Si bure, Mtibwa ina kidudu kinaitafuna!

Muktasari:

  • 1988 Mwaka iliyozaliwa Mtibwa Sugar katika mashamba ya Manungu, Morogoro

UNAIKUMBUKA Tukuyu Stars? Wanabanyambala hawa walishtusha sana Tanzania mwaka 1986. Timu hii ilipanda na kubeba ubingwa wa Ligi Daraja la Kwanza (sasa Ligi Kuu). Ikadumu miaka miwili kisha kushuka daraja. Kwa wanaokumbuka, Tukuyu ilipanda sambamba na RTC Mwanza na Mwadui Shinyanga. Ilikuwa timu moja matata iliyokuwa na wanaume waliokuwa wanaupiga mwingi na wenye vipaji.

Kikosi chao kilichopanda na kutwaa ubingwa ndani ya msimu wao mmoja tu ni; Mbwana Makatta, Chachala Muya, Sekilojoa Chambua, Robert Damian, Muhesa Kihwelo, Ikupilika Nkoba, Gamshard Gamdast, Betwell Africa, Jebby Mohammed, Asanga Aswile, Vincent Buriani, Yussuf Kamba, Costa Magoloso, Jimmy Mored, Salum Kussi, Stephen Mussa, Lumumba Richard ‘Burruchaga’, Kelvin Haule, Godwin Aswile, Peter Mwakipa, Selemani Mathew Luwongo, Caraby Mrisho, Abdallah Shaibu, Peter Mwakibibi, Taisi Mwalyoba, Augustine Mumbe, John Alex, Daniel Chundu na wengineo wengi.

Sitaki kuiongelea timu hiyo ambayo baada ya kushuka wakati huo Coastal Union ikitwaa ubingwa wake wa kwanza na wa pekee wa Ligi ya Bara, huku watani zao, African Sports wakibeba taji la Ligi Kuu ya Muungano, ilipambana na kurudi tena miaka ya kati ya 1990 na kushuka 2004. Na tangu iliposhuka, haijarudi tena katika Ligi Kuu Bara.

Kilichonifanya niiguse Tukuyu ni kutokana na ukweli iliporudi kwa mara nyingine katika ligi hiyo, kuna timu moja nyingine ilikuja kuandikisha rekodi katika Ligi ya Bara.

Naizungumzia Mtibwa Sugar. Timu hii ilipanda daraja hadi Ligi Kuu Bara (enzi hizo Ligi daraja la Kwanza) msimu wa 1995-1996.

Hakuna aliyetishwa nayo. Ni kama ambavyo Tukuyu haikuzitisha Simba, Yanga, Coastal, Pamba au Majimaji zilizokuwa moto kwelikweli enzi hizo. Hata hivyo wao, walimaliza nafasi ya nne katika msimu wa kwanza na wa pili. Kisha ligi ikabadilishwa na kuwa Ligi Kuu ikamaliza ya nane, lakini msimu uliofuata ikabeba ubingwa, japo ulijaa mizengwe baina yao na watetezi Yanga.

Katika kuthibitisha kuwa, taji lao la kwanza halikuwa la kubahatisha kama ilivyokuwa ikibezwa baada ya maamuzi yaliyowanyima Yanga kuitetea taji kwa mara ya nne mfululizo, msimu wa 2000, Mtibwa ilitetea taji hilo na kuandika rekodi ambayo bado haijafutwa kwa klabu zilizo nje ya Simba na Yanga. Hakuna klabu yoyote nje ya vigogo hao, waliowahi kutetea ubingwa wa Bara, lakini Mtibwa iliweza. Chini ya Kocha John Simkoko, aliyeirejeshea makali KMC kwa sasa katika Ligi Kuu Bara ndiye aliyefanya jambo hilo. Na tangu ilipopanda na kufanya yake katika ligi hiyo, huku pia ikinyakua mataji kadhaa ikiwamo ya Kombe la Mapinduzi, Kombe la Tusker, Mtibwa haijawahi kushuka daraja. Hii ina maana ni moja ya klabu zilizodumu kwa muda mrefu baada ya Simba na Yanga kwa timu zinazoshiriki ligi ya msimu huu. Imedumu kwa miaka kama 25 katika ligi hiyo.

Sio kushiriki tu, lakini ndani ya ligi hiyo, Mtibwa imewahi kutoa Mfungaji Bora wa ligi hiyo mara mbili, wa kwanza akiwa Abubakar Mkangwa, mshambuliaji moja aliyekuwa na macho madogomadogo, lakini yanayoona vyema vyavu zilivyo. Huyu alifunga mabao 16, kisha akaja Abdallah Juma aliyekaribia kuifikia rekodi ya Mohammed Hussein 'Mmachinga' aliyeiweka wakati Mtibwa ikitwaa taji lake la kwanza yaani 1999.

Mzanzibar huyo alifunga mabao 25 msimu wa 2006, bao moja pungufu na yake ya Mmachinga, aliyeweka rekodi ambayo imeshindwa kuvunjwa mpaka leo, licha ya kuibuka na kupotea kwa mastarika wakali kutoka nje ya nchi na wazawa.

