ya Tenga kina mengi ya kusimulia. Marejeo yamekuwa mengi badala ya kuendeleza pale alipoachia. “Mbona wakati wake kulikuwa na hili na lile,” ndivyo kauli nyingi zinavyosema, badala ya kwamba “yeye aliishia pale, sisi tumeendeleza kwa kufanya haya na haya.”

Mfano, suala la Leseni za Klabu liliingizwa katika Katiba, lakini hadi leo limebaki kama lilivyo. Hakuna kamati au jopo lililoundwa kwa ajili ya kutengeneza kanuni zinazoendana na kiwango chetu cha maendeleo na hali yetu ya kiuchumi ili kufuata vizuri Leseni za Klabu, suala ambalo lina mambo makuu matano; michezo, miundombinu, utawala na wafanyakazi, fedha na sheria.

Hata vyombo vya kusimamia utoaji wa leseni za klabu kwa angalau vigezo vya hali yetu, bado havijaundwa. Yaani chombo cha kwanza cha utoaji leseni na cha rufaa.

Haya yote ni lazima yatengenezewe kanuni ili yaanze kufanya kazi vizuri. Naelewa TFF imenakiri mwongozo uleule wa CAF na kuubandika muhuri kuwa ni kanuni zake, lakini sijaona kitu tofauti kinachohusu uendeshaji wa ndani ambao ni tofauti na nchi nyingine.

Leseni za Klabu pia zinazungumzia wafanyakazi. Hapa ndipo nilipotaka kugusia leo. Wakati fulani Shirikisho la Soka Afrika (CAF) lilitoa mwongozo wa jinsi maofisa habari wa klabu wanatakiwa wafanye.

Lakini ule mwongozo unahusu michuano ya klabu barani. Maana yake ukiukogesha jimbo, unaweza kusaidia sana kutengeneza mazingira ya ufanyaji kazi wa watu hawa.

Kwa jinsi hali inavyokwenda, kuna umuhimu wa TFF kuchomoa kipengele hicho cha maofisa habari na kukipanua zaidi ili kiwe na ufanisi katika uendeshaji wa klabu zetu na soka kwa ujumla.

Leseni za klabu zinataka wafanyakazi wote katika sekretarieti wawe professional, kwa maana wawe na weledi katika kazi yao. Na wapate mafunzo kutoka kwa mtoaji leseni ili wafanye kazi kwa mujibu wa utashi wa mpira wa miguu.

Najua hiki hakifanyiki na kikifanyika, klabu hutuma wasiohusika na hivyo mafunzo kutofanikiwa.

Hili ni suala muhimu sana kwa sasa kwa kuwa klabu zimeamua kuchukua watu wanaoweza kuzungumza sana kuwa ndio maofisa habari, badala ya wale wanaoweza kumudu majukumu yaliyoandikwa katika Leseni za Klabu.

Katika ulimwengu huu wa maendeleo ya teknolojia, ulimwengu wa mitandao ya kijamii, ni lazima kuwe na mwongozo wa utendaji kazi wa maofisa hao, sit u katika mikutano yao na wana habari, bali hata kwa mambo wanayoposti katika mitandao ya kijamii; iwe akaunti zao binafsi au za klabu kwa kuwa ni ngumu kumtofautisha mtu na kazi yake.