Prime
SI MCHEZO: Navy Kenzo miaka 16 sasa, bado wapo wapo!

Muktasari:
- Navy Kenzo ambao majina yao halisi ni Aika Marealle 'Aika' na Emmanuel Mkono 'Nahreel' jana Alhamisi walisherehekea kutimiza miaka 16 ya uchumba bila ndoa na Mwanaspoti lilibahatika kuongea na mmoja wao na kufunguka mambo kadhaa.
HII ni habari nyingine kutoka kwa wasanii wa muziki wa Bongo Fleva wanaounda kundi la Navy Kenzo, kutimiza miaka 16 ya uchumba bila ya kusikia migogoro ya kuachana wala kugombana.
Navy Kenzo ambao majina yao halisi ni Aika Marealle 'Aika' na Emmanuel Mkono 'Nahreel' jana Alhamisi walisherehekea kutimiza miaka 16 ya uchumba bila ndoa na Mwanaspoti lilibahatika kuongea na mmoja wao na kufunguka mambo kadhaa.
Aika ndiye aliyeteta na mwandishi wa habari hizi na kusema kuwa pamoja na kutimiza miaka hiyo bado hawana mpango wa kufunga ndoa hadi hapo itakapofikia siku iliyoandaliwa na Mwenyezi Mungu.
Aika anasema, kitu kikubwa kwenye maisha yao ni furaha, amani na malezi mazuri ya watoto wao wawili.
"Mimi katika maisha haya kitu kikubwa ninachoangalia ni furaha, amani kwenye familia yangu, pamoja na malezi mazuri ya upendo kwa watoto wetu," anasema Aika na kuongeza;
"Nafurahia sana kutimiza miaka kumi na sita ya uchumba na Nahreel na wala sichukulii changamoto za kutokufunga ndoa, huo mpango haupo kwa sasa hadi hapo itakapofikia siku iliyoandaliwa na Mungu."
CHANGAMOTO VIPI?
Alipoulizwa kama aliwahi kupata changamoto zozote katika uchumba wao, mwanadada huyo akajibu; "Nikisema hakuna changamoto nitaonekana mwongo, hivyo changamoto zipo hasa zile za mashabiki wetu kutaka tufunge ndoa kwa maana tumekaa muda mrefu kwenye uchumba.
"Yaani kila tunapoenda sehemu tukikutana na watu neno ni hilo hilo la kufunga ndoa, kwa kweli hii ni changamoto ambayo kuitatua kwetu ni ngumu sababu watu wanashindwa kuelewa kwamba kwenye uchumba ndio mapenzi yenyewe yalipo na sio kwamba tunashindwa kufunga ndoa au ni waoga wa ndoa kama baadhi ya watu wanavyosema," anaongeza Aika.
SIRI YA MIAKA 16
"Nadhani ni heshima na upendo wa dhati kutoka kwetu, pamoja na kusikilizana, na hata kutokuwa na haraka ya kutaka kufanya jambo fulani, subira ni nzuri sana kwenye uchumba."
Alipoulizwa Nahreel ni mwanaume wa aina gani, Aika anajibu kwa bashasha;
"Kwanza anapenda kula vizuri, pili ana upendo sana na familia yake yaani ni baba bora, tatu mcheshi na mwenye huruma sana na wala sio muongeaji."
Kwa upande wake, Aika anasema yeye ni mtu anayejiheshimu na mpole asiye na makasiriko.
"Mimi napenda kucheza, mpole na nina wivu sana, kukasirika nakasirika kidogo halafu napenda kucheka."
UJUMBE KWA WAPENZI
Aika anasema ni ngumu kuingilia uhusiano wa wapendanao, lakini anatoa ushauri wake hasa wale wanaodumu kwa muda mfupi.
"Siwezi kuwazungumzia sana sababu kila mtu yuko na tabia zake kwenye uhusiano, ila kikubwa waongeze upendo tu. pia wafahamiane kabla ya kuingia katika uhusiano, hii itawasaidia kuishi kwa muda."
ISHU YA MUZIKI
Aika anafichua sababu ya yeye na mchumba wake kutotoa nyimbo mfululizo kama wasanii wengine, lakini bado wanaonekana kuwa imara zaidi katika fani.
"Hatupo kimya sana maana mwishoni mwa mwezi Mei tuliachia ngoma ya 'Your Style'. Ila pia huku kutoachia nyimbo kila wakati ni kutokana na kutaka kujiboresha kwa kila kitu ikiwemo ubunifu, ubora, uimara na maisha yetu kwa ujumla hivyo mashabiki wetu wategemee kupokea vitu vizuri vya ubunifu kutoka kwetu."
ASICHOKISAHAU
"Aisee safari yetu ya muziki, tumepambana sana hadi kufikia hapa tulipo, kuna kipindi tulikosa hela kabisa hadi tukawa tunashinda na njaa, na hii imesababisha sisi wawili kupata vidonda vya tumbo sababu ya msoto," anafichua Aika na kueleza faida alizopata kupitia muziki kwa kusema;
"Nashukuru Mungu tunaishi kwenye nyumba yetu, ambayo tumeijenga kupitia huu huu muziki, hapa ndipo tulipofahamu kuwa kazi ya muziki ukiifanya vizuri na mashabiki wakikukubali basi inakuletea mafanikio makubwa sana, mbali na nyumba pia tulinunua magari kupitia muziki."
KOLABO ANAYOTAMANI
Aika anapoulizwa anatamani kufanya kolabo na msanii gani wa kike nchini, anacheka kwanza kisha anasema;
"Mimi nafanya kazi na mwanamuziki yeyote anayefanya vizuri kwenye tasnia hii ya muziki, maana muziki ni biashara hivyo najua nikifanya na mtu ambaye anafanya vizuri basi itakuwa poa kwenye kupata pesa na naimba wapo wengi wanaofanya vizuri ni suala la muda tu."
NAVY KENZO
Kundi hili lilizaliwa mwaka 2023 mara baada ya kundi la Pah One lililokuwa likishirikisha wasanii wanne akiwamo Aika na Nahreel sambamba na Igwee Damas na Ola More Karisma.
Kundi hilo lilitamba na ngoma kali lakini baadaye lilisambaratika na Aika na Nahreel wanaungana kuunda Navy Kenzo lililokimbiza na ngoma kali zilizowatambulisha kama Chelewa, Kamatia Chini na nyingine kabla ya mwaka 2016 kufyatua albamu ya kwanza iliyooenda kwa jina la AIM-Above in a Minute.
Navy Kenzo liliwahi kutwaa tuzo mbalimbali limewahi kufanya kazi na wasanii mbalimbali wakubwa nchini kama Vanessa Mdee, Diamond Platinumz, Joh Makini, Alikiba, Patoranking na wengine.