Yaliyojiri paredi la ubingwa Yanga
Muktasari:
- Hili ni paredi la tano mfululizo kwa timu hiyo, ikiwa imeweka rekodi ya pekee ya kutwaa ubingwa mfululizo kwa miaka ya hivi karibuni.
JANA Yanga iliendeleza ubabe wake baada ya kushangilia ubingwa wao wa tano mfululizo kwa paredi la kibingwa huku likihudhuriwa na mashabiki wengi kutoka kila pande ya jiji la Dar es Salaam.
Hili ni paredi la tano mfululizo kwa timu hiyo, ikiwa imeweka rekodi ya pekee ya kutwaa ubingwa mfululizo kwa miaka ya hivi karibuni.
Yanga ilitwaa ubingwa wa msimu huu baada ya kukusanya pointi 75 mbili mbele ya wapinzani wao wa jadi Simba ambao walifanikiwa kukusanya pointi 73 baada ya kila timu kucheza michezo 30 ya ligi hiyo inayoshirikisha timu 16.
Katika kipindi cha miaka mitano, Yanga imeonekana kufunika kwenye utaratibu wa mzuri wa paredi lao ikiwa ni pamoja na kukusanya mashabiki wengi, mpangilio mzuri, basi zuri na la kuvutia lakini pia mpangilio mzuri wa sehemu ya kuanzia na kumalizia kwa paredi hilo.
MASHABIKI WALALAMIKIA ENEO
Wakati timu hiyo ikisherehekea ubingwa wa Ligi Kuu Bara kwa kufanya paredi jana Jumamosi ya Julai 4, 2026, mashabiki kadhaa wa timu hiyo walionekana kutoridhishwa na utaratibu uliotumika wa maandalizi hayo. Katika maeneo ya Karume jijini Dar es Salaam, ambapo paredi hilo lilianzia, mashabiki hao walionyesha hali ya wasiwazi na kutoridhishwa na maandalizi hayo.
Mashabiki hao walikuwa wakikosoa utaratibu uliotumika kuweka eneo la Karume ambalo wanaamini ni dogo na halina hadhi kwa kuanzisha paredi hilo kama ilivyokuwa utaratibu wa misimu yote inayofanya kikosi hicho kilipotwaa ubingwa.
Kwa misimu ya hivi karibuni, shughuli hizo zimekuwa zikianzia Uwanja wa Ndege wa Mwalimu Julius Nyerere, japo safari hii mambo yamekuwa ni tofauti na inaanzia Karume, ikipita Msimbazi iliko makao makuu ya Simba na kuhitimisha mitaa ya Twiga na Jangwani yalipo makao makuu ya kikosi hicho.
Mbali na hilo, lakini mashabiki hao pia wamekosoa utaratibu wa muda uliotangazwa na kinachoendelea kwa sasa, ambao wanaona ni kutotendewa haki ya kuendana na muda uliopangwa.
Minong’ono hiyo ilijiri baada ya uongozi wa Yanga kutangaza paredi hilo litaanza saa 4:00 asubuhi, ingawa baadaye lilianza saa 7:00, mchana.
MOALLIN, MAX ACHA KABISA
Kaimu kocha Mkuu wa Yanga, Abdihamid Moallin na mchezaji Maxi Nzengeli walikoleza paredi la ubingwa la kikosi hicho, lililoanzia mitaa ya Karume jijini Dar es Salaam. Katika shamrashamra hizo, Moallin aliyeipa taji timu hiyo alionekana akiwa mwenye furaha sambamba na nyota wengine wakiongozwa na Maxi Mpia Nzengeli.
Moallin na Maxi walipanda gari maalumu iliyoandaliwa kwa ajili ya shamrashamra hizo, sambamba na mastaa wengine wakiwemo Mohamed Damaro na Kouassi Attohoula Yao. Wachezaji hao na benchi la ufundi likiongozwa na Moallin walikuwa kwenye gari maalumu lililoandaliwa kwa ajili ya paredi lililoanza saa 7:00 mchana Karume jijini Dar es Salaam zilipo ofisi za Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF).
HERSI ANOGESHA
Rais wa Yanga, Hersi Said aliibua shangwe katika mitaa ya Msimbazi wakati timu hiyo ikiendelea na paredi la ubingwa wa Ligi Kuu Bara iliyochukua kwa mara ya tano mfululizo.
Paredi hilo lilifanyika jana Jumamosi Julai 4, 2026, lilianzia mitaa ya Karume saa 7:00 mchana, ingawa lilipofika mitaa ya Msimbazi saa 8:00 mchana ambapo ndio makao makuu ya watani zao wa jadi, Simba ndipo ilipoibuka shangwe baada ya Hersi kujitokeza na kushangilia na mashabiki wa timu hiyo waliojitokeza kwa wingi.
Hersi aliibuka katika gari maalumu lililoandaliwa kwa ajili ya paredi hilo na kushangalia huku akiwa na makombe matano iliyotwaa timu hiyo ya Ligi Kuu Bara.
Hata hivyo, licha ya Yanga kuteka shoo hiyo kwa kushangilia baadhi ya nyimbo mbalimbali za timu hiyo, ila mashabiki wa Simba hawakuwa nyuma kwani walijibu mapigo na kuimba pia nyimbo za kikosi hicho ukiwemo ule wa Tunda Man wa ‘Simba Tambeni’.
Katika mitaa ya Msimbazi ndipo yalipo makao makuu ya Simba, ambapo Yanga inatumia sehemu hiyo kuwakejeli kila ikifika eneo hilo baada ya kukosa ubingwa wa Ligi Kuu kwa mara ya tano mfululizo.
Hata hivyo kwa kipindi hiki Simba ilionekana kujipanga vizuri ikiwa ni pamoja na kuweka skrini kubwa ambayo ilikuwa inaonyesha bao ambalo lilifungwa na kiungo wao Clatous Chota Chama kwenye mchezo wa Ligi Kuu Bara dhidi ya Yanga, mechi iliyopigwa Uwanja wa Meja Isamuhyo na kumalizika kwa sare ya mabao 2-2.