SINDELAR: Aliyewadhalilisha manazi huko Austria ndani, nje ya uwanjani
Muktasari:
- Hata Tanzania alikuwepo Mathias ambaye watu wa umri mkubwa humueleza siyo kama mchezaji mzuri tu, bali mmoja wa watu walioitetea vyema nchi hii katika michezo ya kimataifa wakati ule. Huyu ni Mathias Kissa wa Cosmopolitan ya Dar es Salaam na kikosi cha Tanganyika ambaye aliiaga dunia Juni 25, 2013 akiwa na miaka 84.
KATI ya miaka ya 1950 na 1970 miongoni mwa majina ya wachezaji wa kandanda yaliyopendwa na mashabiki wa mchezo huo hapa nchini Tanzania lilikuwa la Mathias. Hii ilitokana na kuwepo wachezaji wachache katika nchi mbalimbali wenye jina hilo ambao waliwika na mashabiki wa kandanda katika nchi nyingi kuwapenda huku habari zao zikitawala katika magazeti na vipindi vya michezo vya redio.
Hata Tanzania alikuwepo Mathias ambaye watu wa umri mkubwa humueleza siyo kama mchezaji mzuri tu, bali mmoja wa watu walioitetea vyema nchi hii katika michezo ya kimataifa wakati ule. Huyu ni Mathias Kissa wa Cosmopolitan ya Dar es Salaam na kikosi cha Tanganyika ambaye aliiaga dunia Juni 25, 2013 akiwa na miaka 84.
Nakumbuka kumkuta mchezaji huyo katika Klabu ya Cosmopolitani mwanzoni mwa miaka ya 1990 akisikitika kuiona imeporomoka na mashabiki wengi na wachezaji mashuhuri walikuwa wanakimbilia Yanga, Simba, Pan na Nyota Nyekundu. Mathias Kissa aling’ara katika michuano ya Kombe la Taifa wakati ule ikiitwa Kombe la Sunlight Cup lililotolewa na kampuni ya Gossage ya England.
Kampuni hiyo ilikuwa inatengeneza sabuni kupitia kampuni yake ndogo ya Unilever ambayo miongoni mwa sabuni ilizotengeneza zinaitwa Sunlight (Mwanga wa Jua).
Mathias wa Tanzania alicheza kama beki imara pamoja na wachezaji mashuhuri waliong’ara wakati ule kama Yunge Mwanansali, Afande Edwin Akutende, Hamisi Penda na Nasib Mwambe.
Mathias ambaye alipata tuzo ya mchezaji bora wa karne kwa Tanzania Bara alikuwa msomi kupita wenzake walioichezea timu ya taifa na hii ilifanya baadhi ya mashabiki kumuita Msomi. Alikuwa amehitimu elimu ya Darasa la 10. Katika miaka ya karibuni aling’ara Mathias Jensen, mchezaji wa kiungo wa Denmark ambaye alikuja kuwa nahodha wa timu ya taifa na aliifungia mabao 12 katika michezo 36.
Lakini leo nitamzungumzia mchezaji wa Austria, Matthias Sindelar anayekumbukwa kwa ujasiri wa kukataa amri za watawala manazi waliozua balaa la Vita Vikuu vya Pili vya Dunia vilivyoanza 1938 na kumalizika 1945.
Mathias Sindelar alizaliwa 1903 katika mji mdogo wa Kozlau katika ile inayojulikana sasa kama Jamhuri ya Czech ambao wakati ule ilikuwa sehemu ya utawala wa kifalme uliojulikana kwa jina la Austria-Hungary.
Baba yake ambaye alikuwa mtaalamu wa kutengeneza matofali alihamia Austria ambapo ndiko alikozaliwa mama yake ambaye kazi yake ilikuwa kufua nguo na kufanya usafi wa nyumba. Huyu Mathias wa Austria alianza kuonyesha kipaji cha kusakata kandanda wakati akicheza kwenye viwanja vidogo vya mtaani kwao huku akifanya kazi za shuluba baada ya baba yake kuuawa katika mapambano na majeshi ya manazi.
Baada ya kuchezea klabu nyingi ndogo za watoto na vijana alisajiliwa kama mchezaji wa kulipwa 1922. Alipata umaarufu alipokuwa na Klabu ya Viennese ya Austria kuanzia 1924 na kuendelea.
Kwa miaka 15 aliichezea klabu hiyo na timu ya taifa ya Austria kati ya 1926 na 1937. Uwezo wake mkubwa wa kumiliki mpira kupiga chenga na kufunga mabao yasiyotarajiwa ulimfanya atambulike kama mmoja wa wachezaji bora Ulaya.
Lakini, alishindwa kuendelea kusakata kabumbu vizuri baada ya kuumizwa vibaya katika mchezo wa nusu fainali wa Kombe la Dunia 1934. Mwezi Machi 1938 akiwa na miaka 35 majeshi ya manazi wa Ujerumani yaliivamia Austria na timu ya taifa ya Austria kuvunjwa.
Hata hivyo, ulipangwa mchezo wa timu ya wavamizi (manazi) na wale waliotekwa wa Austria. Wachezaji wa Austria walicheza kwa woga, lakini Mathias alikataa kudhalilishwa na aliwapiga chenga za maudhi manazi ambazo ziliwaudhi makamanda wa jeshi lao.
Kabla ya mchezo kufanyika yalikuwepo mazungumzo kuhakikisha mchezo unamalizika sare ya bila kufungana ili kuonyesha urafiki. Lakini, Mathias aliona huo ni upuuzi na kuamua kufunga mabao mawili kinyume na makubaliano jambo ambalo liliwaudhi manazi.
Alipoambiwa kwa nini alivunja makubaliano, alisema manazi ndio walivunja makubaliano ya nchi za Ulaya kuishi kwa amani kwa uamuzi wao wa kuiteka Austria.
Kwa vile Austria wakati ule haikuwa na timu ya taifa aliitwa 1936 kuichezea Ujerumani katika Kombe la Dunia, lakini alisema hawezi kuwa mchezaji anayewawakilisha majahili walioua maelfu ya watu katika vita.
Baada ya hapo alisakwa na majasusi wa Ujerumani, lakini alipata tetesi ya kuwepo njama ya kumkamata na kwenda mafichoni na mkewe mwenye asili ya Kiyahudi. Hata hivyo, Januari 23, 1939 yeye na mkewe walikutwa wameuawa baada ya kushindiliwa matambara yenye sumu midomoni.
Mathias Sindelar ameingia katika orodha isiyozidi watu 10 walioiwakilisha Austria mara nyingi. Aliichezea klabu yake ya Austria, Vienna, michezo 703 na kuifungia mabao 600. Mwaka 2001 aliingizwa katika timu ya karne ya 20 ya kikosi cha Austria.