Gwiji Bi Mwanahawa aongea mazito

Muktasari:
- Bi Mwanahawa miezi minne iliyopita aliwahi kufanya mahojiano na media moja na kusema anatamani kuacha kuimba ila hali ngumu ya maisha ndio inayomsababisha asiache kuimba.
LEO kwenye safu ya Dakika 5, tumempata Bi Mwanahawa Ally, muimbaji gwiji wa muziki wa taarabu nchini aliyewahi kufanya kazi na bendi mbalimbali za hapa Bongo.
Bi Mwanahawa miezi minne iliyopita aliwahi kufanya mahojiano na media moja na kusema anatamani kuacha kuimba ila hali ngumu ya maisha ndio inayomsababisha asiache kuimba.
Pia alisema anatamani kuonana na Rais Samia Suluhu au mtoto wake anayeitwa Wanu Hafidh Ameir, mbunge wa viti maalumu na mwenyekiti wa taasisi ya Mwanamke Initiative Foundation Zanzibar ili awaambie shida zake za kimaisha.
Hata Hivyo, Mwanaspoti lilipoongea na Bi Mwanahawa kwa njia ya simu akiwa Zanzibar amesema alifanikiwa kuonana na Mh Wanu na kupewa Sh10 milioni ambazo aliambiwa zimetoka kwa Rais Samia Suluhu, jambo ambalo anashukuru sana. Mbali na jambo hilo, haya ndio maongezi ya Mwanaspoti na Bi Mwanahawa Ally anayefahamika pia kama Jembe Gumu.
SWALI: Maradhi gani yalisababisha ukaacha kuimba?
JIBU: Mimi sasa hivi nimeamua kuacha kuimba, kwa sababu naumwa sana miguu, huu ndio ugonjwa wangu mkubwa sana sasa hivi, najua mashabiki wangu wananihitaji ila ndio hivyo tena sitaweza kurudi jukwaani tena.
SWALI: Tukio gani ambalo huwezi kulisahau kwenye maisha yako ya taarab?
JIBU: Nililala mzima nikaamka na majipu kichwani na macho yana vidonda sioni kabisa, mama yangu alikuwa analia kama mtoto mdogo, nikaenda hospitalini na sikujua niliponaje maana mama yangu ndio alikuwa ananihangaikia sana na nilipopona akaniambia niache kuimba, mimi nikawa mbishi tu.
SWALI: Nani aligundua kipaji chako cha kuimba?
JIBU: Watu tu ndio waligundua, baada ya kuona naenda kuimba kwenye vikundi vidogovidogo vya mitaani hapa Zanzibar, ndio wakasema mimi nina uwezo wa kuimba wakanipeleka kwa viongozi wa majukwaa makubwa sababu mimi nimesoma sana madrasa ndio maana sauti yangu iko imara hadi sasa.
SWALI: Unakumbuka wimbo wako wa kwanza kuimba kwenye taarab?
JIBU: Wimbo wangu wa kwanza nakumbuka ulikuwa unaitwa ‘Maisha ya Vijijini’ nikiwa na kundi la Culture Music, huu wimbo ulikuwa unahusu maisha ya jamii maana kipindi hicho kulikuwa hakuna nyimbo za mapenzi ,zilikuwa zinaimbwa nyimbo za Siasa, matukio ya jamanii na vitu vingine lakini sio mapenzi”
SWALI: Unajivunia nini tangu uanze kuimba taarab?
JIBU: Hakuna kitu kingine cha kujivunia zaidi ya kujenga nyumba na hii ni kutokana na uimbaji wetu wa zamani, tulikuwa tunaimba na hakuna pesa, tulikuwa tunaimba kwa mapenzi tu ndio maana hakuna mafanikio.
SWALI: East African Melody ulianza kuimba mwaka gani?
JIBU: Kundi la East African Melody nilianza kuimba mwaka 1995, na ndio kundi ambalo nimeimba nyimbo nyingi pendwa maarufu za taarabu.”
SWALI: Habari zilikuwa zinadai kuwa ulikuwa unachukua pesa za bendi na haudumu kwa muda unaondoka?
JIBU: Sio kweli, kuna baadhi ya bendi walikuwa hawatimizi ahadi zangu, sasa nawezaje kukaa sehemu kama hiyo, walikuwa wananichafua tu hao, mbona bendi nyingine nimedumu kwa muda mrefu!
SWALI: Unakumbuka umeimba nyimbo ngapi?
JIBU: Kwa kweli hapana, sikumbuki maana ni ziko nyingi na hata nyingine majina sikumbuki maana ni muda mrefu sana na wakati mwingine nazisahau hata hata kuziimba.
SWALI: Umepita katika bendi ngapi za taarab?
JIBU: Bendi ni nyingi sana, kwa umri huu nilionao nyingine nimezisahau, unajua mie saa hizi napoteza kumbukumbu kwenye hizi mambo za taarab, ila nakumbuka nilipotoka East African Melody, nikaenda Jahazi Morden Taarab, nikatoka nikaenda Zanzibar Stars, nimefanya pia bendi ya JKU Zanzibar, nimefanya TMK Morden Taarab.
Na sikumbuki kuimba nyimbo za zamani ila za hivi karibuni nikipewa kuimba naimba napo hadi nizisikie yaani kuzifanyia mazoezi”
SWALI: Wimbo wako wa mwisho kurekodi unaukumbuka?
JIBU: Ndio naukumbuka, unaitwa ‘Rabi Nilinde’. Huu wimbo aliutunga marehemu Haji Mohamed nikiwa na kundi la East African Melody na yeye Haji ndiye aliyekuwa mkurugenzi wa bendi hiyo.
SWALI: Ulishawahi kutunga nyimbo?
JIBU: Hapana, sijawahi kutunga wimbo wowote, zaidi ya kupewa tu kuimba.
SWALI: Kitu gani utakikumbuka kwenye taarab?
JIBU: Nitawakumbuka waimbaji wenzangu waliokuwa na upendo, maana sisi wasanii tupo wengi lakini hatupendani, ukiona mwenzako ana kipaji unaenda kumfanyia mambo ya husuda, pia nitawakumbuka mashabiki wangu nilipokuwa jukwaani wanacheza nyimbo zangu na kufurahi na hata kunituza pesa.
SWALI: Wimbo gani unaupenda zaidi tangu uanze kuimba?
JIBU: Wimbo wa Rabbi Nilinde, huu wimbo una historia ya maisha yangu, yaani aliyenitungia huu wimbo ni kama alinitungia mimi na na huwa nafurahi sana nikiwa nauimba.
Zipo nyimbo pia kama Viumbe Wazito, Jitoe Kimasomaso, Roho Mbaya Haijengi, Mwanamke Hulka na Kinyago cha Mpapure. Hizi nyimbo ndio zilikuwa nyimbo pendwa za mashabiki zangu.