Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

SHOTI: Kutoka ubaunsa hadi ubingwa wa dunia

NGUMI Pict

Muktasari:

  • Lakini, bado macho ya Watanzania yalihamia nchini Ufilipino ambako ilishuhudiwa Mchanja Yohana akipigwa kwa uamuaiz wa majaji wote watatu katika pambano ambalo halikuwa la ubingwa. Kisha macho yakaelekezwa Saudi Arabia na kumshuhidia Pius Mpenda akitoka sare na Julio Ruiz wa Mexico katika pambano la raundi sita kwenye uzani wa middle.

WIKIENDI iliyopita Tanzania ilikuwa bize kushuhudia mabondia wake wakiwakilisha nchi katika pembe za dunia kupitia mchezo huo ambao unatajwa kuwa ni hatari. Tanzania ilianza kwa kushuhudia mabondia wanne waliokuwa Kenya wakichezea vichapo ambao ni Halima Vunjabei, Maisha Samson, Ally Mulenga na Shabani Kaoneka.

Lakini, bado macho ya Watanzania yalihamia nchini Ufilipino ambako ilishuhudiwa Mchanja Yohana akipigwa kwa uamuaiz wa majaji wote watatu katika pambano ambalo halikuwa la ubingwa. Kisha macho yakaelekezwa Saudi Arabia na kumshuhidia Pius Mpenda akitoka sare na Julio Ruiz wa Mexico katika pambano la raundi sita kwenye uzani wa middle.

Baada ya hapo macho yalielekezwa Romania ambako Mtanzania Lupakisyo Shoti alikuwa na kibarua cha kuwania mkanda wa kimataifa wa IBO katika uzani wa Super Middle dhidi ya mwenyeji wake, Daniel Buciuc.

Shoti ambaye ni maarufu kama Sakuveda King alifanikiwa kumchapa mpinzani wake kwa pointi katika pambano la raundi kumi na kuweka rekodi ya kuwa Mtanzania wa pili kushinda mkanda wa ubingwa huo baada ya Mbwana Mtumla. Mwaka 2006, Matumla alishinda ubingwa huo katika uzani wa Super Fly na kuwa Mtanzania pekee kuwahi kushinda mkanda wa IBF kabla ya bondia Shoti kuvunja rekodi hiyo wikiendi iliyopita nchini Romania.

Bondia huyo mwenye rekodi ya kucheza mapambano kumi akifanikiwa kushinda tisa, akipoteza moja akiwa namba nne kati ya mabondia 39 wa uzani wa super middle nchini wakati duniani akiwa wa 220 katika mabondia 1736 huku akiwa na hadhi ya nyota moja na nusu.

Mwanaspoti limepiga stori na bondia huyo mzaliwa wa Kijiji cha Lungu, Wilaya ya Mbozi mkoani Mbeya kabla ya kugawanywa na kuwa katika Mkoa wa Songwe.

"Binafsi nimezaliwa katika kijiji cha Lungu kilichopo wilaya ya Mbozi mkoani Mbeya, lakini baada ya kugawanywa sasa inajulikana kama Mkoa wa Songwe hivyo mimi ni mwenyeji wa Songwe.

NGUM 01

SWALI: Kitu gani kilikuvutia ukaingia kwenye mchezo wa ngumi?

JIBU: Kwanza kabisa sikuanza kama bondia, guard (baunsa) wa bosi wangu Feyherous ambaye kwa sasa ndiyo kocha wangu na meneja wangu. Sasa kuna muda tulikuwa tunaenda kuangalia ngumi tukawa tunaona mchezo wa ngumi unavyochezwa, mabondia wanavyopigana, bosi wangu akawa ananiuliza jinsi ninavyowaona wanavyopigana na kama nikiingia nitaweza.

Nakumbuka nilimwambia hakuna kitu kisichowezekana kwa sababu nina kawaida ya kuamini kwamba chochote unachokifanya kinawezekana. Kwa hiyo nikamwambia kama tufanya mazoezi tutatoboa, kinyume na hapo ni uongo.


