Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Sikia Mligo alichosema Simba


SIMBA ina mabeki wawili wa kushoto, Antony Mligo na Nickson Kibabage, waliosajiliwa kuziba pengo la Mohammed Hussein 'Tshabalala' aliyetimkia Yanga baada ya zaidi ya miaka 10 Msimbazi.


Mligo ndiye alianza kusajiliwa akitua wakati wa dirisha kubwa la usajili lililopita akitokea Namungo FC, na kuingia moja kwa moja kwenye kikosi cha kwanza, kwani nafasi yake haikuwa na mshindani.

Katika dirisha dogo la usajili lililofungwa mwishoni mwa Januari, Simba ilimsajili Nickson Kibabage kutoka Singida Black Stars kwa lengo la kuongeza nguvu upande huo ambao sasa una mabeki wawili, kila mmoja akihitaji namba ya kuanza kwenye kikosi cha kwanza.

Kama kuna shabiki au mdau wa soka anayefikiri Mligo amechukizwa kuongezewa ushindani, pole yake, kwani mwenyewe ameweka wazi kuwa anapenda ushindani, hivyo ujio wa Kibabage utamuongezea ubora katika kupambania namba kikosini.

Mwanaspoti limezungumza na beki huyo, ambaye amezungumza mambo mbalimbali ikiwa ni pamoja na kufurahishwa na ujio wa Kibabage akisema ushindani ni sehemu ya mafanikio na ubora kwa mchezaji na haukwepeki kwani hata angekwenda timu nyingine nje ya Simba, bado angekutana na changamoto ya ushindani.

USHINDANI, KIBABAGE FRESHI

Wakati Simba ikiongeza nyota mwenye uzoefu katika nafasi ya beki wa kushoto ambayo tayari ilikuwa na Mligo, mwenyewe anasema hakuna kilichoharibika kuongezewa mchezaji eneo hilo, kwani anapenda changamoto.

“Napenda changamoto ya ushindani na ndivyo inavyomfanya mchezaji akue kiuchezaji na kuwa bora. Hivyo, kuongezwa kwa Kibabage kutaniongeza kasi ya ubora kwa lengo la kiushindani kupambania nafasi ya kikosi cha kwanza,” anasema.

“Namheshimu, ni mchezaji mzuri na bora. Naamni atanipa changamoto kwenye ushindani, na hilo linafanikisha maisha. Ukiondoa soka, usikimbie changamoto; ni mwanzo wa nafasi nyingine bora. Sio Simba tu kuna changamoto ya namba. Hata ningetua JKT Tanzania, pia kuna wachezaji na wangenipa ushindani.”

Mligo anasema uwepo wa Kibabage ni chachu kwa klabu na kwao kama wachezaji kujiweka katika nafasi bora, kwani kila mmoja yupo Simba kwa lengo la kuipambania timu kufikia malengo.

“Ujio wa Kibabage ndani ya Simba utaongeza ubora, lakini pia utatoa nafasi kwetu sote kupambana kwa wakati wetu kuhakikisha timu inafikia malengo. Naweza nisiwe bora leo, Kibabage akafanya kazi yake kwa usahihi, lakini pia anaweza asiwe poa, mimi nikafanya kazi ambayo Wanasimba wanaitegemea.”

KUNA WAGENI WANA MADINI

Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), kwa mujibu wa kanuni, limeruhusu klabu za Ligi Kuu kusajili nyota wa kigeni 12 kwa lengo la kuongeza chachu ya ushindani. Beki Mligo anaungana na TFF akisema nyota kutoka mataifa mbalimbali wanaocheza Ligi Kuu Bara wamekuwa sehemu ya ubora wake.

“Faida niliyopata kufanya kazi na mabeki wa kigeni ni kupata nafasi ya kujifunza zaidi na kuwa na hamu kubwa ya kupambana, kwani ushindani unakuwa mkubwa sana,” anasema.

“Mchezaji yeyote aliyesajiliwa kama nyota wa kigeni kwenye nafasi unayocheza, lazima uwe na juhudi ya kupambana ili upate nafasi ya kucheza. Hilo ni faida kwake kuongeza ubora binafsi, lakini pia kupata vitu bora vya kujifunza kutoka kwa mpinzani.”

