Simba yaipoteza Yanga, Azam

Thursday July 15 2021
simba pic
By Clezencia Tryphone

SIMBA licha ya kufungwa na Yanga msimu huu, lakini imeendeleza ubabe na kuipoteza katika mbio za mfungaji bora.

Upinzani huo kwa sasa umeibuka ndani ya Simba na Azam FC ambazo wachezaji wao wanachuana kuwania kiatu cha dhahabu huku Yanga wakiangukia pua.

Licha ya ligi kuwa na timu 18 lakini vita hiyo iko kwa timu hizo pekee kutokana na kuwa na idadi ya nyota ambao wakimaliza michezo miwili iliyosalia huenda mmoja akaibuka kinara.

Kwenye mbio hizo Simba ina wachezaji watatu Azam wawili huku Gwambina akiingiza mmoja wakati Yanga haina hata mmoja katika nyota sita wanaowania kiatu hicho.

Nahodha wa Simba, John Bocco anaongoza usukani wa mabao akifunga 15 hadi sasa huku Prince Dube wa Azam akifunga mabao 14, Chris Mugalu wa Simba akiwa na mabao 13.

Wengine ni Mrwanda Meddie Kagere (Simba) mabao 11, Iddy Nado (Azam) mabao11 na Meshack Abraham (Gwambina) mwenye mabao tisa.

Advertisement

Katika mbio hizo imeonekana Kagere itakuwa ngumu kutetea taji hilo kutokana na idadi ya mabao yake, pia amekuwa sio chaguo la kwanza kwa kocha wake Didier Gomes.

Kushindwa kuonekana katika michezo mingi ambayo Simba imecheza, huenda ndiyo sababu kubwa iliyopelekea akose nafasi ya kutetea kiatu chake alichokitwaa mara mbili mfululizo.

Kagere ameshindwa kutimiza ndoto yake baada ya msimu uliopita kumaliza na mabao 22 huku msimu huu akishindwa kufurukuta.

Advertisement