Simba ile, Yanga hii...

MABINGWA watetezi wa kombe la Shirikisho (ASFC), watakuwa na kibarua kigumu Jumamosi kwenye Uwanja wa CCM Kirumba Mwanza dhidi ya watani zao Yanga kwenye mechi ya nusu fainali ya mashindano hayo.
Mechi hiyo itakuwa ya kisasi kwa Yanga kwani msimu uliopita ilipoteza mechi ya fainali kwa kufungwa bao 1-0, lililofungwa kwa kichwa na kiungo, Taddeo Lwanga kwenye Uwanja wa Lake Tanganyika Kigoma.
Simba wanaingia kwenye mechi hiyo wakiwa na rekodi nzuri ya kutwaa ubingwa wa ASFC mara mbili mfululizo ikiwafunga Namungo na Yanga msimu uliopita.
Kwenye misimu hiyo miwili Simba iliyotwaa ubingwa kikosi chao kuna maeneo walikuwa bora hadi kufanikiwa ila kwa sasa mambo yamekuwa tofauti kwao.
Makala haya inakuletea Simba imechukua kombe la ASFC mara mbili mfululizo. Je ubora wa kikosi chao ulikuwa wapi ukilinganisha na kikosi cha sasa ?
BENCHI LA UFUNDI
Wakati Simba inatwaa ubingwa wa ASCF Agosti 2 2020, kwa kumfunga Namungo bao 2-1 kwenye benchi la ufundi kulikuwa na utulivu mkubwa wakati huo walikuwa wakinolewa na Sven Vandenbroeck.
Msimu uliopita iliposhinda dhidi ya Yanga bao 1-0, Julai 25, 2021 kocha alikuwa Gomes Da Rosa aliyetoka kuwapatia Simba mafanikiwa ikiwemo kuchukua ubingwa wa Ligi Kuu Bara.
Kwenye nyakati hizo mbili Simba kulikuwa na utulivu wa kutosha katika benchi la ufundi na ulichangia mafanikio ya kikosi hicho hadi kutwaa mataji hayo mawili mfululizo.
Msimu huu kwenye benchi la ufundi hadi Simba inaenda kucheza na Yanga hakuna utulivu na amani kama iliyokuwa kwenye misimu miwili iliyopita kuna taarifa nyingi ambazo zinamuhusu kocha wa Simba, Pablo Franco ambazo si njema na zinaweza kumuondoa utulivu wake.
UWEZO WA WACHEZAJI
Wakati Simba inafanikiwa kutwaa mataji hayo kwa misimu hiyo miwili ilikuwa na kikosi chenye wachezaji imara na uwezo wa aina yake kutokana na huduma bora waliyokuwa wanatoa uwanjani.
Msimu uliopita Simba walikuwa na Clatous Chama, Luis Miquissone, Chriss Mugalu, John Bocco, Meddie Kagere na wengineo wengi waliokuwa kwenye ubora wa aina yake ila kwa sasa wana story nyingine tofauti.
Yule Chama aliyekuwa bora si huyu wa sasa kama ilivyo kwa Mugalu, Kagere, Bocco huku wakiwa na pengo ambalo halijazibwa hadi sasa tangu kuondoka kwa Miquissone.
Kikosi cha Simba wakati huu wachezaji wengi wameshindwa kuonyesha makali yao ukianza na wale waliokuwa msimu uliopita na hata waliyoingia msimu huu kama, Pater Banda, Yusuph Mhilu na wengineo.
KIKOSI KWA PAMOJA
Miongoni mwa silaha nyingine ambayo Simba walifanikiwa nayo ndani ya misimu hiyo miwili walikuwa na kikosi cha kwanza chenye wachezaji waliyokaa kwa pamoja muda mrefu.
Miongoni mwa wachezaji waliokuwa ndani ya Simba kwa muda mrefu wapo, Mohammed Hussein, Shomary Kapombe, Jonas Mkude, Bocco na wengineo lakini kwa sasa hili kwenye kikosi hicho halipo.
Kikosi cha kwanza Simba kwa sasa kina mabadiliko ya wachezaji wengi kwenye kikosi cha kwanza na wameingia, Henock Inonga, Sadio Kanoute, Pape Sakho, Pater Banda na wengine wanaotokea benchi ila wengi wameshindwa kuwa kwenye ubora.
Miongoni mwa wachezaji wapya msimu huu waliyocheza kwa kiwango bora ni Inonga na Sakho ila wengine wote wameshindwa kuonyesha makali yao kama wengi walivyokuwa wakifikilia.
YANGA IMARA
Wakati Simba inatawala na kutwaa ubingwa wa mashindano hayo watano zao Yanga hawakuwa imara kwenye maeneo mengi hadi kushindwa kuwa na timu yenye ushindani wa kutosha.
Ukweli usiopingiza Yanga hawakuwa na wachezaji imara katika kikosi kuna wengine walikuwa kama wanazuga tu kutokana na viwango vyao ambavyo walikuwa wakionyesha kwenye mechi nyingi.
Ukiachana na hilo la kutokuwa na wachezaji imara Yanga hawakuwa na utulivu kwenye masuala ya pesa kuna kesi nyingi za namna hiyo zilisikika na kama haitoshi hawakuwa na watu imara kwenye benchi la ufundi kama ilivyo sasa.
Msimu huu Yanga imeimarika ni ngumu kusikia matatizo ya pesa, matatizo ya uongozi au kwenye benchi la ufundi kila kitu kinakwenda shwari kama kilivyopangwa. Habari njema zaidi kwa sasa Yanga ndio wanatimu bora pengine tofauti na misimu minne iliyopita.
REKODI ZA MAKOCHA
Simba wanaingia kwenye mechi hiyo wakiwa na kocha mkuu, Pablo Franco ambaye ameingoza timu yake kwenye michezo miwili ya dabi na huu ambao watakutana Jumamosi utakuwa wa tatu kwake.
Pablo kwenye mechi mbili alizokutana na Yanga hajapoteza hata moja kama ilivyo kupoteza bali yote miwili ilimalizika kwa suluhu ambayo ilikuwa ya Ligi Kuu Bara msimu huu.
Kwa upande wa Nabi mechi ya Jumamosi inakuwa dabi yake ya sita dhidi ya Simba na amekuwa akipata matokeo tofauti.
Msimu huu Nabi alinza kwa kishindo kwenye dabi ya kwanza ilikuwa mechi ya Ngao ya jamii Yanga ilishinda bao 1-0, ambalo lilifungwa na Fiston Mayele na kuipa timu yake taji kwanza.
Baada ya hapo alikutana na Pablo kwenye mechi mbili za ligi na zote ziliisha bila mbabe kwa wawili hao kumaliza kwa suluhu.
Msimu uliopita Nabi aliiongoza Yanga katika mchezo wa pili wa ligi na Yanga ilishinda bao 1-0, ambalo lilifungwa na Zawadi Mauya ila baada ya hapo alikwenda kupoteza fainali ya kombe la Mapinduzi kwa kufungwa bao 1-0, liliwekwa kambani na kiungo wa Simba, Mganda Taddeo Lwanga.