Mligo anasema wachezaji wa kigeni wamekuwa chachu ya ushindani na sehemu ya mafanikio ya Ligi Kuu kukua msimu hadi msimu, ikiwamo Tanzania kuwa na pointi nyingi za CAF zinazoipa nchi nafasi ya kupeleka timu nne.


TSHABALALA, KAPOMBE VYUMA

Siyo wachezaji wote wana uwezo wa kukubali ubora wa wapinzani wao katika nafasi wanazocheza, lakini kwa Mligo ni tofauti, na hapa anaweka wazi namna anavyomkubali Mohammed Hussein “Tshabalala”, huku akikiri kuwa anatamani kufuata nyayo zake kwa kujitunza na kuwa na nidhamu ya soka.

“Kwa upande wa beki wa ndani, nakusalimia sana. Uwezo wa Tshabalala ni mkubwa; ni beki aliyehudumu kwenye ubora kwa zaidi ya misimu 10 akiitumikia timu kubwa kama Simba. Sio rahisi,” anasema na kuongeza;

“Wachezaji wengi hushindwa kufikia rekodi hiyo kutokana na kuridhika au kulewa sifa. Kwa Tshabalala ni tofauti, kwani ni miongoni mwa wachezaji wenye nidhamu kubwa ya soka. Amekuwa bora kwa sababu anajitunza na anapenda anachokifanya. Natamani kufuata nyayo zake.”

Anasema mbali na Tshabalala, pia anamkubali nahodha wake, Shomari Kapombe, ambao kwake ni mabeki bora wazawa. Amejifunza mengi kutoka kwao, sio ubora wa uwanjani tu, bali pia nidhamu yao ndani na nje ya uwanja.

“Sio rahisi wachezaji kuhudumu kwenye ubora kwa muda mrefu kama ilivyo kwa Kapombe na Tshabalala. Mimi kama mchezaji nina mengi ya kujifunza kutoka kwao na kuyafanyia kazi ili nipite njia zao. Kuonyesha ubora kwa muda mrefu sio kazi rahisi hata kidogo,” anasema Mligo.


SIMBA DAY NJIA BORA

Kuna nyota wengi waliosajiliwa Simba misimu iliyopita na kuibuka kuwa wachezaji wakubwa kupitia tamasha la Simba Day, linalofanyika kila mwaka. Mligo anasema tamasha hilo lilimpa nguvu ya kujiamini.

“Mechi yangu ya kwanza ilikuwa Simba Day. Kwangu ilikuwa kama ndoto, lakini nilijisikia furaha sana kuwa miongoni mwa wachezaji waliopata nafasi kwa mara ya kwanza kuaminiwa,” anasema.

“Kwangu niliicheza kwa ukubwa; ilikuwa mechi yangu kubwa ya kihistoria. Kuanza na mechi ya kimataifa kulinijenga na kunipa imani kuwa nina uwezo wa kuipambania Simba. Nashukuru Mungu nimeaminiwa na ninaendelea kuipambania Simba.”

Mligo anasema kucheza soka la ushindani kunahitaji nidhamu na kuamini kuwa kila kitu kinawezekana. Hicho ndicho kinyago alichovaa, akiamini yupo sehemu sahihi kwa wakati sahihi na atapambana mwanzo hadi mwisho kuipambania Simba ifikie malengo.


KISINDA ALIMLAZA NA VIATU

Tanzania wamepita nyota wengi wa kigeni katika nafasi mbalimbali, lakini Mligo anamtaja Tuisila Kisinda aliyewahi kuichezea Yanga kama winga wa kulia, kwamba ni mchezaji aliyewahi kumpa wakati mgumu.

“Mchezaji niliyewahi kukutana naye na akanipa wakati mgumu uwanjani ni Tuisila Kisinda. Kipindi yupo Yanga na mimi nipo Geita Gold. Alinifanya nione leo kweli kazini kuna kazi,” anasema Mligo na kuongeza:

“Sina maana kwamba wachezaji wengine hawana uwezo, lakini ninachoweza kusema ni kuwa Kisinda alinipa wakati mgumu kutokana na kasi aliyokuwa nayo. Mabeki wengi hatupendi washambuliaji au mawinga wanaokimbia sana.”


KUTUA SIMBA MAFANIKIO

Nyota wengi wa ndani wanaocheza timu za madaraja ya chini, nje ya Simba na Yanga, ndoto yao ni kutua kwenye vilabu hivyo vikubwa, kama anavyothibitisha Mligo.