SWALI: Kazi ya guard 'u-baunsa' kwa bosi wako yaani ilianza vipi kwa maana ilikuwa ajira ya kuomba au kutokana na ukaribu wenu?

JIBU: Kazi ya guard nilianza nikiwa natokea kwa Mwarabu Fighter (baunsa wa Diamond Platnumz zamani) na Mwarabu Fighter yeye ndiyo aliniunganisha na Feyherous kwa ajli ya kufanya kazi za guard.

Lakini kulingana na uzoefu wangu wa kazi, nidhamu ilitokea kwa bosi kuvutiwa na mimi baadaye nikatoka kwa Mwarabu Fighter nikawa nafanya kazi na bosi wangu moja kwa moja na hapo ndiyo nilianza mazoezi.

NGUM 02

SWALI: Rekodi inaonyesha umeanza 'direct' kwenye ngumi za kulipwa, kwa maana hujapita kwenye ngumi za ridhaa unadhani ugumu ulikuwa wapi kwako?

JIBU: Unajua kuwa bondia mzuri siyo lazima upite kwenye ngumi za ridhaa japokuwa ni vizuri kupita kwenye ngumi za ridhaa kwa ajili ya kupata uzoefu mapema. Sikupita kwenye ridhaa, ilichangia kupoteza pambano langu la kwanza kwa sababu niliharakishwa kuingia kwenye ngumi za kulipwa nikiwa sina uzoefu wowote.

Binafsi mara nyingi najutia sana kupoteza pambano langu la kwanza kutokana na kuharakishwa maana naamini ningepata muda wa kutosha basi ningefanya vizuri. Nilianza kupigana baada ya miezi miwili tena nilicheza raundi sita. Nadhani kutojua na ugeni ila yote kwa yote tunamshukuru Mungu naendelea vizuri. Naamini mtu ukiamini unachofanya unafanya vizuri siyo lazima upite ridhaa.


SWALI: Unajutia kupoteza pambano la kwanza au kuchafua rekodi kwa kuwa hukupata uzoefu awali?

JIBU: Ni kweli najutia sana kwa sababu nilipoteza kwa bondia ambaye hana maajabu kutokana na kuwa niliharakisha, ndiyo maana nikapoteza, ila kwa maajabu hakuwa nayo zaidi alikuwa tayari na uzoefu wa kutosha. Nashukuru kwamba niliweza kumaliza raundi zote sita licha ya kuwa ni mara ya kwanza.

NGUM 03

SWALI: Vipi kuhusu familia inasapoti hiki unachofanya kwa kiasi gani?

JIBU: Familia inasapoti hasa upande wa baba hakuwa na shida kwa sababu anapenda mchezo wa ngumi, ila changamoto ilikuwa upande wa mama alikuwa hataki kabisa nicheze ngumi.

Unajua yeye alikuwa akiamini ngumi zinasababisha kifo, maana tayari ameshasikia mabondia waliokufa kutokana na mchezo huu, ila nilimuelewesha akaelewa na sasa napata sapoti kubwa ya familia yote.


SWALI: Tangu umeingia kwenye ngumi kitu gani umekutana nacho hakiwezi kufutika kichwani kwako?

JIBU: Kwa upande wangu sidhani kwa sababu vitu vingi nilivyokutana navyo ni vya kawaida sana.

NGUM 04

SWALI: Inasadikika mabondia wa kilo nyingi wanakula sana, kwako ipoje na ipi ratiba yako ya misosi?

JIBU: Kwanza napenda sana kula, ila ninapokuwa naelekea kwenye pambano huwa naondoka kwenye masuala ya kula kwa sababu nashusha sana uzito hata ratiba yangu ya vyakula inapungua. Kutoka kwenye kilo za awali hadi sasa ambazo nimeshuka na kuweza kupata ubingwa natakiwa kujilinda hapa ili nisipate tabu ya kushuka nitakapotakiwa kutetea ubingwa.