Mtibwa imetoa wachezaji wengi waliokuja pia kuwa manahodha wa timu za taifa. Utakataa nini, wakati Mecky Mexime, Alphonce Modest na Salum Swedi 'Kussi' ni miongoni mwao. Pia imetoa makipa bora waliotamba Stars na kunyakuliwa na klabu nyingine kadhaa ndani na nje ya nchi. Mtibwa imeibua washambuliaji, viungo na mabeki waliokuwa wakiwatoa mate vigogo na kupigana vikumbo kila msimu kuwasajili. Utakataa vipi wakati mwaka 1998 Yanga ikiwa klabu ya kwanza ya Tanzania kufuzu makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika, iliwatumia wachezaji wenye historia kubwa na Wakata Miwa hao, japo walitokea Simba kipindi hicho. Nawazungumzia Monja Liseki, Shaaban Ramadhani na Alphonce Modest.

Kabla ya ujio wa Azam FC, Mtibwa Sugar ndio klabu inayoongoza kwa kuzalisha na kuibua vipaji mbalimbali vya soka. Imekuwa ikiwatengeneza wachezaji tangu wakiwa wadogo, kisha kuwauza. Imekuwa ikitunza wachezaji wake na kuwageuza kuwa makocha. Salum Mayanga, Maxime, Zubery Katwila na sasa Vincent Barnabas. Wengine wamekuwa viongozi ndani ya timu hiyo. Pia ni timu ambayo ilikuwa ikizinyima raha Simba na Yanga. Imekuwa ikichangia kuwatimulisha makocha, Sam Timbe, Mganda aliyetua Yanga na kisimati kwa ubingwa wa Kombe la Kagame, alitimuliwa baada ya timu yake kulala Morogoro. Tom Saintfiet naye alitimuliwa baada ya Hussein Javu kuwatia aibu Jamhuri, Morogoro. Simba nayo haikuachwa salama mbele ya Mtibwa. Imeitia aibu mara kadhaa katika mechi mbalimbali zikiwamo za Ligi Kuu na Kombe la Mapinduzi.

Hata hivyo, naanza kupatwa hofu juu ya maisha zaidi kwa timu hiyo ndani ya Ligi Kuu. Nachelea kilichozikuta, Kariakoo Lindi, AFC Arusha, Pamba, Mecco, Tukuyu na klabu nyingine zilipotamba kwenye ligi kuu kisha zikashuka na kushindwa kurudi tena. Na hata zuile zilizopambana kurudi, zilichukua muda mrefu kutimia lengo hilo, lakini zilikaa kwa muda mfupi ndani ya ligi kabla ya kurudi chini na kukwama kimoja.

Kwanini hakuwa na hofu? Mtibwa haivutii kwa sasa. Ni kama kuna kidudu kinaitafuna ndani kwa ndani bila yenyewe kujua. Haina makali ndio maana sio ajabu msimu uliopita iliponea tundu la sindano kushuka. Kama ulidhani ilikuwa imejifunza kitu kwa hali iliyowakuta msimu huu, utakuwa umekosea. Msimu huu wapo unga kinoma! Sio kwa sababu imefumuliwa mabao 5-0 na Simba. Kipigo ambacho kikubwa zaidi kwao kuwani kukipata mbele ya vigogo wa soka nchini, sio tatizo, tatizo ni namna ninavyoiona Mtibwa ikiwa na maisha mafupi kama haitazinduka kutafuta dawa! Kwa namna timu inavyocheza, ni kama iliyokata tamaa na kupoteza matumaini kabisa.

Sio ile Mtibwa ya kila Abdi Kassim 'Babi', John Mabula, Kassim Issa, Kassim Mwabuda, Monja Liseki au Joseph Kaniki kama sio Shekhan Rashid na wakali wengine walioipigania timu uwanjani. Sijajua tatizo ni kocha waliyenaye kwa sasa au aina ya uongozi.

Lakini kama tatizo ni kocha, mbona hata ilipokuwa chini ya Maxime, Mayanga, Katwila na hivi karibuni Hitimana, bado haikutisha kama miaka kadhaa ya nyuma.

Hapo ndipo roho inaponiuma. Sitamani kuiona Mtibwa ikishuka daraja, lakini wa kuiepusha na janga hilo ni wanamtibwa wenyewe, hususani wachezaji. Bado wana muda wa kurekebisha hilo, ili kuepuka aibu ya kuandikwa katika historia ya klabu hiyo, kuwa wao walihusika kuishusha daraja. Hata viongozi wa sasa nao wanapaswa kupambana, ili kusahihisha mambo kisha kujipanga upya kwa msimu ujao, hata kama ni kweli hakuna kilichokuwa na mwanzo kikakosa mwisho. Nitaumia Mtibwa ikishuka daraja msimu huu. Ni kitu yenye umuhimu mkubwa kwa soka la Tanzania kuliko kutwaa kwao ubingwa wa Ligi Kuu au michuano mingine.

Imeandikwa na BADRU KIMWAGA