“Kucheza kwangu Simba ni mafanikio makubwa. Ukiondoa timu niliyopita kama Namungo, Simba, Yanga na Azam ni timu kubwa na za mafanikio. Kila mchezaji anatamani kujaribu bahati na kujitangaza,” anasema.

“Ndoto yangu kubwa ilikuwa kwenda nje ya Tanzania kujaribu soka la kulipwa, lakini baada ya kupata nafasi ya kujiunga na Simba nilifurahi sana na kujipa matumaini, nikiamini safari moja huanzisha nyingine.”

Mligo anasema Simba ni timu kubwa yenye mafanikio ndani na nje ya nchi, hivyo anaamini inaweza kuwa daraja lake la kufikia ndoto ya kucheza soka la kulipwa nje ya Tanzania kupitia michuano ya kimataifa.


SOKA LIMEMPA MAISHA

Soka limekuwa zaidi ya burudani na sasa ni biashara kwa vijana wengi. Mligo anasema soka limempa maisha.

“Pesa yangu ya kwanza ya soka nilinunua kiwanja nikiwa Geita Gold. Soka limenisaidia sana kwenye maisha yangu, lakini faida kubwa zaidi imekuwa ajira,” anasema.

“Siwezi kuweka wazi kiasi nilichopata, lakini niliwekeza kwenye ardhi. Soka bado nalidai, licha ya kupata baadhi ya vitu ninavyojivunia. Ninaendelea kulipambania kwani ndio ajira yangu.”

Anasema hajawahi kushawishiwa kuingia kwenye soka, bali ni mapenzi yake tangu akiwa mdogo. Kama sio soka, hajui angekuwa nani, kwani mpira ndio kitu anachokipenda.


MECHI KUBWA HUONYESHA KIPAJI

Mligo anasema anapenda kucheza mechi kubwa, kwani ndizo zinazowaonyesha wachezaji bora.

“Kumekuwa na kauli kuwa wachezaji wa timu ndogo wakikutana na Simba au Yanga wanakamia. Naomba kusahihisha, hakuna ukweli wa hilo. Kilichopo ni morali kubwa tuliyonayo,” anasema na kuongeza:

“Wachezaji wengi tunapenda mechi kubwa, tunakuwa na morali nzuri ya ushindani na fursa ya kuonyesha uwezo wetu.”

Anasema soka linahitaji morali kuliko maneno mengi, hasa kuelekea mechi kubwa. Ndiyo sababu wachezaji wa timu ndogo huonekana ‘wanakamia’ wanapokutana na Simba au Yanga.

“Licha ya maandalizi kuwa tofauti, kujiandaa kuikabili Simba au Yanga kunahitaji pia kujengwa kisaikolojia na kuwa na morali ya juu, kutokana na kucheza dhidi ya nyota wenye uzoefu na ubora.”

MLIGO NI NANI?

Mligo ni mchezaji aliyeibukia klabu ya Geita Gold msimu wa 2023/2024 kabla ya kuhamia Namungo FC msimu uliopita, ambako aliendelea kufanya vizuri na kuitwa kwenye kikosi cha timu ya taifa ya vijana chini ya miaka 20, “Ngorongoro Heroes”.

Chipukizi huyo alikuwemo kwenye kikosi cha Tanzania kilichotwaa ubingwa wa Mataifa ya Afrika Mashariki na Kati kwa vijana chini ya miaka 20, CECAFA U20, Oktoba mwaka juzi, akibuka mfungaji bora wa michuano hiyo.

Pia alikuwepo kwenye kikosi cha Ngorongoro Heroes kilichoshiriki Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) U20 nchini Misri.

Ndani ya Simba, alikuwa mchezaji mpya wa saba kutambulishwa mwanzoni mwa msimu huu baada ya beki wa kati Rushine De Reuck (29) kutoka Mamelodi Sundowns ya Sauzi; kiungo Msenegali Alassane Kante (24) kutoka CA Bizertin ya Tunisia; winga Mohammed Bajaber aliyetokea Police Kenya na mshambuliaji Mghana Jonathan Sowah kutoka Singida Black Stars. Wengine ni wazawa; viungo Hussein Semfuko (21) kutoka Coastal Union na Morice Abraham (21).