SWALI: Kawaida kiwango chako ulaji awali kilikuwa kiasi gani? mfano robo, nusu au kilo?

JIBU: Unajua kwa maisha yetu ya Kitanzania huwa tunakula kumaliza. Unaweza kupika chakula kingi kisichokuwa na idadi, lakini ule umalize. Kwa hiyo mara nyingi nakula kumaliza siyo kula kushiba.

Unajua hata kama inatokea nimeshiba ila natakiwa kula kumaliza kwa sababu sipendi kumwaga chakula, ingawa naweza kuweka makadirio ya kuweza kula nusu (kilo) mchana na nusu usiku hasa upande wa ugali, ila wali sina kipimo maalumu maana nakula sana.

NGUM 05

SWALI: Umekuwa bondia wa pili kutoka Tanzania kushinda IBO baada ya Mbwana Matumla, unalizungumziaje hili?

JIBU: Upande wangu ni jambo kubwa hasa upande wa familia, menejimenti na timu nzima ya Feyherous, pia na taifa langu kwa sababu kupata ubingwa kama huu katika nchi ya watu siyo jambo rahisi kwani pambano lilimalizika kwa pointi mbele ya mzawa. Lakini ni furaha yangu kubwa kwa sababu ni pambano langu la kwanza kwenda nje halafu narudi na ubingwa. Kwangu ni jambo kubwa. Nimeipa heshima nchi yangu nashindwa hata jinsi ya kueleza.

NGUM 06

SWALI: Kabla ya pambano mategemeo ya kushinda yalikuwa kiasi gani maana siyo rahisi ushindi wa pointi ugenini?

JIBU: Katika mapambano niliyopigana hili niliona mapema naenda kushinda kwa sababu nilikuwa nikilala, nikiamka naota ushindi upo mbele yangu na nilikuwa nikiamini nikipata pambano la nje nitarejea na ushindi. Naongea hili Mungu ananiona.

Unajua hili pambano nimeling'ang'ania sana kwenda kulicheza kwa sababu imani yangu ilikuwa inaniambia pambano langu la kwanza kwenda nje nitarejea na ushindi, na Mungu amesimama upande wangu, halijaidhalilisha imani yangu.

Huko nyuma zimekuja ofa za mapambano mengi, lakini meneja wangu alikuwa anazikataa kwa sababu alikuwa anaona bado na mimi ndiyo nililazimisha kutokana na imani yangu ya kuweza kurudi na ushindi. Nilijipanga na kufanya mazoezi sana.


SWALI: Kuna mipango gani ya kutetea kwa sababu siyo mkanda ambao umezoeleka kuwaniwa hapa Bongo?

JIBU: Kuhusu kutetea ni jukumu langu, haliwezi kukwepeka. Natakiwa kuwa fiti muda wote kwa sababu vita ndiyo imeanza kwa kuwa kila mtu atakuwa akiutolea macho. Natetea vipi? Nadhani hilo ni jukumu la menejimenti yangu.

NGUM 07

SWALI: Kwa nini unajiita Sakuveda King?

JIBU: Hilo jina limeletwa kiutani ila mwisho wa siku limezoeleka. Imebidi nilikubali. Sehemu ambayo naishi ndiyo inaitwa Sakuveda sasa watu ambao wananizunguka wakawa wananiita Sakuveda King, ila sidhani kama litadumu sana kwa muda mrefu ikitokea nimehama Sakuveda huenda likaisha kabisa.


SWALI: Watu wa Songwe baada ya kusikia umeshinda ubingwa nje wamesema kitu gani na kuna mpango wa kupeleka ubingwa huko?

JIBU: Songwe wanafuraha sana hasa baada ya kusikia naenda kupigana Romania halafu nimerudi na ushindi furaha yao imekuwa kubwa. Nadhani kwa sasa nasubiri kumalizana na vipengele vya mjini halafu nianze safari ya kupeleka mkanda wa ubingwa wa IBO Songwe wakaufurahie moja kwa moja na siyo kuusikia.