SEHEMU YA TATU - Msuva anawakeraa

STRAIKA Mtanzania Simon Msuva wa klabu ya Wydad Casablanca ya Morocco ameeleza mengi katika mfululizo wa makala haya yaliyofanyika Morocco kabla hajarejea kuungana na timu ya taifa, Taifa Stars kwa ajii ya mechi za kufuzu kwa fainali za Kombe la Dunia dhidi ya DR Congo aliyofunga bao kali la video katika sare ya 1-1, na mechi nyingine dhidi ya Madagascar itakayopigwa leo kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam. Twende pamoja…


ANAOA LINI!

Msuva akiwa nchini Morocco anaishi peke yake na hatujawahi kusikia kama ameoa. Hapa anaeleza jinsi maisha yake ya uhusiano yalivyo akiwa na mchumba wake na watoto.

“Mimi bado sijaoa ila nina mchumba ambaye nimeshazoea kumuita mke wangu, niko naye tunashirikiana katika maisha, niko naye kwa zaidi ya miaka 10 sasa, huenda huyu ndio nikaja kumuoa kama Mungu atatufikisha salama katika ahadi hiyo.

“Mimi nina watoto watatu. Mtoto wa kwanza ni wa kiume anaitwa Godfrey ana miaka 11 sasa, wa pili ni wa kiume pia anaitwa Ibrahim anaenda kuwa na miaka 9 sasa na wa mwisho anaitwa Careen ana miaka minne sasa, ndiye binti yangu pekee.

“Hawa wote sikubahatika kuwapata kwa mama mmoja, kila mmoja ana mama yake, lakini wote niko nao. Hao wawili wa kwanza wanakaa sana na babu na bibi yao na huyu wa mwisho yuko na mama yake ambaye ndiye mwenzangu wa sasa ingawa huwa wanakuja wanakaa naye mama yao hana shida kabisa na anaishi nao kama watoto wake,” anasema Msuva.


ANAWAKEERA

Wakati nikiwa kwa Msuva ghafla anatembelewa na beki mwenzake wa Wydad, Cheick Comara, raia wa Ivory Coast ambaye walikutana ili wanyoe nywele zao kabla ya kwenda kambini na hapa anamuelezea jinsi anavyomfahamu Msuva.

“Msuva ni mtu mzuri sana, anapenda utani na kufurahi, anapenda sana kucheza muziki, akifunga bao hata mazoezini anacheza muziki, wakati huo anakuwa amekupita, inakera sana lakini ndio rafiki yangu, ni rafiki yangu sana tuliingia pamoja Wydad na sasa tuko wote, ila namchukia tukiwa mazoezini ananikera sana, unajua Msuva ana kasi sana na hatulii, mimi kama beki sipendi mchezaji wa namna hii, lakini ndio ananisaidia ili na mimi niwe imara.

“Upande mwingine tukija kwenye mechi ni mtu ninayemfurahia sana anajua kufunga na ana juhudi sana akiwa uwanjani, kuna wakati tuliwahi kukaa benchi pamoja, unaona jinsi anavyoumia kukaa nje na anapoingia uwanjani unaona anafanya vizuri, ni mchezaji bora sana kuwahi kukutana naye,” anasema Comara.


KINYOZI MAALUM

Tukiwa hapo anaingia kinyozi wao ambaye ni raia wa Morocco akija kuwanyoa wakati wakijiandaa kuingia kambini na hapa anaeleza anavyofanya naye kazi ya kupendezesha kichwa chake.

“Huyu ndio kinyozi wangu hapa Casablanca, huyu jamaa nilikutana naye baada ya kuunganishwa na mchezaji mwenzangu ambaye sasa amehamia Berkane, aliponinyoa mara ya kwanza alinipatia, kichwa chake ni rahisi sana kushika na tangu hapo ndio akawa kinyozi wangu, mimi nanyoa kila baada ya wiki mbili na nalipa Dirham 100-150 (Sh25,000 hadi Sh38,000) kila akija kuninyoa na baada ya kuona ananipatia ndio unaona na hawa rafiki zangu nao wakavutiwa na wao anawanyoa,” anasema Msuva.


VAR YAMPA UMEME

Teknonolojia ya kusaida uamuzi kupitia marudio ya televisheni imemuingiza Msuva katika historia ambapo katika maisha yake ya soka yalimfanya kupata kadi ya pili nyekundu katika maisha yake ya soka lakini pia akiwa na kadi mbili tu za njano.

“Tangu nianze kucheza soka la kulipwa nimewahi kupata kadi mbili nyekundu ya kwanza wote mnafahamu kwamba niliipata nikiwa Yanga katika mchezo wa Yanga na Simba na wakati huo akili yangu ilikuwa bado haijakomaa, nakumbuka nilisababishiwa na Nyosso (Juma) alitumia uzoefu wake.

“Kadi ya pili nimeipata hapa Morocco nakumbuka ni kwa hii teknonoljia ya VAR hapa tunaitumia mpaka kwenye ligi, nakumbuka nilionekana nimemkanyaga mtu katika kifundo wakati tunawania mpira, mwamuzi hakuona akaenda kuangalia na kuona hivyo basi nikapata kadi nyekundu.

“Ukiacha hiyo mimi tangu nifike Morocco nina kadi moja tu ya njano na hiyo nayo nilisababishiwa na VAR hiyohiyo ilirudiwa nikaonekana nilimgonga na kiwiko beki mmoja hivi basi nikapata kadi na sikupata kadi nyingine yoyote.”


SALUTI KWA PLUIJM

Msuva anakumbuka wakati akianza maisha Yanga alikuwa akizomewa na mashabiki huku wengine wakimtuhumu kwamba alikuwa na mapenzi na mahasimu wao Simba.

Lakini anasema alionyesha juhidi na kuja kuwa kipenzi cha Wanajangwani kutokana na mabao yake aliyokuwa akifunga na kujituma kwa ajili ya timu.

“Mashabiki walikuwa hawataki kuniona nikikosea, walikuwa wakali, nawashukuru sana makocha watatu katika maisha yangu Ernie Brandts, Hans Pluijm na Minziro (Fred) hawa walinitaka niwasikilize wao, hawakutaka nisikilize nini mashabiki wanachosema,” anasema Msuva.

Usikose sehemu ya mwisho kesho.