Simba, Yanga hazijawatoa kwenye reli, wanapiga kazi

Thursday April 29 2021
kazi pic
By Olipa Assa

YANGA na Simba ni klabu kongwe zaidi Tanzania. Ndio timu zenye mafanikio makubwa zaidi hadi sasa na kwa miaka mingi zimekuwa zikipokezana kutwaa mataji makubwa nchini na hata kupishana angani katika kusaka mafanikio kimataifa.

Tangu kuanzishwa kwa timu hizi, Yanga (1935) na Simba (1936) zimekuwa na mabadiliko mbalimbali na hata kushuhudiwa nyota kadhaa wakija na kuondoka katika timu hizi, wengine wakiondoka kwa mafanikio, huku wengine wakiondoka patupu.

Wapo wanaomaliza mikataba yao na wengine kuamua kuondoka au kupigwa chini kwa maana ya kutupiwa virago vyao kutokana na viwango vyao kuaminika vimeshuka na si rafiki kwa timu hizo.

Hata hivyo, kutemwa kwao katika timu hizo hakukuwakatisha tamaa, kama ilivyo kwa msimu huu wa 2020/21 kwa baadhi ya mastaa waliotesa Yanga na Simba kwa misimu kadhaa nyuma kabla ya kutemwa na sasa wanawasha moto kwengineko.

Ni kutokana na kuwepo kwa imani kwa baadhi ya mashabiki na wadau wa soka, mchezaji yeyote atakayetemwa na klabu hizi kongwe, huo ndio huwa mwisho wao kisoka na wanakokwenda wanapotea kabisa.

Mwanaspoti limewafuatilia nyota kadhaa waliotemwa na klabu hizo na mzimu huu wa 2020/21 wanafanya yao na baadhi yao wamekuwa tegemeo kwenye vikosi vya kwanza katika timu zao mpya.

Advertisement


ANDREW VICENT ‘ DANTE’ - KMC

Amekuwa tegemeo katika kikosi cha KMC tangu ajiunge nao akitokea Yanga walioachana naye kabla ya msimu kuanza.

Msimu huu amekuwa mwiba mkali kwa washambuliaji wa timu pinzani hasa Yanga na Simba akicheza nafasi ya beki na kuthibitisha kutemwa kwake na Wanajangwani hakukuwa na maana ameshuka kiwango na huko aliko ni moto kutokana na uzoefu alioupata Jangwani.

Uimara wake pamoja na kikosi chao msimu huu, umeifanya KMC hadi sasa kukamata nafasi ya tano kweny6e msimamo ikiwa na alama 40 baada ya mechi 27.


KELVIN YONDAN - POLISI TANZANIA

Wengi waliamini atadumu na Yanga hadi mwisho wa soka lake kutokana na kuitumikia kwa muda mrefu akitokea Simba.

Hata hivyo, kandarasi yake Yanga iliisha mwishoni mwa msimu uliopita baada ya kushindwana kimasilahi na Wanajangwani.

Kwa sasa Yondani anakipiga Polisi Tanzania baada ya kukaa nje kwa muda hadi alipotua hapo kwenye dirisha dogo la usajili msimu huu.

Cotton kama anavyoitwa beki huyu kisiki ameimarisha ulinzi akisaidiana na chipukizi aliwowakuta na kiwango chake msimu huu kimemrudisha timu ya Taifa, Taifa Stars chini ya Kim, kilichokuwa kinajiandaa na kufuzu Afcon na kilicheza dhidi ya Libya (walishinda 1-0, Uwanja wa Benjamini Mkapa) baada ya kutoka kuchapwa na Guinea ya Ikweta bao 1-0.


ALLY SONSO - KAGERA SUGAR

Alitokea Lipuli akatua Yanga alikokaa kwa msimu mmoja kabla ya kutemwa na kutua Kagera.

Kiwango chake akiwa Lipuli kilimfanya acheze hadi Taifa Stars chini ya Kocha Etienne Ndayiragije.

Alidumu Yanga kwa msimu mmoja kabla ya kutemwa kutokana na kiwango kushuka lakini kwa sasa ameonekana kuimarika akiwa na Kagera.

Kocha mpya wa Kagera Sugar, Francis Baraza ndiye aliyeanza kumwamini kwenye mechi ya kwanza akichukua mikoba ya Mecky Mexime, na amekuwa akitumika kwa dakika zote 90 katika mechi tatu za kwanza na kuonyesha kiwango dhidi ya Mbeya City, Mtibwa Sugar, Simba na mchezo wa juzi Jumatatu dhidi ya Biashara United licha ya kichapo cha mabao 2-1.


RAFAEL DAUDI - IHEFU

Kwa sasa ametua Ihefu baada ya kucheza Yanga kwa misimu kadhaa kabla ya kutemwa.

Msimu huu ameonyesha kiwango bora chini ya kocha mkuu Zuber Katwila, na hadi sasa amefanikiwa kufunga mabao mawili baada ya kujiunga nao kupitia usajili wa dirisha dogo na kuonyesha wazi hakushuka kiwango licha ya Yanga kumtupia virago.


JAFARY MOHAMED - NAMUNGO

Namungo inashiriki michuano ya Afrika ikiwa Kombe la Shirikisho. Ingawa kwa sasa haifanyi vizuri na inashika nafasi ya mwisho kwenye kundi lao D, lakini Jafary ameonyesha kiwango bora.

Aliondoka Yanga kwa kukosa nafasi kikosi cha kwanza na kushuka kiwango na Namungo kuona ana kitu na kumsajili dirisha dogo na sasa anatesa akienda kimataifa na Ligi Kuu na hakosi namba kikosini.


HARUNA SHAMTE - NAMUNGO

Haikuwa mwisho wa kuonyesha uwezo wake baada ya kutemwa Simba, amekuwa mchezaji tegemeo kwenye kikosi cha Namungo ambacho kimecheza Kombe la Shirikisho Afrika kwa msimu huu na kimefanikiwa kutinga hatua ya makundi, Shamte akiwa miongoni mwa wachezaji waliotoa mchango wao.


SHIZA KICHUYA - NAMUNGO

Anacheza mara kwa mara katika kikosi hicho, ingawa hajawa kwenye kiwango ambacho alikuwa tishio kwenye kikosi cha Simba kabla hajauzwa Misri.

Alichemka huko Misri akiwa na Pharco FC kabla ya kutolewa kwa mkopo ENNPI na kote alichemka kabla ya kurudi Simba ambako hakukaa sana na kutua Namungo ambako ameonyesha kiwango kizuri.


CHARLES ILANFYA - KMC

Ni mchezaji tegemeo KMC iliyomsajili kupitia dirisha dogo akitokea Simba alikoonyesha kiwango ambacho hakikuwaridhisha mabosi wa timu hiyo na kuamua kumtema kabla ya kutua KMC dirisha dogo la usajili na hadi sasa amefanikiwa kufunga mabao matatu.


YUSUPH MLIPILI - KAGERA SUGAR

Anapata muda wa kucheza Kagera akiimudu beki ya kati tofauti na alivyokuwa Simba na alikalia mechi mbele ya Pascal Wawa na hivyo kuamua kuondoka kwenda kuonyesha makali yake kwengine.

Advertisement