Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Simba, Yanga mto wenye mamba huvuki kwa miguu

ZENGWE Pict


HUENDA Yanga nayo ikawa imeaga Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya kufungwa bao 1-0 na AS Far Rabat ya Morocco katika mechi ya tano wa Kundi B na kusalia na pointi tano, wakati wapinzani hao katika nafasi ya pili wakifikisha pointi nane.


Kusalia kwa Yanga katika mashindano hayo makubwa kwa ngazi ya klabu kunategemea zaidi maombi. Rabat wana pointi nane na tofauti ya bao moja, wakati Yanga ina pointi tano na tofauti hasi ya mabao mawili, hivyo katika mechi ya mwisho ya nyumbani dhidi ya JS Kabylie ya Algeria, Yanga itahitaji ushindi ambao utategemea pia matokeo ya mechi ya Al Ahly na Far Rabat.


Kadri Wamisri watakavyofunga bao, ndivyo mzigo kwa Yanga utapungua kwa kuwa tofauti ya mabao itakuwa dhaifu kwa Wamorocco, hivyo kuufanya mzigo wa Yanga kuwa mwepesi. Lakini mchezo kati ya Wamisri na Wamorocco haujawahi kuwa mwepesi. Yanga waliweza kubadili matokeo misimu michache iliyopita walipoiadhibu CR Belouizdad kwa mabao 4-0 na kuwapiku katika nafasi ya pili, mwaka ambao Ahly pia alikuwa kundi la Yanga.

Tayari watani wao wa jadi, Simba wameshatolewa kwenye hatua hiyo baada ya kupoteza mechi tatu na kutoka sare mbili na hivyo kushika mkia kwenye kundi ambalo timu ya tatu ina pointi sita.

ZENG 01

Kuna uwezekano Azam FC ikaenda robo fainali baada ya kushinda mchezo wa Jumamosi kwa bao 1-0 na hivyo kufikisha pointi tisa. Hali si nzuri sana kwa Singida Black Stars, ambayo pamoja na Azam FC zinashiriki Kombe la Shirikisho Afrika.

Kufika hatua ya makundi kunaweza kuchukuliwa kuwa ni mafanikio kwa klabu hiyo, hasa Yanga ambayo ilipitisha maazimio kwenye mkutano mkuu kuwa malengo yao mwaka huu ni kufika hatua hiyo, na mengine ni ziada, uamuzi ambao ulikuwa kama kinga.

Si rahisi kuweka malengo mapya kwa kutumia kiwango kilichofikiwa msimu uliopita. Huwezi kuelewa ni kwa nini viongozi waliweka malengo ya kufikia hatua ambayo wameifikia kwa misimu miwili mfululizo badala ya kuweka malengo ya juu zaidi. Sijawahi kuona taasisi inayoweka malengo ya hivyo.

ZENG 02

Simba, ambayo kuelekea msimu uliopita ilisema inajenga timu, ilibadilisha msimamo baada ya kufika fainali ya Kombe la Shirikisho na kujiona kuwa inaweza hata kutwaa ubingwa wa Afrika, lakini mwenendo wake kimataifa na ndani hauonyeshi kuwa inaweza kufikia ndoto hiyo iliyokuwa inaonekana inawezekana misimu minne iliyopita.

Yanga na Simba zimefikia kiwango ambacho sasa zinaona zinaweza kufanya lolote, na zikiulizwa zinatoa mifano ya klabu kubwa za barani Ulaya zilizofanikiwa kwa kufanya uamuzi mgumu wakati mgumu.

Zikiwa zinaelekea hatua muhimu za mashindano hayo ya kimataifa, ziliachana na makocha wake muhimu, kutokana na matokeo mabaya ya mechi za ndani. Yanga iliachana na Romain Folz, wakati Simba iliachana na Fadlu Davids, ambaye alitimka wakati timu ikiwa imeenda ugenini.

ZENG 03

Hii imekuwa kawaida kwa klabu hizo katika misimu kama miwili sasa. Kocha anaajiriwa na kuwekewa malengo ya muda mfupi. Anaanza program zake, huku akiwasoma wachezaji kujua ni nani wataunda kikosi imara kinacholingana na falsafa yake, lakini ghafla kunatokea matatizo na anaonyeshwa mlango wa kutokea.

Anatafutwa kocha mwingine na kupewa malengo yaleyale aliyopewa kocha aliyeajiriwa kabla ya msimu kuanza. Kwa bahati anaanza na matokeo mazuri na inaonekana viongozi walitumia akili sana kumtimua aliyeondoka na kumuajiri wa sasa.

Lakini kwa kuwa anaajiriwa baada ya msimu kuanza na ghafla dirisha dogo linafika, anaachana na baadhi ya wachezaji aliodhani wangemsaidia, naye ananza kazi mpya ya kujenga kikosi wakati timu ikiwa katika kipindi kigumu ndani na nje.

ZENG 03 (1)

Na kwa sababu naye anahitaji muda wa kuingiza falsafa zake vichwani mwa wachezaji, anaangukia pua na kushindwa kutimiza malengo. Msimu unaisha huku viongozi wakisaka kocha mwingine kuridhisha mashabiki na si wa kusaidia kujenga timu.

Kuna klabu zinazofanikiwa kwa kubadilibadili makocha, lakini nyingi hushindwa kufanya vizuri kama Manchester United inavyosumbuka tangu kuondoka kwa Alex Ferguson au Arsenal ilivyosota tangu kuondoka kwa Arsene Wenger hadi kupatikana na Michel Arteta ambaye anaonekana kuituliza.

Bado mpira wa miguu unachezwa na binadamu ambao wanahitaji sana utulivu wa kichwa na utimamu wa mwili. Ni muhimu kuheshimu taaluma ya ukocha na kuachana na kuajiri au kutimua kwa sababu za kisiasa; au kwa ajili ya kuridhisha au kupumbaza mashabiki.

ZENG 05

Lazima kuwe na akili ya kujua kocha fulani anaajiriwa kwa sababu viongozi wameona nini kwake na si kwa sababu anashinda huko anakotoka. Timu inakosa nini ambacho kocha mpya atawapa na itamchukua muda gani kukipandikiza vichwani mwa wachezaji.

Kama tatizo ni dogo linaloweza kutatuliwa na kocha mpya, basi matarajio ni lazima yawe makubwa, lakini kama ni tatizo kubwa ni lazima matarajio yawe ya muda mrefu.

Simba waliona tatizo ni kubwa ndio wakaibuka na falsafa ya kujenga timu, lakini walipata mwalimu sahihi wa kujenga timu? Wana vikosi vya pili vinavyoweza kumpa fursa kocha mpya kuwapeleka wachezaji anaotaka wapate nafasi ili warekebishe kasoro zao huko? Au ni kutimua mchezaji ambaye hapati nafasi na kutafuta mwingine?

ZENG 06

Angalia timu zote zilivyosajili mwaka jana na idadi ya wachezaji walioondoka. Ni lazima utaona kuna tatizo.

Katika mazingira hayo huwezi kutegemea kuvuna mafanikio makubwa wakati kilichopandwa ni kidogo kisicholingana na ukubwa wa timu.

Simba na Yanga zimevuna zilichopanda na hazina budi kuchutama kutathmni zilipokosea na nini kifanyike.